Jalada la kesi ya mauaji ya Meneja wa Baa ya Mo-Town
mjini Moshi, James John Massawe, limepotea katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Kilimanjaro.
Massawe aliuawa
Juni 9, 2009 katika Kijiji cha Kindi Kibosho, Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya
kutekwa, jJalada hilo la uchunguzi lilikuwa limesheheni ripoti zinazoeleza
jinsi wafanyabiashara wanne ndugu walivyoshiriki katika mauaji hayo.
Vilivyopotea ni pamoja na maelezo ya mashahidi sita, huku
ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu ambayo ndani yake inaeleza sababu za
kifo hicho nayo ikidaiwa kupotea.
Kutokana na hali hiyo, familia ya marehemu Massawe,
imemwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, ikimuomba
aingilie kati jambo hilo kutokana na kile familia hiyo inachodai kuwa ni
kushindwa kwa jitihada zao za kulishawishi Jeshi la Polisi kuwakamata
watuhumiwa hao.
Familia hiyo
imeainisha mambo manne ambayo yanalifanya Jeshi la Polisi kutowakamata
watuhumiwa, likiwamo la kwamba jalada halisi la kesi hiyo limeibwa ikiwa ni
mpango mahsusi uliosukwa na baadhi ya maofisa katika ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Inadaiwa kuwa maelezo ya mashahidi sita muhimu
yaliondolewa na maofisa hao kwa makusudi katika jalada lililopelekwa kwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Gama amethibitisha kupokea
barua ya malalamiko kutoka kwa wanafamilia wa Massawe ambao ni Beda Massawe na
Peter Massawe.
Gama ameiambia JAMHURI kwamba suala hilo analifanyia kazi
kwa uzito unaostahili.
Katika barua hiyo, inaelezwa kwamba mashahidi ambao
maelezo yao yamenyofolewa kwa lengo la kuwalinda watuhumiwa hao ni ya Alfonsina
John, Ludovick Munisi, Lelo Selengia, Peter Gerald, Boniface Munishi na
Fulgence Gerald.
Famlia inamuomba Gama aamuru uchunguzi ufanyike upya bila
kuwashirikisha maofisa wa polisi wa Ofisi ya RCO Kilimanjaro.
Mauaji yalivyofanywa
Massawe anadaiwa kutekwa katikati ya Mji wa Moshi na
wafanyabiashara ndugu wanaomiliki vitegauchumi kadhaa katika Jiji la Mwanza na
kupelekwa katika moja ya nyumba za wafanyabiashara hao eneo la Kibosho ambako
inadaiwa alipewa mateso hadi kuuawa. Baada ya mauaji hayo, aliyekuwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko, aliueleza umma kuwa Massawe
aliuawa na wananchi, lakini baada ya kelele nyingi kupigwa na familia, hatimaye
aliyataja majina matatu ya wafanyabiashara wanaotuhumiwa kuhusishwa na mauaji
hayo.
Wafanyabiashara hao ambao baada ya mauaji hayo walikwenda
mafichoni nje ya nchi, walitajwa na Kamanda Ng’hoboko kuwa ni John Joseph
Kisoka (Magazeti) na wadogo zake Musa Joseph Kisoka na Deo Joseph Kisoka.
Hata hivyo, pamoja
na wafanyabiashara hao kutajwa na Kamanda huyo na kutangaza kuwasaka, Jeshi la
Polisi liliishia kuwakamata vijana wawili, Idrisa Hassan Munishi na John Mallya
(Small Boy) na kufikishwa mahakamani ambako walishitakiwa kwa mauaji ya
Massawe.
Vijana hao walifikishwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa
Makahama Kuu Kanda ya Moshi, Stella Mugasha, katika shauri la jinai namba PI
9/2009, lakini Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawe aliliondoa shauri hilo
mahakamani.
Kiini cha kutekwa kwa kijana huyo kinatokana na
madai ya wafanyabishara hao kwamba
Massawe alihusika na mauaji ya mama mzazi wa wafanyabiashara hao, Martha Kisoka
(68) aliyeuawa na watu wasiojulikana Mei 2009 baada ya kuvamiwa nyumbnai kwake
Kindi, Kibosho.
Barua hiyo iliyosainiwa na S.M. Ambika ambaye ni Kamishna
Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACPA) nakala yake ilipelekwa kwa Beda Massawe
wa kijiji cha Kindi, Kibosho ikimtaarifu kufika ofisi ya DCI kwa ajili ya
kupata kile kilichoelezwa kwenye barua hiyo kuwa ni ufumbuzi wa suala lake.
Amesema kuwa hivi sasa wameanza kukosa imani juu ya
maendeleo ya kesi ya mpendwa wao na kuiomba ofisi hiyo ya DCI kuwapa msaada
zaidi baada ya ofisi ya RCO Kilimanjaro kutowapa ushirikiano.
No comments:
Post a Comment