Pages

Wednesday, April 22, 2015

MAJAMBAZI YAPORA MAMILIONI YA SHILINGI KUTOKA GARI LILILOKUWA KWENYE MAKUSANYO YA FEDHA ZA MAUZO BONITE NA KUUA WAFANYAKAZI

Watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamewaua kwa kuwapiga risasi wafanyakazi wawili wa kiwanda cha vinywaji baridi jamii ya Coca Cola cha Bonite Bottles cha mjini Moshi na kupora mamilioni ya fedha.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea Aprili 20, mwaka huu saa 12:15 jioni katika  maeneo ya Soweto chini karibu na kituo cha Redio cha Kill Fm, kata ya Soweto, wilayani Moshi.

Alisema majambazi hayo yakiwa na silaha za moto wakitumia usafiri wa pikipiki mbili ambazo namba zake hazijafahamika, walivamia gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T 803 ATR lilitoka kwenye makusanyo ya fedha za mauzo.

Kamanda Kamwela alisema gari hilo lilikuwa likisindikizwa na mlinzi wa kampuni hiyo akiwa na bunduki aina ya Short gun yenye namba  za usajili 8710653 ikiwa na risasi tano.

“Hata hivyo, mlinzi huyo, Edson Shamba (56), mkazi wa Matindigani aliyekuwa anasindikiza gari hilo, aliuawa kwa kupigwa risasi maeneo ya kichwani na kufariki dunia papo hapo na dereva, Amini Mselemu, mkazi wa mtaa wa Chunya, alipigwa risasi maeneo ya kifuani, tumboni  na mkononi alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC,” alisema.  Alisema watu wanne waliokuwa ndani ya gari hilo ambao ni mawakala wa mauzo wa kampuni hiyo, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa uchunguzi zaidi.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha KCMC.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment