Pages

Friday, April 10, 2015

Mtoto wa Jaji Warioba, June Warioba Ajiunga na Chama cha ACT

MTOTO wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amejiunga na Chama cha Alliance for Change &Transparency-Tanzania (ACT).

Binti huyo aliyejiandikisha kwa jina la June Warioba, alichukua kadi ya kujiunga na chama hicho makao
makuu ya chama hicho Kijitonyama mjini Dar es Salaam jana.

Hata hivyo, June alikataa kupigwa picha wala kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwapo ofisini hapo.

Aliingia ofisini hapo saa 4 asubuhi ambapo alitumia takribani nusu saa kufanikisha usajili wa chama hicho na kutoka ndani akiwa ameongozana na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa.

June alikuwa amejiziba uso kwa mkono ili asipigwe picha wala kuulizwa maswali ambapo aliingia kwenye gari na kuondoka.

Alipoulizwa kwanini amejiunga na chama hicho kimya kimya na kwa haraka, alisema huo ni uamuzi wake.
Naye Mwenyekiti wa ACT, Anna Mughwira alisema 

June hakutaka kuandikwa kwenye vyombo vya habari,hivyo waliheshimu uamuzi wake huo.

Alisema kila mwanachama ana uhuru wa kuamua namna ya kujiunga, kwani wapo wanataka waandikwe au kutangazwa na vyombo vya habari na wengine hawapendi.

“Si mtoto wa Warioba, ni mwanachama wa kawaida tu hajasema chama alichotoka wala hajaweka wazi kama anataka kugombea nafasi yoyote ya uongozi na hakupenda kuandikwa ni kama mimi nilivyoingia.

“Sisi tuna wanachama mbalimbali, siku ya uzinduzi kuna wengine walikuja na kadi zao wakitaka kujiunga,hatutaki ugomvi na vyama pinzani vingine kwa sababu sisi pia ni wapinzani,” alisema.

Jaji Warioba anena

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Jaji Warioba alikiri June ni mtoto wake wa kumzaa.
Kuhusu uamuzi wake wa kujiunga na ACT, Jaji Warioba alisema aachiwe mwenyewe.


“Yule ni mtu mzima, hayuko chini yangu na ana uamuzi wake… siwezi kumwingilia uhuru wake,” alisema Jaji Warioba.

No comments:

Post a Comment