Pages

Monday, April 13, 2015

MWALIMU WA CHEKECHEA AMTANDIKA NA KUMJERUHI MTOTO WA MIAKA MIWILI NA NUSU KWA KUJISAIDIA SHULENI.....MZAZI AENDA MAHAKAMANI....ATOKEA MZAZI FEKI NA KUJIDAI AMESAMEHE....KESI YAFUTWA KINYEMELA

Katika tukio lisilo la kawaida, Mahakama ya Mwanzo Ilemela jijini Mwanza, imedaiwa kufuta kesi ya kujeruhiwa mwanafunzi mwenye umri wa miaka miwili na nusu, inayomkabili mlezi wa shule ya chekechea ya Nelca Day Care, Siwema Bujota (pichani), kinyume na sheria.

Wakati kesi hiyo ikifutwa, polisi mkoani Mwanza inamtafuta mtuhumiwa huyo anayedaiwa kumshambulia na kumdhuru mwili mwanafunzi, Sean Sinani.

Inadaiwa kuwa Machi 27, mwaka huu, katika mahakama hiyo, mtuhumiwa huyo alisimama mahakamani hapo akiwa na mtu mwingine na kujifanya ndiye mama mzazi wa mtoto na kusema ameamua kusamehe kesi wakati mhusika halali hakuwapo mahakamani.

Awali ilielezwa kuwa mlezi huyo alimjeruhi mwanafunzi kwa kumchapa  kwa fimbo kwa madai ya kujisaidia shuleni.

NIPASHE Jumamosi ilizungumza na mama wa mtoto huyo, Sabrina Hamis, aliyesimulia kuwa  mtoto wake alimkuta na majeraha maeneo ya mwili wake na kuamua kumfikisha kituo cha polisi cha Kirumba ambapo alipewa fomu ya polisi (PF3) na kumpeleka hospitalini.

Alisema alimpeleka hospitali ya Seketure ambapo alitakiwa kufanywa kipimo cha X-ray lakini ilishindikana kwani kilikuwa hakifanyi kazi na kupewa rufaa hospitali ya Bugando.

Alisema majibu ya kipimo hicho yalitakiwa kupelekwa hospitali ya Seketure ambapo mwanae aliendelea kupatiwa matibabu.

Alisema mwalimu huyo alikamatwa na polisi na siku iliyofuata Machi 27, alifikishwa mahakamani.

Hamis alisema akiwa mahakamani majira ya mchana, kesi yake ilikuwa haijaanza kusikilizwa na aliondoka kwenda hospitali kutokana na hali ya mtoto huyo kubadilika na kuamua kumrudisha hospitali.

Alisema alipotoka hospitalini hakuwahi mahakamani hali iliyomfanya ashindwe kuhudhuria kesi hiyo na kuamua kurudi nyumbani ambapo alipata taarifa kuwa kesi yake imefutwa.

Alisema taarifa hizo hakukubaliana nazo na kuamua kufika kituo cha polisi kufuatilia suala hilo ambapo alielezwa kuwa kesi hiyo imefutwa.

Alisema sababu za kufutwa kesi hiyo ni kutokana na upande wa mtuhumiwa mmoja wao alisimama mahakamani akijifanya ni mama wa mtoto na kusema ameamua kusamehe kesi hiyo na hakimu akaifuta.

Hamis alisema mazingira ya ufutwaji wa kesi hiyo yanaonekana kuzingirwa na rushwa kwani hakuhusishwa wakati yeye ndiye mlalamikaji.

Alisema mpelelezi wake anamlaumu kwa kuondoka mahakamani bila kusubiri kesi yake, bila kujali hali ya mtoto wake kwani ilibadilika na kumlazimu kuondoka akijua angewahi kutoka hospitali ili asikilize kesi hiyo.

Hata hivyo, alisema wiki hii aliamua kwenda mahakama kuulizia kesi hiyo na kujulishwa imefutwa na kutakiwa aende kituo cha polisi.

Alisema alirudi kituo cha polisi cha Kirumba lakini hawakumpa ushirikiano. "Cha kushangaza hawa askari wananiuliza huyo mtuhumiwa tutampata wapi maana hapatikani, hivi hilo swali linanihusu mimi inaonyesha kabisa kuna mchezo unaendelea ila haki ya mwanangu nitaipata," alisema. 

"Hivi huyo hakimu aliiona sura yangu mahakamani hadi aifute kesi yangu nashangaa kesi inafutwa hata PF3 haijajazwa na mtoto wangu bado hajapona vizuri," alisema. 

Kwa upande wake, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, Japhet Lusingu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa kesi hiyo ilifutwa Machi 27, mwaka huu.

Alisema kesi iliendeshwa na kufutwa siku hiyo hiyo  na kwamba sababu za ufutwaji wa shauri hilo ni mlalamikaji kueleza watamalizana nje ya mahakama.

Lusingu alisema mlalamikaji alirudi kituo cha polisi na kulalamikia suala hilo, hivyo juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea.

Aidha, alisema mlalamikaji huyo anatakiwa kurudisha PF3 na kwamba kuna uwezekano wa kesi hiyo kupelekwa wilayani.


No comments:

Post a Comment