Pages

Monday, April 13, 2015

MWENYEKITI YUPO MAHUTUTI BAADA YA KUKATWA UUME..

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Suhunyi (CCM), Wilaya Siha, mkoani Kilimanjaro, Moses Kileo (53), amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Mjini Moshi akiwa mahututi baada ya kuvamiwa na kutekwa na kundi la watu wasiojulikana na kukata sehemu ya uume wake na kutokomea.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Godfrey Kamwela, aliiambia NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu jana kwamba, Mwenyekiti huyo alinusurika kifo baada ya watu hao kutaka kipande cha juu cha uume wake, kwa kile alichoeleza huenda kinatokana na imani za kishirikina.

“Bado tunawasaka waliohusika kumteka na kisha kumkata Moses kiungo chake kutokana na imani za kishirikina. Nimeagiza polisi kuhakikisha watu hao wanapatikana mara moja na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kamwela.

Alisema Mwenyekiti huyo kwa sasa hawezi kuzungumza kutokana na hali mbaya aliyokutwa nayo na kwamba Polisi wameshindwa kumhoji.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Kileo alikumbwa na mkasa huo, Aprili 10, katika Kijiji cha Kashashi, Wilaya ya Siha.

Alidai kuwa baada ya watu hao kukamilisha zoezi hilo, walimtelekeza kando ya barabara ya Kashashi-Suhunyi, akiwa anavuja damu nyingi na baadae kutokomea na kipande hicho cha uume wake.

Akizungumzia tukio hilo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (Nec), Wilaya ya Siha, Meijo Laizer, alisema tukio hilo la kusikitisha, linajenga taswira mbovu kwa baadhi ya watu kutaka kuvuruga amani kwa misingi ya kuwagawa wananchi kisiasa kwa kisingizio cha ushirikina.

“Matukio kama haya yanaweza kuvuruga amani wakati huu, tukielekea katika uchaguzi mkuu, naomba Serikali kwa maana ya Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk. Charles Mlingwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, alisimamie jambo hili ili kujua watu hao walikuwa na nia gani ovu, ama ni masuala ya kisiasa au ushirikina,”alisema Meijo.

No comments:

Post a Comment