Pages

Monday, April 27, 2015

Raisi Kikwete asamehe wafungwa 4,000....Wapo wenye Ukimwi, Saratani, Wazee zaidi ya miaka 70, walemavu na wanaonyonyesha....Watatakiwa kuthibitishwa na jopo la waganga..

RAIS Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,129 ambako 400 wataachiwa huru na wengine 3,729 watapunguziwa vifungo vyao.
Alitoa msamaha huo katika kuadhimisha miaka 51 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, kwa kutumia madaraka yake aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kusainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, wafungwa waliopunguziwa vifungo watabaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

“Ni mategemeo ya Serikali kwamba wafungwa watakaoachiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,”ilisema taarifa hiyo.

Katika msamaha huo wafungwa wote watapunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu namba 49(1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58, isipokuwa wafungwa wenye makosa yasiyo na msamaha.

Wafungwa waliosamehewa ni wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu na saratani, wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi na wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Wengine ni wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili. Wote waliosamehewa wanatakiwa kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa ama mganga mkuu wa wilaya.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafungwa ambao hawakupata msamaha ni waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, kifungo cha maisha, wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji wa rushwa.

Wengine ni wanaotumikia kifungo kwa unyang’anyi, makosa ya kupatikana na silaha, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.

Pia wale waliowapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na shule za sekondari na ambao walitenda makosa hayo wakiwa na umri wa miaka 18.

Wezi wa magari na pikipiki, kutumia vibaya madaraka, waliowahi kupunguziwa kifungo na msamaha wa Rais, waliozuia watoto kupata masomo, utekaji wa watoto, kufanya biashara ya binadamu, kukutwa na viungo vya binadamu pamoja na vitendo vya ukatili na mashambulio dhidi ya albino.

“Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili, makosa ya wizi, ubadhirifu wa fedha za Serikali na wafungwa wenye makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi halali,” ilieleza taarifa hiyo.

MTANZANIA

No comments:

Post a Comment