Pages

Tuesday, April 14, 2015

TUSIWABEZE ALSHABAAB; WAMEINGIA KWA WANAFUNZI

Tukio la kijana mwanafunzi Mtanzania, Rashid Charles Mberesero kukamatwa nchini Kenya akihusishwa na shambulizi la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa kilicho kaskazini mwa nchi hiyo jirani, haliwezi kupita kirahisi bila watu binafsi, taasisi za serikali na umma kwa ujumla kufanya tathmini ya kina.

Tathmini ya kina ya kujiuliza, ni vipi kijana mdogo kama huyo, ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Bihawana ya mkoani Dodoma, kushiriki katika jambo kubwa na baya tena la kinyama kama hilo, bila watu wake wa karibu, taasisi za usalama na hata majirani kutilia shaka nyendo zake.

Kwa mujibu wa mama yake mzazi, kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, kutoka Same mkoani Kilimanjaro, hakuwahi hata kufika jijini Dar es Salaam, sembuse kuvuka mpaka na kuingia nchi nyingine. Nyendo zake, ni kutoka huko kwao kuelekea shuleni Dodoma.

Kama utamwelewa vizuri mama huyo pamoja na simulizi ya walimu kutoka shuleni kwao na wanafunzi wenzake, ni kwamba endapo Rashid alipata mafunzo yoyote ya kutumia silaha na ugaidi, basi mambo haya yamefanyika ndani ya ardhi ya Tanzania, tena katika mikoa kati ya Kilimanjaro na Dodoma!

Tunaweza kuliona jambo hili kuwa ni dogo na la kawaida labda kwa kuwa kijana huyu amekwenda kutekeleza vitendo vyake viovu nje ya nchi yetu, lakini kwa watu makini tunaotazama kwa macho matatu, suala hili siyo dogo kabisa, ni kubwa linalopaswa kuwaumiza vichwa watendaji wa taasisi zetu za ulinzi na usalama, sambamba na wananchi wenyewe kwa ujumla wao.

Kumbe, katika sebule zetu, ndani ya nyumba zetu na hata mapori yetu, bado kuna watu wanaweza kuwafundisha vijana wetu wa sekondari na vyuo, kuasi taifa lao, kusaliti ubinadamu wao na kujiingiza katika mambo maovu kama anavyotuonyesha Rashid!

Wananchi, labda kwa kutingwa na harakati za kujitafutia mlo wao wa kila siku, wameacha kuwa na macho ya udadisi, hawashangai tena wanapoona jambo lisilo la kawaida linapoendelea.

Ingekuwa zamani, watu wangetilia shaka nyendo za Rashid kupenda kushinda msikitini na kuwa mtu wa peke yake, peke yake!Hata vyombo vyetu vya usalama, navyo vinaonekana vimelala, havijishughulishi tena na mambo magumu, badala yake wamekuwa na intelijensia kali kufuatilia wanasiasa, hasa wa upinzani ambao shughuli zao nyingi ni za wazi.

Wanausalama wetu ni wepesi kufahamu vurugu zitakazotokea katika maandamano ya walimu wanaodai malimbikizo ya mishahara yao, kuliko kuhisi juu ya kuwepo kwa watu wanaotoa ufadhili wa walimu wa maovu kwa vijana wetu.

Kama vijana wetu wa sekondari wanaweza kuingiliwa na kushawishiwa hadi kukubali kufanya ugaidi, sioni wahalifu hawa kama watapata kazi kubwa kuwashawishi kushika silaha mamia ya vijana wasio na kazi wanaoshinda vijiweni na kukaba watu usiku kwa ahadi tamu zisizo na ukweli wowote.

Tuna-relax labda kwa vile wanaoshambuliwa hivi sasa ni Wakenya. Tunasahau kuwa wapo Wakenya ndani ya kundi la Al Shabaab.Kwa tukio la Rashid nashawishika kuamini kwamba ndani ya kundi la Al Shabaab kuna Watanzania sasa ni juu ya serikali na vyombo vyake vya usalama kufuatilia kiintelejensia ili kubaini hili haraka sana kabla mambo hayajaharibika.

Inashangaza, Rashid alikuwa akisoma katikati ya nchi yetu, Dodoma, ilikuwaje hao Al Shaabab wakaingia Bihawana na kumshawishi kijana huyo bila kugundulika? Ilikuwaje Rashid akasafiri hadi mashariki mwaka Kenya akitokea Tanzania bila kujulikana na vyombo vyovyote vya dola?

Hii maana yake ni kwamba kuna watu wanaosuka mipango na kufanikisha vijana kuvuka mipaka na kwenda kujiunga na Al Shaabab, sasa ni nani hao? Watafutwe kwa sababu wanahatarisha usalama wa taifa letu.


Hao ndiyo wanaosababisha vijana wetu kuingia katika mzunguko wa magaidi na siku watakapoanza kutushambulia, wapo baadhi ya vijana wetu, wanaopata mafunzo humu humu nchini, watatumika kutuua na tutakuwa tumechelewa kuwadhibiti! Nashauri hili nalo lionekane kama ni janga la taifa na lipigwe vita.
GPL

No comments:

Post a Comment