Pages

Friday, May 1, 2015

Clinton ziarani Tanzania.....Ndege yake yatua kwa dharura...Ilipata hitilafu angani

Ndege iliyokuwa imembeba rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton na mwanaye Chelsea, juzi ilipata hitilafu katika moja ya injini zake na kulazimika kutua Dodoma kwa ajili ya matengenezo kabla ya kuendelea na safari.

Ndege hiyo aina ya DHC 7 yenye namba za usajili 5Y-CDK, iliyokuwa ikitokea
mkoani Iringa kuelekea Ziwa Manyara, ilitua saa 10.15 jioni juzi  na kuondoka saa 10.24 jioni.

Chanzo cha habari kutoka uwanja huo wa ndege, kilisema ndege hiyo ilikuwa na tatizo dogo na lilirekebishwa wakati Clinton na abiria wengine wakiwa ndani ya ndege.

“Tulimuuliza rubani wa ndege hiyo kama angehitaji msaada wowote kutoka kwetu, lakini alisema kuwa ni tatizo dogo tu na angeweza kutua mwenye bila msaada na akafanya hivyo,” alisema mpashaji habari huo aliyeomba jina lake lisitiriwe.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, (TCAA),  Ludovic Ndumbaro alikataa kulizungumzia kwa madai yeye si msemaji wa mamlaka hiyo.

“Mtafute mkurugenzi ndiyo msemaji wa mambo yote yanayohusu mambo ya anga,” alisema.

Clinton na binti yake Chelsea walifika Tanzania kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na mfuko wa familia ya Clinton.

Gazeti la mtandaoni la CBSNews.com jana liliandika kuwa ratiba ya safari ya Clinton inaonyesha kuwa ndege hiyo haikutakiwa kutua Dodoma, lakini kwa sababu ya hitilafu iliyojitokeza rubani akaamua kutua ili kutatua tatizo.

Hata hivyo, CBSNews.com lilimkariri msemaji wa mpango wa maendeleo wa Clinton aliyesema hakukuwa na dharura yoyote.

Clinton ataendelea na ziara yake ya siku tisa katika nchi za Kenya, Liberia na Morocco. Miradi inayosimamiwa na mfuko wa Clinton ni ya kilimo cha kibiashara.
MWANANCHI


No comments:

Post a Comment