Pages

Friday, May 1, 2015

Mahakama imemuamuru mbunge Abdallah Sharia Ameir wa Dimani Zanzibar kutoa sh 200,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto aliyemtelekeza


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuamuru Mbunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar, Abdallah Sharia Ameir (CCM) kutoa Sh 200,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mtoto wake wa kiume, mwenye umri wa miaka mitatu na nusu, anayedaiwa kumtelekeza.
Pamoja na amri hiyo, Hakimu Mkazi, Hellen Liwa alisema mbunge huyo atatoa kiasi hicho cha fedha kuanzia siku alipokoma kutoa matunzo na matibabu kwa mtoto huyo, anayetajwa kuwa ni mlemavu.

Pia, aliamuru mtoto huyo kulelewa na wazazi wake na siyo bibi yake, kama alivyokuwa akitaka mbunge huyo. Hivyo ataendelea kukaa na mama yake.

Kwa upande wake, Wakili Gideon Mandes aliyekuwa akimtetea Hawa Deus aliyekuwa mke wa mbunge huyo, alisema kupitia hukumu hiyo Mahakama imetoa uamuzi wa haki.

“Kupitia hukumu hii nimebaini wazazi wanawajibu wa kumtunza mtoto wanayemzaa bila ya kujali hali yake hata kama ni ya ulemavu asitelekezwe na imedhihirisha hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba sheria ipo sawa kwa kila mtu,”alisema wakili huyo.

Wakili huyo aliwashauri Watanzania wenye matatizo na changamoto kama hizo, kuweka bidii ya kuijua sheria na taratibu zake ili waweze kuitumia kupata haki na suluhisho kupitia Mahakama.

Mwezi Januari 2015, Hawa alivamia kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala akiwa amesindikizwa na kundi la watu, ambao mmoja wao alikuwa amembeba mtoto wa mbunge huyo mwenye ulemavu, huku wakipiga kelele na kuwaacha wabunge na viongozi wa dini waliokuwepo kupigwa na butwaa.

Mtafaruku huo ulitokea katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, ambapo kikao hicho kilikuwa kinaendelea na mjadala kuhusu marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Kiislamu.

Miongoni mwa kundi waliomsindikiza Hawa ni mwanaharakati Joyce Kiria, na watu wengine ambao hawakufahamika mara moja.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment