Pages

Monday, May 18, 2015

DAWA KLINIKI ZA MKOREA NUSURA ZIUE MTOTO WA MWANASHERIA DAR

Licha ya serikali kutochukua hatua kuokoa maisha ya raia wake, mtoto wa mwanasheria mmoja wa jijini Dar es salaam, amenusurika kifo kutokana na kutumia dawa zinazotolewa kliniki za raia wa Korea Kaskazini.

Kliniki hizo zilizopo maeneo ya Temeke, Magomeni na Kariakoo (sasa karibu na msikiti wa Kwa Mtoro), zimedaiwa
kwa muda mrefu kutoa dawa za asili zisizokuwa na majina au maelekezo kuhusu namna ya kuzitumia.

Pia sehemu ya dawa hizo zinaelezwa kuwa na kiasi kikubwa cha madini ya chuma yanayoathiri afya za watu, ingawa madhara hayo yanatokea baada ya muda mrefu.

Bernadeta Shayo, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, mkazi wa Mbagala Mponda jijini humo,  alisema mtoto wake,  Gabriel Shayo (18), alitumia dawa alizopewa kwenye kliniki hizo wakati akisumbuliwa na matatizo ya kifua.

Alisema tukio hilo lilitokea Agosti, mwaka jana baada ya kupatiwa matibabu katika kliniki ya Wakorea hao iliyopo Tambukareli, ambapo alipata maumivu makali, kubanwa kifua na kutapika damu.

Kwa mujibu wa Bernadeta, alipofikishwa hospitalini hapo, Gabriel alibainika kushambuliwa na vijidudu kifuani na tiba yake iligharimu Sh. 150,000, na kiasi kingine cha Sh.10,000 kila siku kwa muda wa wiki mbili.

Alisema hakupewa risiti  ya malipo hayo kama inavyotakiwa kisheria, badala yake kiasi hicho cha fedha kiliandikwa kwenye daftari la wateja wanaolipia gharama za matibabu.

Bernadeta alisema baada ya muda huo, hali ya Gabriel ilizidi kuwa mbaya huku akipata maumivu makali kifuani, licha ya kuhakikishiwa na raia hao wa Korea Kaskazini kwamba angepona ndani ya wiki mbili.

Hata hivyo, Bernadeta alisema alilazimika kurejea kwenye kliniki hiyo ambapo watoa huduma wanaotambulika kama madaktari, walimjulisha kwamba vijidudu havijaisha na kutaka malipo ya Sh. 150,000 kwa ajili ya matibabu ya wiki mbili za nyongeza.

ATAPIKA DAMU
Bernadeta, anasema mwanaye alipata dawa za aina tofauti za kutafuna na kumeza, zisizokuwa na majina na kuandikwa kwa lugha ya Korea, hali iliyomfanya ashindwe kutafuta ukweli wa tiba hiyo baada ya kuzidiwa na kutapika damu.

“Siku ya kwanza alipokunywa, alikohoa na kutoa makohozi yenye mchanganyiko wa damu, kila alipozidi kutumia ndipo damu ilizidi kutoka na matokeo yake alitapika damu kwa wingi mfululizo,” alisema.

KUGUNDUA TB
Bernadeta, alisema Agosti 28, mwaka jana, hali ya Gabriel ilizidi kuwa mbaya hivyo akamrejesha kwenye kliniki hiyo ili kujua ukweli wa tiba zao.

“Tulimkuta daktari mmoja (anamtaja jina) ambaye tulibishana sana kuhusu hali mbaya ya mtoto wangu, niliwahoji kwa nini waliniongopea na kunipatia dawa zilizomuathiri mwanangu, lakini wakaishia kutufukuza,” alisema.

Bernadeta alisema ili kuokoa maisha ya mwanaye, alikwenda hospitali ya Zakhem ilipothibitika kwamba Gabriel alikuwa anaumwa kifua kikuu ambacho kilifikia hatua ya hatari kutokana na kuchelewa kupata tiba.

Gabriel alipata tiba kwenye hospitali hiyo ya serikali hadi Februari mwaka huu ambapo kwa mujibu wa Bernadeta, hali yake inaendelea vizuri.

WAKOREA WAKACHA
NIPASHE Jumapili ilipofika kwenye kliniki hiyo na mwandishi wetu kujitambulisha, wafanyakazi wenye asili ya Korea walimzuia asiingie ndani na kusema hakuna mtu wa kutoa ufafanunuzi wa kadhia hiyo.

Pia, walianza kuongea kikorea hivyo kushindwa kutoa fursa kwa mwandishi kujua hoja iliyokuwa inazungumzwa.

TRA YABAINI UKWEPAJI KODI
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Richard Kayombo, alisema kitendo cha hospitali hizo kutoa huduma bila kutoa risiti ni kuvunja sheria na utaratibu wa haraka unafanyika kuzifanyia uchunguzi.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Kayombo alisema anawasiliana na wenzake wanaofanya kazi kanda za Temeke na Kinondoni kufanyia uchunguzi hospitali hizo,  kabla ya kutoa tamko la adhabu gani wanaweza kuzichukulia kama ikibainika wanakwepa kulipa kodi.

JEURI INATOKA CCM
Wakati hayo yakijiri, taarifa za ndani zinaeleza kuwa ‘kiburi’ kinachoendelezwa katika utoaji tiba hizo kinatokana na mafungano ya kibiashara yaliyopo kati ya kliniki hizo na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hivi karibuni, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abilah Mihewa, alithibitisha chama hicho kuingia ubia na Wakorea Kaskazini katika biashara ya kliniki hizo, ingawa miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa na uongozi uliopita yanafanyiwa kazi.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment