Pages

Monday, May 18, 2015

USHOSTI UKIINGIA SHUBIRI NI SHIDA..

Hivi karibuni, baada ya kuvunjika kwa urafiki wa ‘kupika na kupakua’ kati ya mashostito wawili walio katika tasnia ya Bongo Movies, Aunt Ezekiel Grayson na Wema Isaac Sepetu maneno hayo yametumika pasipo sababu, Ijumaa Wikienda lina kila kitu!

 AUNT BILA KUUMA MANENO

Juzi, Aunt ameibuka na kutoa kauli kali bila kuuma maneno kwamba, Wema akitangulia kuaga dunia, yeye hatakwenda kumzika kwa maana ya kuuaga mwili wake sanjari na kuomboleza.

KISA CHA KAULI

Kauli hiyo ya Aunt imekuja siku chache baada ya Wema naye kudaiwa kutoa kauli kama hiyo akisema kwamba, kutokana na urafiki wake na Aunt kufa na kuwa maadui, basi hata akifa, Aunt asiende kumzika.

 MSIKIE AUNT ‘LAIVU’

Ijumaa wikienda: Aunt pole kwa kulea mimba! Nina machache sana. Wema amedaiwa kuanika hatima ya ugomvi wenu kwamba, hali ilipofikia hata akifa wewe usiende kumzika. Wewe unasemaje?

Aunt: Kwanza nashangaa taarifa za kwamba nina ugomvi na Wema maana hata hao ndugu zake nimesikia wanaongea mambo kibao.

“Ila mimi sioni kama kuweka picha ya tangazo la shoo ya Zari (Zarinah Hassan) kwenye peji yangu ya Instagram ni kosa. Kwa hiyo kama yeye hataki kuzikwa na mimi, hata mimi nasema sitamzika Wema.

AANZA KUFUNGUKA

”Halafu sidhani kama kuna mtu anaweza kunipangia kitu kwenye peji yangu mwenyewe ambayo nina uamuzi wa kufanya chochote ninachojisikia.

 ILIKUWA UTANI, IYOBO ATAJWA

“Mimi sidhani kama hapo kuna ugomvi, maana nilichoandika na kuweka siku hiyo ilikuwa ni utani lakini hata kama yeye na ndugu zake walichukulia ‘siriasi’ basi bado walitakiwa kutambua kuwa, mchumba wangu Iyobo (Moses) ni mfanyakazi halali wa kundi la muziki la Diamond (Nasibu Abdul), hivyo nilikuwa na haki ya kumsapoti kwa asilimia zote maana fedha anazopata kupitia huko ndizo zinazonifanya mimi na familia yangu niishi,” alisema Aunt.

 FAMILIA YAWEKA KIKAO

Kufuatia vuguvugu hilo kushika kasi, hivi karibuni familia ya  Wema inadaiwa kuweka kikao na kusema kwamba walimuonya ndugu yao huyo siku nyingi kwa kumwambia kuwa, urafiki wake na Aunt ni sawa na ‘spea’ za ki-China kwani waliamini hautadumu kwa sababu ni unafiki tu bora hata alivyokuwa na Kajala Masanja.

Chanzo makini kutoka katika familia ya Wema kimelipenyezea ubuyu Ijumaa Wikienda ambapo kilitiririka:

“Mama Wema kama kawaida yake, alifikia hatua ya kusema kwa sasa hataki tena kumwona mwanaye akirudia urafiki wake na Aunt kwa sababu ni mnafiki.

MAAZIMIO YA KIKAO YAFIKA KWA WEMA

“Maneno hayo ya mama na ndugu wengine, yalifikishwa kwa Wema, akawaelewa na kusema hana haja tena ya kuwa karibu na Aunt hata itokee nini maana hakuna anachomsaidia.”

 AUNT TENA, AMWANIKA WEMA SASA

Aunt alipoambiwa kuhusu maazimio ya kikao cha familia ya Wema na jinsi staa huyo alivyoyapokea, alisema:

 “Kama familia yake wamefikia hatua ya kuingilia hili, mimi nafikiri sina tatizo maana nina maisha yangu na yeye (Wema) ana maisha yake. Ila tu kama ni ishu ya wazazi, naomba wajue pia mimi sijajizaa wala sijazaliwa na miti, nina ndugu tena wanajitambua kwa kila hali.

“Nikiangalia sababu za ugomvi ni za kibinafsi sana hata hazifai kuingiliwa na mtu, maana haiwezekani kwenye maisha haya eti Wema akinuniana na mtu basi na mimi nimnunie, sijaumbwa hivyo wala sina unafiki huo.

“Kama staili ya maisha ikiwa kila atakayekwazana naye na mimi nimchukie siku wanapoelewana mimi si nitaonekana sifai kote? Wao wafahamu kuwa mimi najitambua wala si wa kuburuzwa hivyo.

“Kama wanasema hawawezi kushiriki lolote kwangu hata mimi sina sababu ya kujipendekeza kwao.

 WEMA AZIDI KUCHAMBULIWA

“Hakuna kitu kibaya katika maisha kama kuwa na rafiki ambaye siku zote yeye akikosana na mtu basi na wewe ukosane naye. Mbona mimi maadui zangu yeye ni marafiki zake na wala sijawahi kununa. Iweje sisi tukorofishane na watu yeye aongee nao ila yeye akikorofishana na watu basi hataki kabisa hata kutuona nao?”

 WEMA NAYE ATEMA NENO

Baada ya Ijumaa Wikienda kupata fukunyuku hizo lilimsaka Wema kwa maana ya kujiridhisha na kinachodaiwa kusemwa na yeye na familia yake, mambo yalikuwa hivi:

“Yaani hata sitamani kusikia jina la Aunt maana alichokifanya ni bora hata ya Kajala ambaye ishu yake ni ya moja kwa moja. Nashindwa kuliweka wazi sana lakini familia yangu haitaki hata kumsikia kwa jinsi ilivyochukizwa naye.

“Sifikirii kama kuna siku nitakuja kukaa naye tena au kuongea chochote mbele yake maana alichokifanya si cha kunifanyia mimi tuliyeshibana kama mapacha.”

Aunt  ‘mama kijacho’ na Wema walikuwa marafiki walioshibana kabla ya kutofautiana baada ya Aunt kutoa sapoti kwa mpenzi wa Diamond, Zari kwenye shoo yake ya Zari All White Party kwa kuposti picha kwenye mtandao iliyoonesha kupigia debe shughuli hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City hivi karibuni jambo lililomkera Wema akiamini Aunt  ni mnafiki, yuko kwake na kwa mahasimu wake hao.

GPL

No comments:

Post a Comment