Pages

Friday, May 22, 2015

Filamu chafu za mabanda ya vichochoroni zinasababisha wanafunzi wasihudhurie shule

MH. BETTY MACHANGU, MBUNGE VITI MAALUMU CCM
Serikali imetakiwa kupiga marufuku uonyeshaji wa filamu chafu kwenye mabanda ya vichochoroni kwani zinasababisha wanafunzi wengi kutohudhuria mashuleni na badala yake kwenda kuangalia picha hizo.
Rai hiyo ilitolewa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Betty Machangu, wakati akiuliza swali bungeni jana.

"Serikali itafanya lini opereshini ya kuwaondoa watu wanaoonyesha picha chafu na kusababisha mahudhurio ya wanafunzi wa shule za msingi kuwa mabaya," alihoji mbunge huyo.

Akijibu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, alikiri kuwapo kwa uonyeshwaji wa filamu hizo katika maeneo ya Dar es Saalam na baadhi ya miji mikubwa nchini.

Alizitaka halmashauri na Jeshi la Polisi kuchukua hatua kuzuia vibanda ambavyo vinaonyesha picha za sinema ambazo ni chafu.

"Mara nyingi picha hizo huwa zinaonyeshwa mchana wakijua fika kwamba wazazi wa wanafunzi wapo makazini...narudia tena kuziomba mamlaka zinazosimamia maeneo yao kuchukua hatua za haraka," alisema.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment