Pages

Thursday, May 14, 2015

MAHABUSU 12 WAGOMA KUINGIA MAHAKAMANI......KESI INA MIAKA 7 HADI SASA......HAKIMU ASEMA TATIZO NI WAKILI AMBAYE ANA KESI NYINGINE MAHAKAMA YA RUFAA..

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mahabusu 12 waliokuwa wakipelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, jana waligoma kushuka katika gari la polisi wakidai mahakama imeshindwa kusikiliza malalamiko yao.

Tukio hilo limetokea jana
ambapo baadhi ya mahabusu  waliozungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti wakiwa wamelala ndani ya gari la polisi, waliwatupia lawama
baadhi ya wanasheria wa Serikali wanaosimamia kesi hiyo.

Mahabusu hao ambao wanakabiliwa na Kesi ya Jinai namba 83 ya mwaka 2009 inayohusiana na unyang'anyi wa kutumia silaha katika Mgodi wa Dhahabu wa Resolute, walisema, kesi hiyo ina miaka saba hadi sasa, lakini bado haijasikilizwa hivyo kusababisha usumbufu kwao na ndugu zao.

Waliutaka mhimili huo, kusikiliza kesi zote za zamani haraka iwezekanavyo na kuzitolea hukumu.

Mshtakiwa mmojawapo katika kesi hiyo, Edward Bunela alisema mahakama inapaswa kuwatendea haki kwani wamekaa mahabusu muda mrefu na kumuomba Jaji Mkuu Othumani Chande, kuingilia kati kesi hii ili hatua iliyosalia ikamilike kwa muda stahiki.

"Tunamuomba Jaji Mkuu aingilie kati kesi hii ambayo imedumu miaka saba bila kutolewa hukumu...upande wa Jamhuri unatusumbua wakati sisi tunataabika gerezani, bora hukumu itoke tujue hatima yetu," alisema Bunela.

Mshtakiwa mwingine, Shaabani Amour, alisema kuwa hawajui hatima yao kwani mwenendo wa kesi hiyo haufahamiki na kuziomba mamlaka za juu kuwasaidia ili kutekeleza agizo la Jaji Mkuu ambalo alizitaka Mahakama zote nchini kuharakisha usikilizwaji wa kesi mbalimbali zilizokaa muda mrefu bila kutolewa hukumu.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo ambaye anasikiliza kesi hiyo; Spraphine Nsana, alisema tatizo ni wakili wa washtakiwa namba 14, 15 na 16 ambaye ana kesi katika Mahakama ya Rufaa; hivyo hakuweza kuhudhuria kwenye shauri hilo.

Alisema wakili huyo aliwasilisha barua ya taarifa mahakamani, hivyo shauri hilo litasomwa Mei 25, mwaka huu.

Baadhi ya ndugu wa washtakiwa, wameutupia lawama upande wa Jamhuri kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kesi hiyo kuchukua muda mrefu na hakuna kinachoendelea.

Hivi karibuni, Jaji Chande alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo, aliwataka Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya, Mkoa na Mahakama Kuu kuhakikisha wanamaliza kesi ambazo zina miaka saba hadi miwili ili kupunguza msongamano wa mahabusu gerezani katika mkoa huo.

MAJIRA

No comments:

Post a Comment