Pages

Thursday, May 14, 2015

Mmmhh....KISWAHILI NI KIPANA.....UNGEKUTANA NA HIKI KICHWA CHA HABARI UNGEELEWA NYONGO 100 NI NINI?..

Nyongo 100 Zampeleka Chuo cha Mafunzo miezi Sita

Hassan Khamis, Pemba

MAHAKAMA ya Mkoa Wete, imetoa hukumu ya kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka sita (6) kwa mshtakiwa Fadhil Mussa Sharif (25) mkaazi wa Chasasa Wete kwa kosa la kupatikana na bangi nyongo 100.

Mara baada mshtakiwa kupanda kizimbani akisubiri taratibu za mahakama, ndipo hakimu wa mahakama hiyo Makame Mshamba aliposoma hukumu hiyo.

“Mshtakiwa bado ni kijana mdogo na taifa linakuhitaji katika shughuli za kuliletea maendeleo, hivyo utatumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka sita, ili ukajirekebishe tabia”,alisema hakimu huyo.

Mwendesha mashtaka katika mahakama hiyo Ali Haidar alimuomba hakimu huyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwani, dawa za kulevya imekuwa ni tatizo kubwa katika nchi.

Mwendesha mashitaka huyo aliishawishi mahakama hiyo kwa kueleza kuwa, viongozi wamekua wakipambana na tatizo hilo kwa nguvu zao zote hivyo adhabu kali itakua ni fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Kabla ya kusomwa hukumu hiyo mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea, ambapo aliiomba mahakama hiyo isimpe adhabu ya kutumikia chuo cha mafunzo na badala yake impe adhabu ya kutumikia jamii.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Juni 9, mwaka jana majira ya saa 6:00 mchana eneo la Chasasa wilaya Wete Pemba, bila ya halali mshtakiwa alipatikana na bangi nyongo 100 zenye uzito wa gramu 154.36.

Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 115 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009, kama kilivyorekebishwa na sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria ya uingizaji na matumizi ya dawa haramu ya kulevya sheria ya Serikali ya Zanzibar.

Mshtakiwa amepewa nafasi ya rufaa ndani ya siku 30 imetolewa kwa upande wowote ambao haukuridhika na hukumu iliotolewa na mahakamani hapo.

ZANZIBARNEWS

No comments:

Post a Comment