Pages

Friday, May 15, 2015

MALI ZA HOSPITALI YA AMI ZAKAMATWA NA DALALI.....NI KUTOKANA NA KUDAIWA KODI YA PANGO ZAIDI YA SH BILIONI 3

DALALI wa Mahakama, MEM Auctioneers and General Brokers Ltd, jana alikamata na kuondoa mali za Hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Centre iliyoko Msasani Dar es Salaam, kutokana na kudaiwa kodi ya pango ya zaidi ya Sh bilioni tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo mwakilishi wa kampuni hiyo ya udalali, Elieza Mbwambo, alisema kiasi hicho ni kodi ya pango ya zaidi ya miezi 26 kinachodaiwa na mmiliki wa jengo hilo, Navtej Singh Bains.

“Hapa tunatekeleza amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara ya Aprili 24 mwaka huu iliyoamuru kukamatwa kwa fedha, magari na mali za AMI ili kupigwa mnada kwa ajili ya kulipa deni la kodi ya pango na kisha kuondolewa kwenye jengo na kumkabidhi mmiliki, ” alisema Mbwambo.

Alitaja mali zilizokamatwa kuwa ni magari matatu ya kubebea wagonjwa (ambulance), vitanda maalum vya kulaza na kuwahudumia wagonjwa, gari ndogo ya Mark II, mashine mbalimbali kama kompyuta, viti, meza, makochi na hata vitambaa na mashuka ya hospitali hiyo.

Alisema mdai aliwaomba wakamate na kuchukua vitu ambavyo havitumiki kutibu wagonjwa kwa sasa ili wagonjwa hao wahamishwe na kufikia Mei 22, mwaka huu hospitali hiyo itafungwa rasmi.

“Ingawa mahakama ilitoa amri ya kukamatwa mali zote baada ya kikomo cha notisi ya siku 14 ambayo imeisha jana, mdai amefanya ubinadamu na ametuomba kama madalali wa mahakama, kuondoa na kukamata vitu ambavyo havitumiki na wagonjwa waliolazwa.

“Tumewapa notisi nyingine ya kuwahamisha wagonjwa na hawatapokea wagonjwa wapya hadi Mai 22 mwaka huu, kisha tutaondoa kila kitu na kumkabidhi mmiliki jengo lake,” alisema Mbwambo.

Alitaja mashine ambazo zimeachwa kwa ajili ya kuwapa huduma wagonjwa kuwa ni City-Scan, X-ray na mashine nyingine ambazo ni muhumu katika kuchunguza maendeleo ya afya ya mgonjwa.

Taarifa zaidi zinasema kwamba akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zilikutwa zimefungwa na fedha zote zikiwa zimetolewa.

Hata hivyo jana wakati wa ukamataji wa mali hizo wafanyakazi wa hospitali hiyo walionekana kupigwa na butwaa na walipohojiwa kuhusu tukio hilo walikataa kuzungumza kwa kudai kuwa wamechanganyikiwa.

“Naomba uniache siwezi kuzungumza kwa sababu nimechanganyikiwa,” alisema muhudumu mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya rangi ya kijani ambaye hakutaja jina lake.

Baadhi ya ndugu na jamaa wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo walionekana wakifanya taratibu za kuanza kuwahamisha wagonjwa wao, huku uongozi wa hosipitali ukionekana kupigwa butwaa.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hosipitali hiyo, Lawrence Ochola alisema kwa ufupi kuwa bado madaktari wanaendelea kuwahudumia wagonjwa waliolazwa na kwamba hawezi akazungumzia zaidi suala hilo.

Amri ya kufungwa AMI ilitolewa Mei 7 mwaka huu na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

MTANZANIA

No comments:

Post a Comment