Pages

Thursday, May 21, 2015

Mbunge Ahoji "Hekalu" la Mbunge Mwenzake Kutobomolewa

Mbunge wa viti maalum Esther Bulaya, CCM
Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya (CCM) (pichani), ameishambulia Serikali hususani Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kuwa ndumila kuwili kwa kushindwa kubomoa hekalu lililojengwa eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Bila kumtaja anayemiliki hekalu hilo,  Esther alisema kuwa baadhi ya watu waliojenga majumba katika maneo yasiyoruhusiwa kisheria, wameketi upande wa kulia na kushoto kwake bungeni humo.

Alisema hayo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) jana.

Alisema kumekuwa na double standard (undumila kuwili) kwa serikali kutekeleza matakwa ya kisheria kwa watu waliojenga majumba kama vile maeneo ya ufukwe wa bahari ambayo hayaruhusiwi kisheria.

Alisema tabia hiyo ya undumila kuwili, imesababisha kubomolewa kwa nyumba za watu aliowataja kuwa ni dagaa na kuziacha nyumba za watu wenye nazo ambao ni mapapa.

“Wengine (mapapa) wapo humu ndani, sijui kushoto au kulia kwangu. Majumba waliyojenga yamesababisha Mto Mbezi kuziba na kupasua daraja mara kwa mara nyakati za masika,” alisema.

Alisema katika zoezi la bomoamboa lililoendeshwa na Nemc, nyumba 24 zilibomolewa maelezo kuwa zilijengwa kando ya mito ya Mbezi na Mndumbwe na eneo la hifadhi ya miti ya mikoko lakini taasisi hiyo imeshindwa kubomoa hekalu la zaidi ya Sh. Bilioni moja.

“Jumba la Shilingi bilioni moja lile bomoeni…mnasema sheria ni msumeno, huu msumeno unakata kwa baadhi tu huku kwa wengine unakuwa butu?,” alihoji.

Alisema ingawa baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo kati ya 24 walikwenda mahakamani kupinga nyumba zao zisibomolewe sawa na mmiliki wa jengo la zaidi ya shilingi bilioni moja, lakini nyumba zao zilibomolewa.

“Msumeno huu unakata kwa wengine tu kwa mapapa unakuwa butu,” alisisitiza na kuongeza, “hii ni double standard.”
Oktoba mwaka 2012, Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema Serikali inatakiwa kumdhibiti na kumuondoa, kisha kuibomoa nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Getrude Lwakatare.

Alisema  wakati raia wengine wakibomolewa nyumba ambazo kama ilivyo ya Mchungaji Lwakatare, zilijengwa kinyume cha sheria, Mbunge huyo amehamia na kuishi kwenye nyumba yake.

Julai mwaka 2012, nyumba za wananchi waliojenga katika maeneo tengefu ya ufukwe wa Jangwani, Mto Ndumbwi na Mto Mbezi, zilibomolewa katika operesheni iliyoendeshwa na Nemc.

Hata hivyo, Septemba 2012, Nemc ilithibitisha kukwama kwa mpango wa kubomoa nyumba hiyo inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni 1.5 kutokana na zuio la mahakama.

Mwanasheria wa Nemc, Manchare Heche, alithibitisha kuwapo kesi iliyofunguliwa na mmiliki wa jumba hilo.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.

CHANZO NIPASHE

No comments:

Post a Comment