Pages

Thursday, May 21, 2015

MAKALA: Tunaweza Kusimama Wenyewe bila Misaada

MOJA ya mambo ambayo yamekuwa yakisumbua vichwa vya wanajamii walio wengi, ni kutambia misaada tunayopewa na nchi wahisani na madai kuwa tunakubalika au nchi hizo zinaikubali nchi yetu kwa kutupa misaada.

Kinachosumbua zaidi ni kwamba, misaada inayotolewa walio wengi
huwa hawajui inatumika vipi na wengine wanaweza kusema kuwa hawajaona faida ya misaada yenyewe.

Mara nyingine misaada hiyo inaweza kuwa ni ya kutupambaza licha ya tambo kuwa tuna rasilimali nyingi ambazo tukizitumia ipasavyo tutapiga hatua mbele.

Lakini tumekuwa tunasahau jinsi ambavyo tunawaita wageni kutoka nje kwa madai kuwa zipo fursa za uwekezaji ambazo tunaingia ubia na kushuhudia mgawanyo ukiwa ni mdogo kwa wenye mali.

Ndani ya mazingira kama hayo, masharti ya misaada inawekwa na kwa kuwa tunakuwa tumeshalemazwa na misaada inafikia hatua ya kuyatii masharti hayo ili kuendelea kukubalika kwa wahisani.

Haishangazi kuona kuwa wahisani hao wanatulemaza hata kwenye mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu hasa pale inapotokea wahisani wanapotujengea hata matundu ya vyoo na baadaye kuwekwa bango ‘kimejengwa kwa hisani’ ya watu wa nchi husika. Hoja ni kwamba hata yale tunayoyaweza tunaona ni sifa kusaidiwa?

Hapa inajiweka wazi kwamba tulishasahau ile kampeni ya ‘Mtu ni Afya’ ambayo ilirindima miaka ya 1970 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa maana hiyo ni kwamba, baada ya kuzama kwenye ‘Mtu ni Pesa’ basi tukawa tumetawaliwa na mali, tamaa na utengano vyote vikiwa vinaota mizizi na matunda yake yamekuwa kukosekana kwa uadilifu ambako kumeikumba jamii leo ikizongwa na ukosefu wa misingi ya uadilifu, uaminifu na ustaarabu na badala yake kujengeka vitendo vya rushwa, ufisadi na uroho wa madaraka.

Kwa kuzama kwenye lundo hilo, kila uchwao inakuwa ni kupokea masharti, na hata hivyo wakati huu yanapofanyika maandalizi ya kuandika Katiba Mpya ni wakati sawia kuwa na kipengele kinachotaja, “Tanzania haitakubali au kupokea misaada yoyote yenye nia na masharti ya kuondoa au kudhalilisha utu wetu, utamaduni wetu, utaifa wetu, uhuru wetu na amani yetu.”

Aidha, kipengele hicho kifafanue kwamba nchi yetu haitapokea misaada yoyote yenye makusudi, masharti au nia ya kutudhalilisha utu wetu, utaifa wetu, utamaduni wetu, mshikamano wetu, uhuru wetu na yoyote yenye nia ya kuathiri amani yetu hata kama misaada hiyo ina faida kiasi gani.

Kimsingi uhai wa taifa unategemea nguvu kazi ya vijana na ambao wengi leo hii wanashuhudia mabadiliko na kasi ya utandawazi yanavyofanya mabadiliko hayo kuingia ndani ya jamii hata pale, ambapo yanakuwa si kwa hiari, lakini kwa misingi ya kushinikizwa na wahisani.

Kwa kuona mbali na kutambua hali hiyo, Mwalimu Nyerere aliweka bayana kwenye moja ya hotuba zake mwaka 1985 aliposema, “Tunataka kuona katika taifa hili vijana jeuri na wenye kujiamini; si vijana waoga akina ndiyo bwana.

“Tunataka vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mifumo ya kijamii isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya Kitanzania. Tunataka vijana waasi dhidi ya mifumo kandamizi ya kutugawa na kuutenga umoja wetu, vijana wenye maadili nidhamu na wasema kweli hata wakichukiwa.”

Nchi maskini ni wapokeaji wa mambo kuanzia mifumo ya uchumi, teknolojia na hata tamaduni, hivyo kuingia kwenye mashinikizo kutokana na kuwa tegemezi kwa misaada.

Mwaka 2011, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroon kwenye Mkutano wa Nchi za Jumuia ya Madola alisema kuwa misaada ya nchi hiyo haitatolewa kwa nchi zisizozingatia haki za mashoga na wasagaji.

Kauli hiyo iliwachefua viongozi wengi wa nchi za Afrika ambao wanaunda sehemu kubwa ya wanachama wa jumuia hiyo awali zikitawaliwa na Uingereza.

Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alitoa kauli kuwa ni bora kufa njaa kuliko kukubaliana na suala la ushoga.

Marekani nayo iliibuka na suala hilo na kutangaza hadharani kuwa itapambana na ubaguzi wa wapenzi wa jinsia moja nchi za nje kwa kutumia misaada ili kushinikiza mabadiliko.

Hivyo Tanzania inapinga kwa nguvu zote uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja. Lakini ni miongoni mwa nchi zinazopokea msaada kwa wingi kutoka Marekani na Uingereza.

Kati ya nchi zinazopokea misaada na ambayo imepitisha sheria ya kupingana na matakwa ya nchi za magharibi ni Uganda ambayo inaweza kuonekana kuwa inamweka Rais Yoweri Museveni katika kitanzi cha kunyimwa misaada. Lakini mwenyewe alisema kuwa nchi hiyo inaweza kusimama bila msaada kwani ina utajiri mwingi.

Mashinikizo ya nchi za magharibi yasiyo na tija kwa jamii yanaweza kubainishwa kwenye historia kwamba chenye udhia kwao, wanataka kiwe udhia kwa wengine pia.

Walipopiga marufuku mila na tamaduni zetu na hata kuangusha mifumo ya utawala wakiona kuwa haifai lengo lilikuwa ni kuilisha jamii utamaduni wao na walifanikiwa.

Udhia huo unawekwa wazi na Mwanahistoria maarufu wa Ghana, Profesa Adu Boahen kwenye kitabu cha ‘Topics History of West Africa’ anasema kuwa baada ya kutengwa maeneo ya Sierra Leone na Liberia kwa ajili ya makazi ya watu walioondolewa kwenye utumwa, ndani yake walijumuishwa makahaba wa Ulaya ambao hawakutakiwa huko kwao.

Hao walionekana kuwa ni udhia kimaadili basi suluhisho lilikuwa ni kuwapeleka mbali, na hivyo walihamishiwa Sierra Leone.

Mwangwi wa hilo tukio ndio huu kwamba, kwa kuwa udhia huo umeshaenea miongoni mwa nchi zilizoendelea hivyo kila wanachokiona kukubalika kwao wanataka kikubalike au kienee sehemu nyingine zisizo na utamaduni huo hususani Afrika.

Aidha, ili kufanikisha azma ni pamoja na kushinikiza kwa kutumia udhaifu uliomo ndani ya nchi hizo maskini.

Hiyo inamaanisha kuwa kama shinikizo hilo likikubalika na kutambuliwa basi itakuwa imefikia hatua nzuri kwao ya kuhamisha udhia wa ushoga uliomo miongoni mwao na kuuingiza Afrika.

Hata hivyo, kama ni kusimama kidete na kusimamia maadili kama alivyosema Mwalimu Nyerere wa kuwa na jamii yenye maasi dhidi ya mifumo kandamizi, basi itakuwa heri umaskini kuliko misaada ya udhalilishaji.

Lakini kwa upande mwingine kauli ya Rais Museveni inasadifu hapa kwamba tunaweza kusimama wenyewe kwani tuna utajiri mwingi.

JAMBO LEO

No comments:

Post a Comment