Pages

Wednesday, May 6, 2015

Meya wa Kinondoni Yusuph Mwenda ndiye meya bora barani Afrika......Pamoja na vitu vingine amepewa pesa taslimu Sh Milioni 200

MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda amekabidhiwa tuzo ya kuwa meya bora barani Afrika.

Tuzo hiyo alikabidhiwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.

Meya Mwenda amefanikiwa kupata tuzo hiyo katika kundi la mamlaka za miji ya kati ambayo ina majiji yenye idadi ya watu isiyozidi milioni moja.

Akitaja sifa za tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty, alisema vigezo hivyo ni pamoja na uongozi na dira katika utoaji wa huduma kuchochea maendeleo, uadilifu, ubunifu na usimamizi bora wa shughuli za halmashauri.

Natty alisema sifa nyingine ni uhamasishaji wa jamii katika kushiriki masuala ya halmashauri, uwezo wa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, uwezo wa kusimamia ulinzi na usalama wa wananchi ikiwamo kujenga mahusiano mazuri katika jamii.

Mamlaka ya miji iliyoshinda na tuzo kwenye mabano ni Accra, Ghana (majiji makubwa), Kinondoni, Tanzania (majiji ya kati) na Praia, Cape Verde (majiji madogo).

Zawadi alizokabidhiwa Mwenda ni kikombe, cheti na fedha taslim kiasi cha dola za Marekani 100,000 sawa na Sh milioni 200.
Waziri Ghasia aliipongeza halmashauri hiyo ikiwamo na kuishauri kutumia zawadi ya fedha walizopata kuzalisha ajira kwa vijana na akina mama wa Kinondoni.

MTANZANIA

No comments:

Post a Comment