Pages

Friday, May 15, 2015

Msitake kumridhisha kila mtu hamtaweza na hata mtakaowaridhisha hawatawashukuru....Raisi Kikwete kuhusu kubomoa nyumba za mabondeni na kingo za mito

Kikwete aagiza bomoabomoa Dar.

Rais Jakaya Kikwete ametoa maagizo magumu kwa viongozi wa Halmashauri ya Jijini la Dar es Salaam kwa kuwataka kuzibomoa nyumba zote zilizojengwa katika kingo za mifereji, mito na mikondo ya kupitishia maji.
Alitoa agizo hilo jana, baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha ya Boko, Basihaya Tegeta na Mkwajuni katika wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Nyumba za wakazi wake zimezingirwa na maji kutokana na baadhi ya watu kujenga katika mifereji ya kupitisha maji na mabondeni.

Rais Kikwete akiwa eneo la Boko alimuuliza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na Mhandisi wa Manispaa hiyo, Baraka Mkuya, sababu za maji kujaa katika nyumba za watu na hatua zilizochukuliwa kuyaondoa.

Makonda alijibu kuwa, Manispaa ya Kinondoni imeandaa bajeti ya Sh. bilioni 3.5 ili kuondoa maji hayo pamoja na kutengeneza miundombinu.

Mkuu huyo wa wilaya alieeza sababu za kujaa maji katika nyumba kuwa imesababishwa na baadhi ya watu kujenga nyumba zao juu ya mifereji na mikondo ya kupitishia maji yanayoelekea baharini.

“Mkuu wa wilaya na watendaji wako hapa kama mnajua sababu ni watu kujenga juu ya mitaro bomoeni nyumba zote msitake kumridhisha kila mtu hamtaweza na hata mtakaowaridhisha hawatawashukuru,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema wale ambao hawataki nyumba zao zisibomolewe licha ya kujengwa juu ya mifereji watakuwa ni wajinga kwani hata katika nyumba hizo hawawezi kuishi kutokana na kujaa maji. Aidha, alimwagiza mkuu huyo wa wilaya na wataalamu wake kutumia pampu 27 za manispaa hiyo kunyonya maji kutoka katika nyumba ambazo maji yamejaa badala ya kufikiria kuandaa miradi ya fedha nyingi.

Rais Kikwete aliagiza manispaa hiyo kukaa chini na watendaji wake ili kupata jawabu la kumaliza tatizo la kujaa maji katika nyumba za watu, vinginevyo maeneo hayo yatageuka kama maeneo ya kufugia samaki.

“Mhandisi hivi hauna maarifa, kwanini mmefikiria kuandaa fedha nyingi za kutengeneza miundombinu badala ya kuangalia namna ya kuondoa maji katika nyumba za watu, tumia maarifa yangu niliyoelekeza, achana na hayo ya kwako ambayo hayasaidii kumaliza tatizo kwa muda mfupi,” alisema.

Akiwa ofisi za Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), Rais Kikwete, alihoji sababu za maji kujaa katika ofisi hizo wakati kuna wataalamu wa maji ambao wanaweza kumaliza tatizo hilo.

Hata hivyo, Mhandisi Maro Wambura alimweleza Rais kuwa maji hayo yanatoka kwenye kiwanda cha saruji cha Wazo ambayo yanatakiwa kuelekea baharini, lakini yamekuwa yakikwama kwenye ofisi hizo kutokana na baadhi ya watu kujenga katika mikondo ya kupitishia maji.

Wambura alisema kutokana na tatizo hilo ambalo linajitokeza kila mwaka kila unapofika msimu wa mvua, wanalazimika kufunga ofisi na kwamba hawana uwezo wa kuyaondoa bila kushirikiana na manispaa.

Naye Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Mkuya, alisema awali walimwita mkandarasi wa Kichina kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya eneo hilo, lakini kazi haikufanyika kwa sababu mkandarasi huyo alikuwa anahitahi kulipwa fedha nyingi.

Rais Kikwete akiwa eneo la Mkwajuni, Mkuu Wilaya Kinondoni, Makonda alimweleza kuwa eneo hilo kila mwaka limekuwa likikumbwa na mafuriko kutokana na bonde na asilimia kubwa ya wakazi wake wamejenga nyumba zao katika mkondo wa mto Msimbazi.

Makonda alisema kutokanana na hali hiyo, kaya 102 zilipewa viwanja eneo la Mabwepande ili wahame bondeni, lakini kaya 42 kati ya hizo zimeshikilia maeneo Mambwepande na Mkwajuni.

‘WA MABONDENI HAMENI’
Rais Kikwete aliagiza viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha watu wote waliojenga nyumba zao bondeni Mkwajuni wanahamishwa kwani suala la kuzuia mvua lipo nje ya uwezo wa serikali.

“Mlioko mabondeni hatuna namna ya kuwasaidia kwa sababu mvua zilizonyesha mwaka huu ni nyingi kupita kiasi, hivyo mkubali tu yaishe muondoke, hakuna jinsi hali hii itandelea kila mwaka na itajirudia,” alisema Rais Kikwete.

Alisema wananchi watakaokuwa tayari kuhama serikali itawasaidia kwa kuwapatia viwanja ili waondoke eneo hilo hatari.

Mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 12, huku mamia wakikosa makazi kutokana na nyumba zao kuzingirwa na nyingine kujaa maji.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, ameshatangaza na kusisitiza kwamba mwaka huu hakuna mtu atakayesaidiwa na serikali kutokana na kukaidi maagizo ya kuhama maeneo ya mabondeni ambayo ni hatarishi.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment