Pages

Tuesday, May 12, 2015

Ulishawahi Kusikia hii?.....MWANAMKE SUMBAWANGA KAJIFUNGUA MAPACHA WATATU KWA SIKU MBILI TOFAUTI.....MMOJA ALIJIFUNGUA TAREHE 6.......ILIPOFIKA TAREHE 8 AKAJISIKIA TENA UCHUNGU AKAJIFUNGUA WAWILI...

MKAZI wa kijiji cha Kisalala, Kata ya Laela wilayani Sumbawanga katika mkoa wa Rukwa, Lydia Shazi (29) amejifungua watoto watatu wote wa kiume kwa siku tofauti na hospitali mbili tofauti.

Akizungumza na HABARI LEO hospitalini hapo jana mama huyo ambaye sasa amekuwa na idadi ya watoto saba alieleza kuwa mtoto wake wa kwanza alijifungulia katika Kituo cha Afya kilichopo mji mdogo wa Laela wilayani Sumbawanga uliopo umbali wa kilometa 97 kutoka mjini Sumbawanga.

Aliongeza kueleza kuwa mtoto huyo alizaliwa Mei 6 mwaka huu katika zahanati hiyo akiwa na uzito wa kilo 2 na gramu 200.

“Wakunga na wauguzi katika kituo cha afya cha Laela walifahamu kuwa nitajifungua mapacha hivyo baada ya kubaini kuwa nina upungufu wa damu mwilini waliamua kunikimbikiza katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga kwa uchunguzi na matibabu,” anaeleza.

Aliongeza kuwa alifika hospitalini hapo Mei 6, mwaka huu ambapo alilazwa ambapo baada ya siku mbili tangu nijifungue mwanangu wa kwanza nilihisi uchungu na nikajifungua mtoto wa pili na watatu Mei 8 , mwaka huu.

“Mtoto wa pili alizaliwa akiwa na uzito wa kilo mbili kamili wakati wa tatu alikuwa na kilo 2 na gramu 600… hawa wawili nilijifungulia hapa hospitali ya mkoa Mei 8, mwaka huu wakati wa kwanza alizaliwa katika kituo cha afya Laela Mei 6, mwaka huu… namshukuru Mungu wanangu wote ni wazima wenye afya njema isitoshe nilijifungua salama tena kwa njia ya kawaida,” alibainisha mzazi huyo.

Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo ambapo mzazi huyo anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na kubainika kitabibu kuwa ana upungufu wa damu, ameiomba Serikali na jamii imsaidie chakula na mavazi kwa ajili ya watoto hao kwa kuwa uwezo wake wa kipato kuwahudumia ni mdogo.

“Namshukuru Mungu nimeweza kujifungua salama …licha ya watoto hawa watatu niliojifungua hospitalini hapa, bado nina watoto wengine wanne nyumbani …hali ya kipato mie na mume wangu si nzuri hata kidogo …hivyo naiomba Serikali na jamii inisaidie katika malezi na makuzi ya watoto hawa watatu,” alisisitiza.

Mama huyo alikiri alikuwa akifahamu kuwa angejifungua pacha, lakini hakudhani wangekuwa watoto watatu, “maandalizi yangu kabla ya kujifungua yalikuwa hafifu sana naomba mwenye nguo, mafuta ya kupaka watoto wanisaidie,” alieleza kwa hisia.

Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo, mkunga na muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi hospitalini hapo, Cremensia Kagoma alithibitisha kuwa hali ya kiafya ya mama huyo inazidi kuimarika mara baada ya kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na kuongezewa damu.

Kwa mujibu wa muuguzi huyo wa zamu, alieleza kuwa mzazi huyo alifika hospitalini hapo hali yake ikiwa duni sana hivyo iliwalazimu wahudumu wa afya hospitalini hapo kuchanga kiasi cha Sh 70,000 ambazo zimetumika kuwanunulia watoto hao nguo nzito ili kuwakinga na baridi.

No comments:

Post a Comment