Pages

Sunday, June 7, 2015

Askofu Kagera asema anamuunga mkono Lowassa

Askofu wa Jimbo Katoliki  Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi, amesema anamuunga mkono, kada wa CCM, Edward Lowassa katika safari ya matumaini.

Aidha
amewahimiza Watanzania wanaofikiri wanazo sifa za kuwaongoza wananchi wajitokeze ili wapimwe uwezo wa kuitumikia nchi.

 Mbali na hilo ameungana na Lowassa katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana ambayo mara nyingi amekuwa anaizungumzia.

Askofu Niwemugizi alitoa msimamo huo  jana kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya seminari ndogo ya Mtakatifu Karoli Lwanga.

 Alisema Watanzania wanajua Lowassa ametangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM  na wanamuombea na kumtakia mafanikio katika safari yake hiyo.

 “Tunatamani kuiombea nchi yetu iwapate viongozi makini, waadilifu, wakweli, watakaoongoza kwa misingi ya haki na usawa.

Watakaoijenga jamii yenye kuaminiana na kuheshimiana, inayojali mema ya wote, watakaolinda amani na kudumisha umoja wa taifa,”alisema na kuongeza:

“Nimefurahi Lowassa kukubali mwaliko wangu, tumekualika wewe maana najua yatasemwa mengi yasiyo sahihi kwa kuja kwako huku, sote tunajua kuwa sasa ni joto kubwa la uchaguzi.”

 “Wanaweza kufikiri nimekuita kukupigia kampeni katika safari yako ya matumaini uliyoitangaza kule Arusha, hayo siyo malengo yangu, ila wanaotaka kuliona hivyo basi juu yao, na  kwanini sikuita mwingine ila wewe, nafikiri tuna uhuru wa kupanga na kuchagua,”alisisitiza.

Alisema amemualika Lowassa kumshukuru kwa kumpokea bila miadi , kumsikiliza wakati akiwa Waziri Mkuu mwaka 2007 na kutatua msigano wa ardhi ya Two Biharamulo iliyokabidhiwa na jeshi kwa askofu mtangulizi wake mwaka 1996.

Alisema alimuagiza Waziri wa Ardhi kipindi hicho Dk. John Magufuli, kulitatua na  jimbo likapewa ardhi yake na sasa jimbo  lina hati ya kumiliki ardhi hiyo hata kama ilipunguzwa kiasi.

Akizungumzia vijana, elimu na ajira alimwambia Lowassa:“Ujue kuwa tuko pamoja na wewe ndiwe mwasisi wa shule za kata, sasa zina wanafunzi wengi sana, lakini wanapomaliza kidato cha nne wengi wao wanarudi vijijini na wanajikuta hawana ajira, hali hii inawatesa sana na wana hasira.”

 Akizungumza,  Lowassa aliwaomba kuendelea kumuombea kwa sala na maombi ili Mungu akijalia katika safari yake ya matumaini kazi ya kwanza iwe ni kuunda chombo maalum cha elimu kwa kushirikisha wadau na wataalam.

“Baba Askofu kwa heshima na taadhima, nisingeweza kukataa heshima hii uliyonipa, hata kama kwa taarifa  fupi sana na pia kuwa katika ratiba ngumu ya kuzunguka nchini kutafuta wadhamini, baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM,”alisema.

Alisema chombo hicho kitapitia mfumo wa elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na vyuo vikuu ili kupata muongozo thabiti.

Waliohudhuria katika Jubilee hiyo ni Askofu msaidizi wa Bukoba, Methodius Kilaini, Akkofu wa jimbo la Kayanga, Almachius Rwetongesa, mwangalizi wa jimbo la Singida Desderius Rwoma na Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Darry Rwegasira.


CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment