Pages

Sunday, June 7, 2015

SERIKALI IMEKIRI KURUHUSU KUSINDIKA NYAMA YA PUNDA....Nyama hiyo imepimwa na wataalam haina madhara kwa binadamu

SERIKALI imekiri kuruhusu uanzishwaji wa kiwanda cha kusindika nyama ya punda kilichopo mkoani Dodoma.

Imekiri hivyo baada ya Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF), kuibua hoja hiyo juzi jioni wakati wa kupitisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

Katika hoja yake, alitaka kujua juhudi zilizofanywa na Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA), kukagua viwanda vya usindikaji wa chakula ikiwa ni pamoja na kiwanda hicho.

Aliilaumu Serikali kukaa kimya bila kutoa taarifa za kiwanda hicho ambacho mwekezaji wake ni raia wa kigeni kutoka China, huku akihoji iwapo nyama hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Alisema uzalishaji wa nyama hiyo licha ya kuashiria kutoweka kwa wanyama kazi hao, lakini pia unaweza kuzua hofu ya kiimani miongoni mwa jamii kutokana na nyama hiyo kuingizwa sokoni.

“Sasa hivi kuna kiwanda hapa nchini kinachakata nyama ya punda, ipo hatari ya hawa punda virongwe (wanyama kazi) kuadimika kwa kuwafanya kitoweo,” alisema Rajab.

Hata hivyo, aliishangaa Serikali kuruhusu kiwanda hicho bila kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na matumizi ya nyama hiyo.

“Mimi napata wasiwasi mkubwa kuhusiana na nyama hii, kwanza uzao wa punda ni mdogo, sasa kuwavuna kwa ajili ya kitoweo kunatishia wanyama hawa kutoweka.
“Lakini hata hivyo mimi nashangaa, hapa Tanzania tunao ng’ombe wengi, mbuzi, kondoo na kuku wa kutosha tumeshindwa kuwekeza katika mifugo hii halali hadi tuanze kuchinja punda ndiyo uwekezaji uliofika huo?” alihoji.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titas Kamani, alikiri uwepo wa kiwanda hicho na kusema kuwa nyama hiyo imepimwa na wataalamu na haina madhara kwa binadamu.

Alisema nyama ya punda inayozalishwa katika kiwanda hicho inasafirishwa nje ya nchi na haitumiki kwa mahitaji ya soko la ndani.
“Hapa kati kati kulikuwa na wimbi kubwa la wanyama kazi hawa kusafirishwa kwenda Kenya huko kuna viwanda hivi, sasa tulioana bora tuwachinje na kuwasindika wenyewe kisha tuuze nyama tupate fedha,” alisema Dk. Kamani.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe, alisema wizara yake kupitia TFDA imefanya uchunguzi na kujiridhisha kuhusiana na ubora wa nyama hiyo.


Akizungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Bunge jana, Naibu Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Uvuvi, Kaika Telele, alisema mahitaji ya soko la nje ndiyo yaliyoisukuma Serikali kuruhusu kiwanda hicho.

“Mwanzo sisi tulikataa kwa sababu uzao wa punda ni mdogo, kwa hiyo tuliona mazingira ya wanyama hawa kutoweka ni mkubwa.
“Taarifa za kwanza ilikuwa punda takriban 200 walikuwa wanachinjwa kwa sasa sijui ni wangapi, baadaye tuliona kama hilo soko lipo nje ya nchi na hiyo fedha ipo, kwanini tusifanye wenyewe,” alisema Telele.

No comments:

Post a Comment