Pages

Wednesday, June 24, 2015

Jaji Ramadhani Sasa Tishio

Jaji Augustino Ramadhani amesema endapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watu wasitarajie kuwa “uchungaji” wake utamfanya awe na huruma na wakosaji.
Katika mahojiano maalum na JAMHURI, Jaji Ramadhani amesema atapambana na wala rushwa kama alivyofanya wakati akiwa Jaji.
“Mimi ni Mchungaji ndiyo. Mimi ni mcha Mungu, nimesimamia haki nikiwa jaji kwa sababu Mungu anapenda haki.


“Watu wasitarajie kwa kuwa ni Mchungaji nikiwa rais nitakuwa mpole, kwa hiyo mtu anaweza kula rushwa au kuvuruga mambo halafu nikamtazama tu, hakuna hilo,” amesema.

Ameongeza: “Hata nilipokuwa jaji nimetamka kuwatia hatiani wahalifu. Wengine nimewahukumu kunyongwa hadi kufa nikiwatazama machoni. Adhabu ya kunyonga nimeitamka hivi nikimtazama mshitakiwa.

“Hakuna kitu kizito kama kutamka mtu kunyongwa. Kunyonga ni kitu kizito, lakini nimeweza kufanya hivyo kwa sababu ya kufuata sheria na haki.

“Sasa ninapoulizwa kuhusu wala rushwa nasema hiyo ni kazi nyepesi kwa sababu kazi ngumu ya kuhukumu kunyonga niliiweza, hii ya wala rushwa naimudu kabisa.”

Anasema alipokuwa akiongoza Mhimili wa Mahakama alipambana na rushwa.
“Nilikuwa Jaji Mkuu wa kwanza kuunda Tume ya Uajiri wa Mahakama kwa ajili ya kushughulikia vyeo na nidhamu. Tulitembea mikoa 18 na huko tuliwaambia wakuu wa wilaya na mikoa kuwa wanao uwezo na madaraka ya nidhamu kwa mahakimu.

“Tuliwahimiza watekeleze sheria kwa vitendo ili kuondokana na kero ya rushwa ambayo kwa kweli ni kero kubwa sana.

“Nikiwa rais, sasa nitakuwa nimepewa rungu kubwa zaidi la kupambana na adui rushwa na uonevu,” amesema.
Jaji Ramadhani amesema ameingia kwenye uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ridhaa yake mwenyewe, na kwamba hakuna shinikizo lolote alilopata kutoka upande au kwa mtu yeyote.
 
Mambo yanayomgusa zaidi
 Jaji Ramadhani amesema pamoja na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM endapo atashinda, mambo muhimu matatu ni kati ya mengi atakayoyapa kipaumbele.
Jambo la kwanza anasema ni Umoja wa Nchi. “Kwa sasa mtaona hatuna ule umoja kama kule nyuma. Umoja wetu umeyumba. 

Nitahakikisha narejesha misingi ya umoja ili tuendelee kuwa Taifa moja lenye watu wanaoishi kwa kupendana,” anasema.
Pili, anasema kazi yake nyingine itakuwa kurudisha Heshima ya Nchi na Wananchi.


“Kuna wakati ukisema wewe ni Mtanzania, unaona fahari kubwa sana. Watu wa mataifa mengine wanakufurahia kweli kweli. Hili limeyumba kidogo, nitajitahidi kwa dhati kabisa kuimarisha heshima ya Tanzania na Watanzania ili ile heshima tuliyokuwa nayo iendelee,” amesema.

Tatu, anasema anaguswa mno na hali ya umaskini unaowakabili Watanzania. Kwa maana hiyo, anasisitiza suala la kupambana na maadui watatu waliokwishatangazwa tangu mwaka 1961- Ujinga, Maradhi na Umaskini – kuwa ni moja ya kazi zake kubwa atakazozifanya endapo ataingia madarakani.
 
Umaskini wamkera
Jaji Ramadhani anasema Tanzania ni nchi yenye rasilimali nyingi mno, na kwa hiyo hakuna sababu kwa wananchi wake kuendelea kuwa maskini.

“Mungu ametupendelea kwa rasilimali nyingi sana. Rasilimali zote zipo Tanzania. Mungu alitaka Watanzania tuishi maisha mazuri kwa kutumia rasilimali hizi. Tuna rasilimali chungu nzima. Hakuna nchi katika Afrika yenye rasilimali kama sisi. Kinachotakiwa sasa ni determination (uamuzi) wa kuzitumia rasilimali hizo kuondoa umaskini,” anasema.

No comments:

Post a Comment