Pages

Thursday, June 25, 2015

PAPA MSOFE AMEFUTIWA KESI YA MAUAJI

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifuta kesi ya mauaji ya kukusudia iliyokuwa ikimkabili mfanyabiashara Marijan Abubakar, maarufu kama Papa Msofe (50) na mwenzake, Makongoro Joseph.

Hakimu Mkazi, Renatus Rutta aliifuta kesi hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Aliifuta baada ya Wakili wa Serikali Wankyo Simon, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) kuonyesha kuwa hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.

Msofe na Makongoro wamesota rumande kwa takriban mwaka mmoja sasa kutokana na kile kinachelezwa ni upelelezi kusubiriwa ukamilike. Msofe kwa mara ya kwanza alifikishwa kortini Agosti 2012.

Hata hivyo baada ya kuachiwa huru Makongoro aliruhusiwa huku Msofe akifunguliwa kesi nyingine ya kughushi.
Katika kesi hiyo mpya, Msofe anadaiwa kuwa Desemba 23, 2004 katika Wilaya ya Ilala kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka ya kuhamisha haki ya umiliki wa nyumba namba 288 ambayo ni mali ya mfanyabiashara wa madini Onesphory Kituli (kwa sasa marehemu).

Ilidaiwa kuwa Msofe kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka hiyo akionyesha Desemba 13,2004, Kituli alihamisha haki yake ya umiliki wa nyumba hiyo kwake wakati akijua ni uongo.

Mbali na shtaka hilo, Msofe anadaiwa kuwa kati ya Desemba 23,2004 na Machi 30, 2005 akiwa na nia ya kidanganya alitoa nyaraka hizo za uongo kwa Kamishna wa Ardhi kwa lengo la kuhamisha umiliki kutoka kwa Kituli kwenda kwake.

Upande wa mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 9, 2015 na ametakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 10 milioni.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment