Pages

Monday, July 13, 2015

Kupenya kwa Dk Magufuli ni kama vita vya panzi furaha ya kunguru..mmh

Hatimaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha Dk. John Magufuli, kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Magufuli alipitishwa na CCM baada
ya kupata ushindi wa kishindo wa kura 2,104 kati ya kura halali 2,416 zilizopigwa, sawa na asilimia 87.1. Amina Salum Ali alimfuatia Magufuli kwa kupata kura 253 (10.5%) huku Dk. Asha-Rose Migiro akipata kura 59 za ndiyo, sawa na asilimia 2.4. Kura zote zilizopigwa zilikuwa 2,422 huku sita kati ya hizo zikiharibika.

Magufuli ambaye hajawahi kugombea nafasi yoyote ndani ya CCM mbali ya kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho kutokana na kuwa Mbunge, alikuwa miongoni mwa makada 38 wa CCM waliorudisha fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania urais, lakini pia akiwa miongoni mwa makada watano waliopitishwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM kwenda kupigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho.

Majina yaliyopelekwa Nec mbali na Magufuli ni Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard Membe.

Majina hayo yalipojulikana usiku wa Ijumaa wiki iliyopita, yaliibua taharuki mjini hapa kwa sababu miongoni mwa watu waliokuwa wanatazamwa kama wagombea wenye nguvu hawakuwako.

Hawa ni pamoja na Edward Lowassa, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wasira, Jaji Augustino Ramadhani na Samuel Sitta.

Wachambuzi wa siasa za CCM kwenye vijiwe, mikutanoni na kwenye mijadala mingi, walikuwa wanatazama uchaguzi ndani ya chama hicho kama mpambano baina ya makundi mawili makubwa, licha ya orodha ya wagombea kuwa ndefu.

Makundi haya ni lile la Lowassa, ambalo limetikisa nchi kwa muda mrefu hasa wakati wa kutafuta wadhamini ndani ya CCM na jingine likiongozwa na Membe.

Wachunguzi wanasema kuwa kimsingi mpambano ndani ya CC, NEC na hata mkutano mkuu ulikuwa unatarajiwa ujitokeze kati ya watia nia hao wawili, Lowassa na Membe.

Hata hivyo, usiku wa Ijumaa mjini hapa, hali ilikuwa tofauti kabisa baada ya kuibuka jina la Membe tu bila la Lowassa kuwako.   

Uamuzi wa kukatwa kwa jina la Lowassa siyo tu uliibua mjadala mrefu na mvutano, bali hata wajumbe watatu wa Kamati Kuu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba waliibuka na kusema wazi kwamba hawakukubaliana na maamuzi ya CC wakisema ulikuwa umelenga kuwanyonga wengine.

Kuibuka kwa wajumbe hao na kusema hadharani walichotaka kusema kuhusu mchakato wa kumtafuta mgombea, ni dhahiri uliibua picha ya hatari ya CCM kupasuka.

Habari za uhakika ambazo NIPASHE ilizipata kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa NEC ni kuwa na hasira juu ya maamuzi ya Kamati Kuu na ndiyo maana wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, juzi (Jumamosi) asubuhi anaingia kufungua mkutano wa NEC, alichokutana nacho ni nyimbo za kumsifu Lowassa na siyo yeye kama ilivyo ada.

“Unajua ilivyopigwa nina imani na Lowassa kwa kishindo, ilichanganya meza kuu. Mwenyekiti alishangaa na alisema hiyo haijapata kutokea. Ule ulikuwa ni ujumbe kwamba CC imechemka,” alisema mjumbe mmoja wa NEC aliyeomba kutotajwa jina.

Alisema kutokana na hali hiyo, wajumbe walikuwa wamepania kuifukuza CC yote kwa kuwa walichofanya hakikubaliki.

Hata hivyo, alisema kuwa baada ya kushindikana kuiong’oa CC huku wanachama wengine hasa wa Mkutano Mkuu wakiwa wamepiga kambi eneo la Nyerere Square, kambi ya Lowassa ndani ya NEC iliamua kutumia kura zao kumwadhibu Membe ambaye kwa kitambo kumekuwa na viashiria kwamba ni chaguo la wakuu wa serikali.

“Ilikuwa kama kumwadhibu Mwenyekiti na mgombea wake. Kwa kweli hisia zetu ni kwamba Membe alikuwa anabebwa na wakubwa ndani ya chama na hata serikalini kiasi cha kujiamini kwamba ni rais wa tano wa Tanzania,” alisema mjumbe mwingine wa NEC kutoka Mara.

Kura zilipopigwa na matokeo kutangazwa ilikuwa ni maajabu kwa wengi, Membe ambaye alikuwa anaonekana ni moja ya majabali alipata kura 120 akivuta mkia wa wagombea wengine wanne, akifuatiwa na January Makamba kura 124, Dk. Migiro 280, Balozi Amina kura 284 na Dk. Magufuli 290.

Idadi ya kura hizo, kwa hakika hazionyeshi kama Membe alikuwa na nguvu sana ndani ya NEC kwani kati yake na Mafuguli kuna tofauti ya kura 170.

Alisema kazi ya timu ya Lowassa ndani ya NEC ilikuwa ni kumalizana na Membe mapema kabisa ili kutimiza kile wanachosema  Waswahili ‘ukimwaga ugali ninamwaga mboga’.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa kupenya kwa Dk. Magufuli kunaweza pia kufananishwa na ile dhana ya ‘vita vya panzi furaha ya kunguru’. 

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment