Pages

Friday, July 3, 2015

Kwanini tunapamba nyumba zetu?

Ni swali ambalo hatujiulizi sana lakini inabidi tujiulize. Ni vizuri tuwekane sawa kuwa tendo la kupamba nyumba ni la kibunifu na ni muhimu. Lina nia ya kuleta mpangilio kwenye maisha ili kujitoa kwenye mvurugano na machafuko ya jumla ya duniani, kuweza kuweka nguvu zetu za kupamba hata hapo padogo tunapoishi ambapo tuna uwezo napo.

Kwa kufanya hivyo tunaonyesha na
kuwafundisha watoto wetu somo zuri. Kama vile: umuhimu wa kuweka na kuacha vitu kwenye mpangilio mzuri kuliko walivyovikuta, kwa ukweli kwamba kila kitu kinaweza kubadilishwa kwa uzuri zaidi, kwamba kuweka mpangilio kwenye maisha ni muhimu, kwamba vitu vinavyoonekana kwa macho vinahusika na kwamba baada ya kukamilisha lolote una cha kujivunia.

Ni sanaa ya kutengeneza mahali petu wenyewe pawe kama patakatifu na kushirikishana eneo letu na wengine. 

Kama muundaaji wa makala hii, huwa nafurahishwa ninapotembelea makazi ya watu na kuona jinsi nyumba ya mtu mmoja inavyoweza kutofautiana kabisa kimpangilio na ya mtu mwingine ingawaje maeneo ya msingi ni yale yale.

Tukijua ni kwanini tunapamba itatufanye tupende kuendelea kupamba. Kupamba nyumba ni kama kitu kingine chochote kwenye maisha. Ni kama unavyouweka mwili na nguo zako katika usafi na mpangilio. Ukishajua mkakati wako utapata mwelekeo.

Badala ya kubuni ni kwanini unataka hiyo rangi, ni kiti kipi kinakufaa au ni kwa namna gani uweke fenicha zako – unatakiwa kuwa na sababu kubwa ya muongozo wa kwanini unafanya chochote unachotaka kufanya.

Kwahivyo baada ya kusema yote haya hizi hapa chini ni sababu za kawaida za kwanini tunapamba. Zifurahie na elewa msukumo wako, na naamini itakusaidia kuwa mpambaji mzuri wa mahali unapoishi.

Tunapamba ili kufanya nyumba zetu ziwe rahisi kuishi ndani mwake na kurahisisha maisha yetu.
Tunapamba ili kuleta mazingira ambayo yanatamanisha kujifunza, upendo, furaha na mshikamano.
Tunapamba kufurahisha wengine.
Tunapamba kuonesha vipaji vyetu na kukamilisha ndoto zetu.
Tunapamba ili kujiaminisha wenyewe kuwa tunaweza kufanya jambo na likaonekana.

Tunapamba ili kuonyesha ladha zetu, tunachopenda na tusichopenda.
Tunapamba ili kunogesha mazungumzo, watu wanapenda kufanyia mazungumzo yao mahali panapovutia.
Tunapamba ili kujipa changamoto.
Tunapamba ili kuongeza thamani ya nyumba.
Tunapamba kwa sababu tunatakiwa kufanya hivyo.
Tunapamba kwasababu tunapenda vitu vizuri.
Tunapamba kwasababu inatufanya tujisikie furaha.
Tunapamba kwasababu tunataka watoto wetu wakulie kwenye mazingira mazuri.

Kiukweli hizi zote ni sababu za kupamba nyumba zetu na huenda nawe masomaji wangu unazo zako za kuongezea.

Sasa kuna wale wanaopamba nyumba halafu wanaogopa hata kuitumia wenyewe. Kama utapamba halafu ushindwe kutumia kuamsha furaha yako, mshikamano na burudani sasa kuna raha gani? Kuna baadhi ya nyumba ambazo alama pekee za kwenye zulia ni za mashine iliyosafishia, hakuna mtu anapita hapo! Ni vizuri kufahamu kuwa nyumba yako uliyopamba inakuwezesha kutengeneza kumbukumbu za maisha.

Sio lazima usafiri upigie picha kutengeneza kumbukumbu kwenye maeneo mbalimbali ya dunia ambapo wengi hatumudu, unaweza kutengeneza kumbukumbu hapo nyumbani kwako. Unakuwa na kumbukumbu kuwa nilishawahi kupaka rahi hii, kwa mfano, au nilikuwa na sofa za aina hii kipindi fulani, na kadhalika.
Siku ambayo kitanda chako kikubwa kinawasili na unahamishia kidogo kwa watoto ni kumbukumbu tosha.

Kwahivyo kwenye kupamba nyumba yako ili uweze kuifurahia zingatia vitu ambavyo hutakosa uhuru wa matumizi. Kwa mfano huna haja ya kuwa na rangi ya kitambaa cha sofa au zulia ambayo unaamini zitakunyima uhuru wa kufurahia nyumba. Kwa mfano rangi zinazochafuka ndani ya muda mfupi. Unahitaji mapambo ya uhalisia wa maisha yako zaidi, nyumba ambayo wakaaji wataifurahia. Nyumba ambayo unaweza kualika wageni ndani na wakajisikia huru. Nyumba ambayo watoto wako wanaweza kualika wenzao wakacheza na kufurahi wakiwa ndani. 

Siku hizi ambapo ni ngumu kupata weza wanne kuwaalika nyumbani kwa wakati mmoja (kweli ni ngumu kwa ajili watu wana majukumu mengi ratiba zao zina mengi, unaweza kutumia mwezi mzima kutafuta watu kwa chakula cha usiku bila kuweza kuwapata kwa pamoja) ni vyema kuwa na tabia ya kusherehekea ndani ya familia zetu wenyewe.

Kwa hivyo usipambe kwa jinsi ambayo utashindwa kuifurahia nyumba, maisha ni mafupi na familia na marafiki ni zawadi.

Sasa nawe msomaji wangu niambie sababi za kwanini unapamba nyumba yako. Kweli ni vizuri kukuza uzuri na unadhifu katika kona yako ya dunia ambapo ndio nyumbani kwako, kwa sababu unaweza.

Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tafadhali tembelea www.vivimachange.blogspot.com

No comments:

Post a Comment