Pages

Saturday, October 3, 2015

Lowassa amtosa binti wa Sokoine....amwambia kama akitaka amfuate UKAWA laa amsamehe

MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ambaye anaungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana alitangaza kuitua mbeleko aliyokuwa akimbebea Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Monduli, Namelok Sokoine.

Vyama vinavyounda Ukawa ni pamoja na Chadema yenyewe, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Lowassa alitangaza uamuzi wake huo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Barafu, uliopo Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli, baada ya baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kumhoji namna anavyowaacha na Namelok ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Moringe Sokoine.

Akijibu swali hilo, Lowassa alisema atakutana na Namelok kumshawishi ili abadili msimamo wake wa kuendelea kuwa CCM na badala yake ajiunge naye kwenye vuguvugu na mabadiliko katika Ukawa.

“Nimeongoza jimbo hili kwa miaka 20, nastahili kumfahamu atakayekuja badala yangu, sasa kuna maneno maneno, wamepotea mabasi, wamepotea malori, niachieni kidogo nifanyie kazi.

“Kesho nitakwenda Pemba nitarudi jioni, nitakutana na madiwani na Namelok ili mambo yetu tuliyoongea tuulizane yamekuwaje. Nasema hivyo kwa sababu nisingetaka kuvunja umoja wetu. Katika uchaguzi uliopita tulikuwa na kauli, ‘tulihuzunika pamoja, tulifurahi pamoja na tutasonga mbele pamoja,’ ningependa tubaki na kauli hiyo, kwa hali hiyo, hili mniachie kesho tutakubaliana, akikataa kuingia basi la wengi, basi itakuwa bahati mbaya,” alisema Lowassa.

Lowassa alitumia pia mkutano huo kumnadi Mgombea Ubunge wa Chadema wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga, akimtaja kuwa ni jembe huku akikwepa kumtaja kwa namna ya kumshambulia kisiasa au kuwashawishi wapigakura kutomchagua Namelok.

Baadaye jioni Lowassa alifanya mkutano wa kampeni zake huko Babati, mkoani Manyara na kueleza kuwa Serikali yake itakuwa rafiki kwa mama ntilie, bodaboda na watu wote ambao wanahangaika kutafuta maendeleo.
“Katika serikali yangu mtu atakayesumbua hawa watu, mtu anaingiza daladala yake barabarani anakamatwa huyo atakayemkamata nitamfunga, najua watasema mimi ni dikteta, lakini ni dikteta wa maendeleo,” alisema Lowassa.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, ambaye amekuwa bega kwa bega na Lowassa katika shughuli za kampeni, alisema anawashangaa baadhi ya viongozi wa CCM wanaodai kuwa amekuwa akiilalamikia serikali wakati aliwahi kuwa huko.

Alisema alipotoka madarakani mwaka 2005 bei ya sukari ilikuwa Sh 500, lakini hivi sasa haikamatiki.
“Nilipoondoka niliacha unga wa sembe ukiwa Sh 200, lakini leo haukamatiki, mchele Sh 600 lakini leo haukamatiki, kipande cha sabuni Sh 50 lakini leo hakikamatiki. Nimeondoka huko kwa kuwa serikali imeshindwa kujibu hayo mambo,” alisema Sumaye.

Akimzungumzia Namelok, Sumaye alimtaja mwanasiasa huyo kijana kuwa ni mdogo, ndugu yake na kwamba hana ugomvi naye, lakini kwa sababu anagombea ubunge kupitia gari ambalo halina matairi afahamu kuwa yupo kwenye genge ambalo halifai.

“Tutaongea naye aachane na hiyo kambi ya kijani aje, msije mkampigia kura kwa sababu hatashinda, aje aungane na Lowassa. Lowassa atashinda kwa zaidi ya asilimia 80, Magufuli mwenyewe amekata tamaa na CCM ndiyo maana anasema ni kitanda chenye kunguni, CCM ni chama kilichojaa rushwa, ufedhuli, Namelok kwa kuwa bado ni binti msikivu tutaongea naye,” alisema Sumaye.

Mkutano wa kwanza wa Lowassa akiwa mpinzani
Lowassa, ambaye amekuwa Mbunge wa Monduli kwa miaka 20, jana alifanya mkutano wa kwanza katika Jimbo la Monduli akiwa chama cha upinzani.
Licha ya mkutano wake wa jana kupangwa kufanyika saa 5:00 asubuhi, tangu saa 1:30 asubuhi wananchi walianza kujitokeza uwanjani, huku Lowassa mwenyewe akifika eneo la mkutano saa 7:58 mchana.

Akizungumza juu ya uongozi wake jimboni hapo na hatima yake, alisema: “Nimesema napita Mto wa Mbu niwapungie mkono kwa sababu nitakuja kuaga rasmi, watu uliokaa nao miaka 20  huwaagi hivi hivi. Nilishawahi kusema watu tulihozunika pamoja tutafurahi pamoja.

“Nataka kila mwana Monduli anitafutie kura popote Tanzania, ni muhimu kupata kura nyingi mno. Hawa jamaa ni mahodari wa kuiba kura kwa hiyo lazima tupate kura nyingi,” alisema Lowassa.

Alisema kwa sasa hatakuwa tena mbunge wa jimbo hilo, ila atakuwa mbunge wa zamani wa Monduli, hivyo anataka kuendelea kushirikiana nao katika kutatua matatizo ya jimbo hilo.
“Nataka Monduli iendelee kubaki na amani ile ile, tusaidiane, tuzikane, hata asiyekuwa kwenye chama chetu tumuelimishe siyo kutengana, tuache ugomvi kati ya wakulima na wafugaji,” alisema.

MTANZANIA

No comments:

Post a Comment