Pages

Tuesday, December 8, 2015

NAMNA RAHISI YA KUANDAA SHEREHE NYUMBANI MSIMU HUU WA SIKUKUU


Kama tujuavyo sikukuu za mwisho wa mwaka zimekaribia. Na sikukuu maana yake ni sherehe na shamrashamra kwa wingi. Hivyo basi kwa lengo la makala hii nimefanya mahojiano na Asna Mshana ambaye ni mtaalam wa kuandaa sherehe na anaelezea ni kwa njia gani rahisi kabisa unaweza kuandaa sherehe yako nyumbani msimu huu wa sikukuu. Twende pamoja tuelimike na dondoo hizi za kuandaa sherehe ndogo ya sikukuu nyumbani bila kutoa jasho.

·Kwanza kabisa unapaswa kujiuliza ni
muda gani sherehe itafanyika?
Unapaswa kuamua unataka kufanya sherehe ya chakula cha mchana au usiku. Sababu ya kufahamu hili ni mahitaji yanayotakiwa kwa mfano baadhi ya maeneo, saba mchana jua ni kali sana kiasi kwamba wageni wako watahitaji kivuli wakati kwa chakula cha usiku kivuli hakihitajiki. Vilevile swala la mwanga linazingatiwa kuendana na muda wa sherehe.

·Andaa orodha ya wageni na mialiko
Mara baada ya kuamua ni sherehe ya muda gani unayoandaa (kwa maana ya chakula cha mchana au usiku), jihakikishie tarehe, muda, orodha ya wageni na menu. Ukishaweka pamoja orodha ya watu unaowaalika ndipo unaamua ni kwa jinsi gani unawafahamisha. Kusema ukweli kwa sherehe hii ndogo tu ya nyumbani huna haja ya kuingia gharama za kutuma kadi za mialiko kwa kipindi hiki cha mitandao lukuki ya mawasiliano. Unaweza kutuma mialiko kwa ujumbe wa simu, barua pepe au hata kwa kuwapigia waalikwa simu. Tuma mialiko angalau wiki mbili kabla ya sherehe kwakuwa sherehe kipindi hiki ni nyingi na pia watu wanasafiri kwenda maeneo mbalimbali.

·Chagua menu rahisi
Watu wanaosambaza  vyakula kwenye sherehe wana menu nyingi. Chagua ambayo ni rahisi kwani sikukuu vyakula ni vingi kwenye nyumba nyingi. Bila shaka wageni wako walishakula mno huko walikotoka. Chagua chakula kimoja kimoja ili kupata menu kamili kwa ajili ya sherehe yako. Pia sherehe za buffet huwa ni rahisi zaidi: Hii ina maana watu wa vyakula wanaweka vyakula tayari na wageni wanajichotea wenyewe. Na hii inasaidia sana kwa maandalizi ya sherehe kuliko kupika mwenyewe nyumbani.
Kama kwenye menu yako utachagua viburudisho kama icecream itapendeza zaidi.

·Bandika vyakula majina
Kwa urahisi kwa wageni kujihudumia vyakula vibandikwe majina, ili ijulikane kabisa hiki ni chakula fulani.

·Tengeneza eneo la vinywaji
Weka vinywaji, glasi sahihi na barafu mahali hapo kwa ajili ya wageni wote wakiwa ni wale wanaopenda kujihudumia wenyewe na baadhi wanaopenda kuhudumiwa. Endapo utakuwa unafahamu idadi kubwa ya wageni wako wanatumia vinywaji gani (kutokana na ukaribu wako kwao na sio kuwauliza kabla ya siku ya sherehe) itakusaidia sana kufanya maandalizi kwa upande wa vinywaji.

·Vinywaji vya ziada
Weka vinywaji vya ziada ndani (mbali na eneo la sherehe) ikiwa ni pamoja na napkini, barafu na glasi sahihi. Hili ni jambo muhimu sana kuepuka aibu ya kuagiza vinywaji vya nyongeza dukani mbele za wageni.

·Amua kuhusu mapambo
Kwa swala la mapambo usifikirie mambo makubwa. Acha nafasi mezani kwa ajili ya vyakula na vinywaji kwa kuweka ua dogo tu katikati ya meza na mshuma endapo ni chakula cha usiku.

·Tengeneza orodha na ratiba ya matukio
Angalau siku moja au mbili kabla ya sharehe tengeneza orodha na ratiba ya nini kinatakiwa kifanyike na kwa muda gani na mhusika ni nani. Hakikisha saa nzima kabla sherehe haijaanza kila kitu kipo tayari ili kukupa muda wewe muandaaji kutulia na kufurahia mapokezi ya wageni wako.

·Andaa kila kitu kiwe tayari kabla wageni hawajawasili
Vyakula na vinywaji vyote viwe mahali pake kabla wageni hawajafika. Tumia msambaza chakula mwenye vifaa vya moto kwa ajili ya kuweka vyakula katika hali ya moto muda wote. Ingawaje kuna baadhi ya vitu huwezi kuviweka kabla ya ugeni (kwa mfano vipande vya barafu), ila jitahidi kazi kubwa ya maandalizi iwe imekwishafanyika kabla ya kuingia wageni. Kama utakuwa kwenye mpangilio na kila kitu kuwa tayari utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuhudumia wageni wako.

·Sheherekea kwa furaha!
Mwisho lakini si dogo ni kufurahia sherehe yako! Kama utakuwa na wakati mzuri wageni wako watakuwa na furaha pia.


Je, unauza bidhaa au huduma inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue? Nijulishe simu/whatsapp 0755200023.

No comments:

Post a Comment