Pages

Monday, February 15, 2016

KUTOKA KWANGU:...Unavyoweza kuboresha fenicha za nje ya nyumba kwa kuongeza mito ya gharama nafuu

Huenda unapamba upya eneo la nje ya nyumba yako kwa kuboresha vilivyopo, bila shaka unataka kupata muonekano mpya ambao utaupenda bila kutumia gharama kubwa. Kwa kuwa na mito ya gharama nafuu unaweza kutengeneza muonekano wa kuvutia unaoutaka.

Nakupa dondoo hatua kwa hatua za njia rahisi za kukuwezesha kupata mito ya namna hiyo ili kuondoa ile ambayo imesinyaa au foronya zimepauka, zimechakaa au
chochote kile kinachochangia usiipende tena mito yako hiyo!
Kabla hujanunua au kutoa oda ya kutengenezewa mito yako, au hata kutengeneza mwenyewe, unatakiwa kujua muonekano wa mwisho unaoutaka. Angalia ile ambayo ulikuwa nayo tayari na uone  kama unahitaji kuiboresha ama kununua mingine. Kuboresha mito kuko kwa aina mbili.

Aina ya kwanza ni kuboresha kwa kuongeza sufi ile mito iliyosinyaa na aina ya pili ni kuboresha kwa kubadili foronya zilizochakaa.
Kuongeza sufi isikuogopeshe. Unaweza kununua mito mikubwa ya mitumba (ambayo ni bei rahisi zaidi ya mipya) na ukatoa ile sufi yake ukajazia kwenye mito yako unayotaka kuboresha kutoka kwenye kusinyaa. 

Au unaweza kuweka sufi kidogo iliyopo kwenye mito ya zamani eneo la katikati tu na kwa nje ukazungushia godoro jembamba. Mbinu ni nyingi, angalia mito yako halafu fanya maamuzi sahihi.

Mito ya bei rahisi ipo katika mifumo mingi. Unaweza kununua godoro halafu ukalikatakata vipande kwa ukubwa wa mito unayotaka, ukashonea foronya na ukapata mito ya kukalia juu ya viti vya chuma bila kuhitaji sufi yoyote.

Unaweza kuchanganya mito midogo na mikubwa na pia unaweza kuwa na ya maumbo mbalimbali na ikakuwakilisha kwamba unapendelea nini.

Vitambaa vya kushonea foronya za mito ya fenicha za nje vipo vya aina nyingi kama ilivyo kwa sofa. Rangi na michoro ya kuendana na mazingira ya nje zinapendeza zaidi. Rangi hizo ni zile za udongo na mimea na maua yaliyopo kwenye eneo lako.  Unaweza ukaamua kutumia malighafi za kitambaa au mpira kutengenezea foronya hizo. 

Uzuri wa mpira ni kwamba ni rahisi kwa utunzaji iwe ni kufuta vumbi au maji kulingana na mahali fenicha hizo zilipo.
Tengeneza mito ambayo utakuwa na stori ya kuielezea. Inawezekana umeitengeneza kipindi ambacho kilikuwa na umuhimu fulani kwako.  

Nyakati hizi za digitali kila kitu kinawezekana, unaweza kuweka picha au maandishi ya mahaba au imani kuelezea kumbukumbu na hisia zako kupitia mito hiyo ya viti vya nje ya nyumba yako.


Ikiwa una eneo lolote linakutatiza kuhusu mapambo ya nyumbani kwako, wasiliana na mimi 0755 200023

Nifuate Instagram: vivimachangehomes

No comments:

Post a Comment