Pages

Tuesday, July 26, 2016

Namna ya kuchagua rangi ya kaunta ya jiko

Kaunta ya jiko lako inatakiwa kuwa eneo muhimu sana la kuzingatia katika harakati za kuwa na jiko linalopendeza, sio tu kwa ajili ya muonekano wake bali pia kwa ajili ya gharama za kununua na pia kuisimika. Kama tujuavyo wenye kujenga nyumba za kisasa wengi wanapendelea kuweka kaunta ya marble ambapo gharama yake si ndogo. Unapokuwa umechagua kuweka malighafi hii ambayo ni jiwe la asili basi kinachofuata ni
kuangalia uweke la rangi gani.

Marble zinakuja kwa michoro na rangi nyingi mno kwahivyo kuchagua iliyo sahihi inaweza kuwa  changamoto kubwa. Rangi utakayochagua itakupa mwelekeo wa rangi za vifaa vingine utakavyonunua kwa ajili ya jikoni huku ukijua kuwa ni rahisi kuvibadilisha kuliko kubadilisha rangi ya marble kwani ni gharama kuondoa kaunta moja na kusimika ya rangi nyingine. Ni kazi ndogo tu kupaka makabati rangi nyingine au kubadili mikono ya makabati au hata kubadilisha microwave nyeupe na kuweka ya silva au nyeusi.

Unapochagua rangi ya marble kwa ajili ya kaunta ya jiko, anza kwa kuchagua rangi ya jiwe ambalo unaipenda. Chagua marble ambayo unaona kuwa ina mvuto, bila kujali kama inaendana na rangi ya makabati au ukuta. Mwishoni utaridhika zaidi kwa kuchagua kitu ambacho unakipenda badala ya kuchagua rangi au mtindo ambao unadhani utaoana na vitu vingine.

Wakati wa kuchagua rangi ya kaunta, kumbuka kuwa rangi nzito kama vile nyekundu au nyeusi zina muonekano wa ukisasa lakini zinaweza kufanya chumba kipooze. Marble za rangi hizi hazina michoro inayoonekana kwahivyo ni kawaida kupitwa na wakati mapema zaidi kwani inakuwa haina ushirikiano na rangi nyingine jikoni. Ni bora ukapeleka rangi hizi kwenye vifaa vya kuhamishika. Kaunta yenye michoro inayoonekana wazi ni rahisi kuoanisha na rangi nyingine bila kusababisha jiko kuonekana kama limezidiwa rangi.

Unapochagua rangi ya marble ya kutengenezea kaunta ya jiko zaidi ya kuzingatia rangi ya kuta na sakafu pia ni vyema kufahamu kiasi cha mwanga kinachoingia jikoni kutokana na upande dirisha lililoko.

Ukiwa unachagua rangi ya kaunta yako angalia ambayo itafanya vyema ukutani pia. Kanuni namba moja ya rangi ni kwamba weka pamoja rangi zilizo kwenye familia moja kwani zinasababisha ujirani ambao unaleta muonekano wa kuvutia. Kwasababu marble ni jiwe la asili ni kawaida kuwa na rangi kadhaa ndani yake. Ni vyema kuzishirikisha rangi hizo kwenye maneneo mengine ya jiko iwe ni ukutani au sakafuni.

Vilevile ni vyema kufahamu kuwa rangi inavyozidi kuwa nzito/nyeusi, ndivyo na chumba kinavyozidi kuwa kidogo na inavyozidi kuwa nyepesi/mwanga ndivyo chumba kinavyozidi kuonekana kikubwa.

Unapochagua rangi ya kaunta uwe umeshakusanya mawazo ya rangi za maeneo mengine pia, kama vile makabati, sakafu, kuta, dari na mwanga wa taa.


Ushauri 0755 200023

No comments:

Post a Comment