Pages

Friday, July 22, 2016

Namna ya kutunza matandiko mbalimbali yanayokamilisha kitanda

Kitanda kilichokamilika kwa ajili ya kupanda na kulala kina muunganiko wa matandiko mengi. Nimehojiana na Mary Masho, mwanadada mwenye fani ya utunzaji wa nyumba na hapa anaainisha aina ya matandiko  yanayokamilisha kitanda na namna ya kuyatunza. Twende pamoja tuelimike kama ifuatavyo.

1.  Mito
Mafuta na uchafu kutoka kwenye nywele na nyuso zetu zinazama
hadi kwenye sponji zilizo ndani ya mto uliolalia. Kama hutumii kofia au kitambaa kichwani cha kuzuia uchafu huu usizame kwenye mto basi unatakiwa uwe unaufua japo mara moja kila mwezi au kila baada ya miezi miwili. Kama unakinga mafuta ya nywele yasiingie kwenye mto wako basi unahitaji kuufua angalau mara mbili kwa mwaka. Foronya zinatakiwa kufuliwa japo mara moja kila baada ya majuma mawili. Mito inafaa zaidi kufuliwa kwenye mashine za kufulia, na sio lazima uwe nayo nyumbani unaweza kupeleka kwenye vituo vya kufulia.

2.  Shuka
Kipindi unachotakiwa kufua shuka baada ya kuzilalia mara nyingi kinategemeana na uamuzi binafsi. Wapo wanaopenda kufua shuka zao japo mara moja kila juma. Wanapenda ule muonekano wa shuka safi na huwa wanaweka kitanda kwenye muonekano huo kila juma. Shuka zinapokea mafuta na uchafu kutoka kwenye miili yetu ambapo inaweza kupelekea madoa makubwa. Hakikisha unakagua na kushughulikia madoa yoyote kwenye shuka zako kila unapozifua. Pia epuka kufua shuka kwenye maji ya moto kwani zinaweza kusinyaa. Unaweza usigundue kusinyaa huko hadi pale unapotaka kuzitandika tena. Maji ya uvuguvugu ndio yanafaa.

3.  Blanketi
Kujua ni kila baada ya muda gani ufue blanketi lako, unatakiwa ujue matumizi yake yakoje. Kama una blanketi la kupambia kitanda tu na wala halikunjuliwi na kutumika, basi kulifua kila baada ya miezi kadhaa itakuwa sahihi. Ila kama blanketi linatumika kila unapolala inaweza ikakubidi kuliweka kwenye ratiba ya kulifua kila baada ya majuma matatu hadi mwezi. Kuwa makini kufuata maelekezo ya utunzaji kwenye lebo kama yapo. Mara nyingi blanketi linatoa vimanyoya au pia kuchuja. Hakikisha unalifua bila kuchanganya na nguo nyingine.

4.  Komfota na duveti
Wengi wanatumia komfota na duveti kama tandikio la juu la kupendezesha kitanda. Kwahivyo haya si hasa kwa ajili ya kujifunikia. Kama ndivyo kwa upande wako na kama halijamwagikiwa chochote huna haja ya kulifua zaidi ya mara moja au mbili kwa mwaka. Mengi ya makomfota na maduveti yanatakikana kufuliwa kwenye mashine kwani kwanza ni makubwa kufikicha kwa mikono na pia si rahisi kuyakamua badala yake yatachukua muda sana kukauka na pengine kupelekea kuvunda ama kukata kamba za kuanikia kwa uzito wa maji yake.

5.  Foronya za godoro
Kuvalisha godoro foronya ni njia nzuri sana ya kuongeza uhai wa godoro lako. Foronya ya godoro inasaidia kuzuia uharibifu wa godoro, mzio na pia kuweka godoro safi na nadhifu. Foronya za godoro zinapaswa kuvuliwa na kufuliwa angalau mara moja kila mwezi. Endapo doa lolote limetokea unapaswa kulishughulikia papo hapo bila kujali ratiba ya ufuaji.

6.  Urembo wa fremu ya kitanda
Urembo wa fremu ya kitanda ambao pia unajulikana kama sketi ya kitanda mara nyingi huwa ni kwa ajili ya kukipendezesha na sio kwa kutumika. Huwa hauchafuki ila kama una mzio (allergy) unaweza kuhitajika kuufua japo mara 2-3 kwa mwezi. Kumbuka kuzingatia aina ya kitambaa kilichotengenezea urembo huo ili ufue kwa uangalifu. Sketi za kitanda  nyingi zinatengenezwa kwa vitambaa vyepesi.


Kwa ushauri 0755 200023

No comments:

Post a Comment