Pages

Saturday, September 10, 2016

Makundi matatu ya taa za ndani ya nyumba ya kisasa

Tunapotaka kupendezesha nyumba zetu, tunajikuta tuna vingi vya kuzingatia. Tunakuwa makini kwenye kuchagua rangi na michoro iliyopo kwenye kuta, fenicha na sakafuni. Lakini ni mara chache tunapeleka umakini huohuo kwenye taa na jinsi mwanga wa taa unavyoweza kubadili muonekano wa namna chumba kinavyoonekana. Kutokana na hilo ni
vyema kufahamu kuwa suala la taa za ndai ya nyumba si jepesi kivile.

Unatakiwa kujiuliza maswali kadhaa kama vile ni taa zipi unazohitaji kwenye chumba kipi kwani kila chumba kina mahitaji yake. Na je ni za wati ngapi, ni za kuning’inia, ni za ukutani au ni za kupachikwa kuzamishwa kwenye dari? Taa mbili za mezani au moja ya sakafuni? Maswali ni mengi ila usiwe na shaka kwani kwenye makala hii tunaangalia makundi matatu ya taa kwa matumizi tofauti ambayo ni kundi la taa za lazima, taa za kuelekeza na taa za kupendezesha.

Tukianza na taa za lazima ni zile taa ambazo ni za msingi kwamba utakapoingia kwenye chumba cha giza lazima uiwashe hiyo kwanza. Kiasi cha mwanga kinachozalishwa na taa hizi lazima kiwe cha kutosha kwa ajili ya kuweza kumulika kila sehemu vizuri chumbani. Kwa mfano taa mbili za mezani haziangukii kwenye kundi hili lakini taa inayoning’inia darini imo kwenye taa za lazima katika chumba hichohicho. Hapo unaweza kuona tofauti kati ya kazi za taa hizi za aina mbili.

Fungu la pili la taa ni zile taa za kuelekeza kwenye maeneo maalum kusaidia kuongeza mwanga wakati wa shughuli kama vile ya kusoma, kufanya kazi kwenye kompyuta au wakati wa kula. Lengo la taa hizi ni kupeleka mwanga wa moja kwa moja pale unapohitajika badala ya kuusambaza kila mahali. Taa za namna hii ni kama zile za vivuli za kuweka kwenye vimeza vya kando au kusimamisha sakafuni.

Kundi la tatu la taa ni zile zilizowekwa kwa lengo la kupamba/urembo. Kwa mfano taa za rangi kwenye kabati ulilosambaza sanaa za mapambo. Au pia zile za kwenye kabati la vyombo la kioo zenye lengo la kuweka msisitizo kwenye vyombo vyako zako za kifahari.

Katika makundi haya matatu ya taa, ili kupata lengo ulilokusudia unapaswa kuchagua balbu sahihi kwa kukupa kiasi na aina ya mwanga unaotaka. Fundi umeme John Mangowi anajutuza kuwa kwa kundi la kwanza la taa ambazo ni za lazima, endapo ni chumba cha kawaida cha nyumbani unahitaji baibu ya wati 40 hadi 60.

Kwa taa za kuelekeza na za urembo ni muhimu kutokuwa na mwanga mkali sana. Ambapo unahitaji za bailbu za wati kati ya 10 na 25.


Mwisho ni vyema kufahamu kuwa mwanga wa taa na kupendezesha ndani ya nyumba kwa taa, jambo kubwa la kuzingatia ni muundo, ukubwa na kiasi cha mwanga wa taa husika. Inawezekana umeipenda sana taa ya kuning’inia darini ya umbo fulani, lakini kama nyumba haina dari ndefu taa ya hivyo haikufai.

No comments:

Post a Comment