Pages

Monday, September 5, 2016

Rangi zinazopendeza jikoni

Kuanzia kwenye kuchagua rangi ya makabati, kuta, sakafu na dari jiko ni chumba chenye maeneo mengi ya kutumia ubunifu wako wa kuchagua rangi. Ila tatizo wengi wanajiuliza ni kwa namna gani wanaweza kuchagua rangi ambazo zitafanya chumba hiki kionyeshe mshikamano wa rangi hizo. Kutokana na uwepo wa
rangi lukuki sokoni, hakika hii inaweza kuwa ni changamoto kwa wengi.

Uzuri ni kwamba hata kama utaamua kwenda na makabati meupe bado hukosi fursa ya kutambulisha rangi katika maeneo mengine ya jiko.
Wengi wanaanzia siku zao jikoni, kwahivyo nyeupe ina uwezo mkubwa wa kukipa chumba hisia ya nguvu ya kuanzia siku. Pia ina hisia ya kitu freshi na safi. Jiko lenye rangi nyeupe kote lina mvuto wa aina yake.

Chagua muonekano wa makabati kwanza. Watu wengi wanapendelea makabati ya mbao ngumu kwani ndio imara yanayoweza kukabiliana na majimaji ya jikoni. Hivyo basi kutokana na makabati kuwa ya mbao vilevile wengi wanapendelea kuyapaka finishing ambazo zitayaacha na rangi zake za asili.

Baada ya kuamua rangi ya makabati kinachofuata ni kuchagua rangi za kaunta, kuta, dari na sakafu. Kwavile jikoni kipaumbele ni kuwa na mwanga wa kutosha ni vyema ukatumia rangi nyepesi. Uzuri ni kwamba kila chumba ndani ya nyumba kina rangi inayokifanya kipendeze kuliko nyingine.

Rangi kama nyekundu inaaaminiwa kuleta hamu ya kula na inafanya vizuri kwa chumba cha jiko. Kuna jamii nyingi za nyekundu na huwa inachomoza vyema kwenye makabati  na baadhi ya sehemu za ukuta.

Kijivu ni rangi isiyoegemea upande wowote ambayo imeonekana kushika kasi siku za karibuni kwenye nyumba nyingi. Jamii nzuri ya kijivu inaweza kufanya maajabu jikoni huku ikioanishwa vizuri na ile ya kaunta na makabati.

Bluu ni rangi nyingine pia ambayo inapendeza jikoni. Bluu nyepesi inapotumika, inaleta muonekano nadhifu wa usafi na inashauriwa kwenye kuta, makabati na hata dari. Siku zote tumia bluu nyepesi jikoni kwani kwa kawaida ile nzito inaweza kukizidi nguvu chumba. Bluu inaendana na nyeupe (kumbuka mawingu), kijivu na nyingine ambazo haziegemei upande wowote.

Kama miale ya jua ilivyo, njano inaweza kuongeza mwanga chumbani kwa haraka mno. Ingawa inaaminiwa kufanya watu wasikie njaa, lakini pia ina hisia ya  utulivu kwahivyo kuwafanya watu wawe na furaha wawapo jikoni. Njano ni chaguo zuri kwa jiko dogo kwani inalifanya lionekane kubwa na inaendana vyema na nyeupe.

Kijani pia ni chaguo smati kwa kutumika jikoni. Kuna jamii nyingi za kuchagua kutoka rangi ya kijani ila kile cha rangi ya tunda la epo kinaendana vizuri na nyeupe na rangi asili ya mbao. Kijani inaongeza nguvu jikoni ikitumiwa popote iwe ni sakafuni au lile eneo la kisiwa cha jiko.

No comments:

Post a Comment