Pages

Saturday, February 28, 2015

DC Makonda kutinga kortini kwa kosa la kutukana na kudhalilisha wenzake

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Viongozi wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanakusudia kumfikisha mahakamani Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, Jumatatu ijayo kwa madai ya kuwakashifu, kuwadhalilisha na kuwatukana.
Viongozi hao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Mgana Msindai.
 
Akisoma kusudio hilo jana mbele ya waandishi wa habari kwa niaba ya mwenzake, Guninita alisema.
 
Makonda hakustahili kuteuliwa kushika wadhifa huo kwa kuwa hana maadili ya kuwa kiongozi.
 
Alisema cheo alichonacho ni cha uyoga ndio maana amekuwa akitukana watu bila sababu za msingi.
 
“Sifa ya mtu kuchaguliwa ni lazima awe mnyenyekevu, awe na adabu ya kuzaliwa na siyo ya photocopy na awe anaheshimu watu hivyo wenye vyeo vya uyoga hawana sifa hizo,” alisema Guninita.
 
Alisema alipofikia Makonda, wameshindwa kumvumilia hali ambayo wametaka haki zao kuzipata kupitia mahakama kwa kuwa chama kinaendelea kumlinda.
 
Alisema hawana ugomvi na Makonda lakini wanamshangaa amekuwa akiwatukana kila wakati kwa kuwaita ni vibaraka wa CCM na kuwataka waondoke kwenye chama.
 
Alisema alishaandikiwa barua na mwanasheria wake, Benjamini Mwakagamba, ya kumtaka aombe radhi dhidi ya kauli zake na matokeo yake amegoma na kueleza kuwa alitumwa na chama.
 
“Waliomshauri rais kumchagua awe mkuu wa wilaya hawakuwa sahihi na kama ningekuwa nina uwezo ningetengua hivi ni mtu gani unawatukana viongozi wa dini halafu leo hii unafanyaje nao kazi,” alihoji. 
 
Guninita alisema alitegemea kama kuna kosa amelifanya angeitwa na badala ya kutukanwa na kukashfiwa na kijana huyo ambaye alidai amempita umri na vyeo.
 
Alisema Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) unatumika kuwatukana viongozi wakati dhana yake ni kuandaliwa kuwa viongozi wenye maadili.
 
“Huyu kijana hana maadili ukiachilia mbali kutukashifu alishawahi kumshambuliwa Jaji Warioba...Alishawahi kumpiga Jaji Warioba eti alijitetea alikuwa anamlinda. Je huyu Makonda ana mkataba wa kumlinda jaji Warioba,” alihoji
 
Guninita alisema Makonda aliwahi pia kuwatukana viongozi wa dini lakini waliamua kukaa kimya huku wakimuombea aendelee kuwa na uhai ili wapambane na Makonda mahakamani.
 
Alisema Makonda amekuwa akibebwa na kulindwa na viongozi wa CCM  wakimtetea, lakini mahakama ni chombo ambacho kitamtenda haki.
 
Alisema chama kimefikia sehemu mbaya kuwapo na matabaka ya watu kupewa vyeo kama uyoga ndiyo maana wanakuwa na jeuri kwa watu. Alisema tabaka hilo ndilo linalosababisha kuwapo na mgogoro ndani ya chama.
 
Alisema Jumatatu wataenda mahakamani kuandaa hati ya mashtaka na hivi sasa wanaandaa mchanganuo wa fidia atakayotaka kulipwa.
 
Alisema Mwenyekiti wa Chama ambaye ni Rais Jakaya Kikwete anaheshima kubwa ya kushughulikia migogoro mbalimbali ya nje ya nchi, hivyo wakati umefika wa kushughulikia migogoro iliyopo ndani ya chama.
 
Pia alisema kitendo cha Makonda kuwataka wajiondoe kwenye chama alieleza kuwa hawatatoka kwa kuwa wamewekeza kwa zaidi ya miaka 40 ndani ya CCM.
 
Alisema kama anataka watoke ndani ya chama awalipe fidia la sivyo wao wanauwezo wa kumlipa fidia kwa miaka mitatu ambayo amekitumikia chama.
 
Mwanasheria anayewawakilisha viongozi hao Benjamini Mwakagamba, alisema wateja wake  watafungua kesi Jumatatu dhidi ya Makonda ya udhalilishaji.
 
Alisema awali alishaandikiwa barua na kutakiwa kuomba radhi, kuacha kuwazungumzia viongozi hao pamoja na kulipa fidia ya Sh milioni 100.
 

Alisema barua hiyo aliijibu na kueleza kuwa alifanya hivyo kwa maelekezo ya chama.
Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment