Pages

Thursday, February 5, 2015

Jinsi ya kusafisha maeneo mbalimbali ya nyumba



Mtu alisoma kichwa cha makala atadhani tu kuwa kusafisha nyumba mbona ni jambo linaloeleweka, lakini ukikaa chini ukafikiria unaweza kujiuliza ni wapi pa kuanzia? Na ni namna gani unasafisha eneo fulani la nyumba kwa mfano bafuni.

Vizuri, kwa vile nyumba ina maeneo mengi makala hii itakujuza jinsi ya kusafisha maeneo mbalimbali na kwa haraka na ukishaanza husimami hadi nyumba yote ing’ae.

Kwanza kabisa amua ni kwa namna gani unataka nyumba yako iwe safi, una muda kiasi gani na ni kwa namna gani una mori wa kusafisha siku hiyo.
Kama itawezekana safisha kuanzia juu kushuka chini. Kwa mtu mwenye shughuli za “wastani” (asiyekuwa bize sana) inapendeza kufanya usafi wa nyumba kidogo kidogo kila siku, ili kazi isijilimbikize na kuwa na siku ya kufanya usafi mkubwa mara chache kwa mwezi. Katika makala hii nizungumzia huu usafi wa kidogokidogo wa kila siku.

Kuamua ni chumba gani uanze kusafisha na ni kipi umalizie inapendeza kama utaanzia vyumba vya ndani ukielekea nje. Hii itakusaidia kutorudia kazi ile ile mara mbilimbili, kwa mfano unadeki sehemu halafu unapitia hapohapo tena kudeki ya mbele yake hasa pale inapokuwa ni mtu zaidi ya mmoja anasafisha. Andaa mpango wako wa kusafisha kwa kutizama ni sakafu ipi unadeki, unafagia ama unasafisha kwa mashine ya upepo.

Gawaneni maeneo ya kusafisha kama unaishi nyumba moja na watu wengine, na kazi husika iendane na umri, kwa mfano teenager anaweza kusafisha bafuni kwake na kadhalika.
Usafi wa bafuni pengine ni mgumu kuliko sehemu zote za nyumba, maeneo ya kusafisha kwenye eneo hili ni kwenye sinki la mswaki, bakuli la choo, bomba la mvua au sinki la kuogea, vioo na sakafu. Unapomaliza kusafisha maeneo yote haya ya bafu kwa sabuni na dawa zinazopaswa mwisho ni kukausha kila mahali bafu libaki kavu.

Ukiingia kusafisha jikoni anza na kuosha vyombo ikifuatiwa na kuvifuta na kuvirudisha kila kimoja mahali pake. Safisha microwave. Kazi nyingine ambayo wengi hawaipendi ni kusafisha microwave na oven, hasa pale unapokuta havisafishwi kila siku (kwani saa nyingine tunasahau).
Panga kwenye makabati ya vyombo, safisha kaunta na sinki la vyombo, toa taka nje na mwishoni deki sakafu ya jiko.

Kusafisha chumba cha kulala kwanza kabisa ondoa mrundikano wowote uliopo kwa wakati huo, kwa mfano nguo chafu zilizo sakafuni kwa kuziweka kwenye mfuko wa nguo za kufua. Tandika kitanda, kuna ambao wanadhani kutandika kitanda haina maana kwani wanaenda kulala tena na kitavurugika. Lakini pale unapokitandika utaona ni kwa jinsi gani chumba kinaonekana vizuri. Hata hivyo unaweza kuondoa shuka, foronya na blanketi chafu na kutandika safi. Panga kwenye kabati lako la nguo, zile unazovaa mara kwa mara ziweke karibu na kama ni kwenye droo ziweke juu. Futa vumbi. Safisha kwa mashine ya upepo kama sakafu ni ya zulia ama deki kama sakafu ni ya kusafisha kwa maji. Mwishoni puliza airfreshner kwa ajili ya harufu nzuri.

Sehemu itakayokuwa imebaki ni maeneo ya wazi kama vile chumba cha chakula, sebule na ujia. Panga mito ya sofa vizuri, futa vumbi kwenye fenicha na kama zipo za mbao unaweza kuzifuta kwa polishi yake. Malizia usafi wa ndani kwa kusafisha sakafu ya maeneo mengine wa wazi kwa kutegemea na aiana ya sakafu iliyopo.

Ili usafi wa nyumba yako ukamilike usisahau kusafisha nje ya nyumba. Eneo la kufagia lifagiliwe na kwenye majani kuokotwe.
Kama kuna nguo za kufua zoezi hili lifanyike.

Tembea maeneo yote ya nyumba na kujiridhisha kuwa kila mahali ni pasafi na hakikisha kila kifaa cha usafi kimesafishwa na kurudishwa mahali pake. Umemaliza na hongera kwa kumaliza usafi wa makazi yako na hivyo kuishi mahali pasafi!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 na pia tembelea www.vivimachange.blogspot.com 

No comments:

Post a Comment