Pages

Friday, April 10, 2015

Gwajima Ahojiwa na Polisi..... Aulizwa Mambo Mengi Nje ya Madai ya Awali ya Matumizi ya Lugha Chafu.....Wafuasi wake Wamsubiri na Kumpokea Mithili ya Mfalme

MAHOJIANO baina ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Jeshi la Polisi yaliyokwama wiki iliyopita kutokana na kuzorota kwa afya ya askofu huyo, yaliendelea jana saa sita huku akitakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu kumi siku ya mahojiano mengine yatakayofanyika wiki ijayo.

Hali hiyo imeonekana kumchanganya wakili wa kiongozi huyo wa kiroho,
kiasi cha kusema hakutegemea kama ingefikia hatua hiyo, kwani alitarajia mteja wake angehojiwa juu ya matumizi ya lugha ya matusi dhidi ya kiongozi mwingine wa dini nchini.

Akizungumza mara baada ya mahojiano hayo katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam, Gwajima aliyeonekana kuwa na afya njema tofauti na wiki iliyopita alipowasili Polisi na kushindwa kupanda ngazi kiasi cha kusababisha kuahirishwa kwa mahojiano, alisema mahojiano ya jana yalifanyika vizuri na yanatarajiwa kuendelea Aprili 16 mwezi huu na kutakiwa kupeleka nyaraka muhimu kwa mahojiano zaidi.

Akielezea jinsi mahojiano yalivyokuwa, Wakili anayesimamia kesi hiyo, John Mallya alisema
mahojiano yamekwenda vizuri, lakini amesikitishwa na mambo ambayo mteja wake ameulizwa kwani walidhani wataulizwa kuhusiana na matumizi ya lugha chafu ambayo polisi walidai mchungaji aliitumia kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini.

“Mahojiano yamekwenda vizuri lakini nasikitika sana kutokana na mambo waliyokuwa wanamhoji. Wamemuuliza mambo ambayo hayahusiani kabisa na kile tulichotarajia na ndicho kilichotuleta hapa, nilidhani mteja wangu ataulizwa kuhusiana na matumizi ya lugha chafu iliyodaiwa kutumika kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini,” alihoji wakili wa Gwajima.

Aliendelea kusema kuwa, mambo aliyoulizwa ni kuhusiana na ukoo wake, wazazi wake hata ndugu zake na watu wengine wa kwao waliokufa.

Alisema walihoji pia juu ya mambo mengine kama umiliki wa helikopta, utajiri wake, nyumba anayoishi, uhusiano wake na watu mbalimbali.
“Nimeshangaa sana kuona mteja wangu ameulizwa vitu kama hivyo ambavyo havihusiani na madai ya hapo awali ya matumizi ya lugha ya matusi.

Tumeagizwa tulete nyaraka kumi siku ya mahojiano yetu tena yatakayofanyika tarehe 16 mwezi huu na sisi tutafanya hivyo,” alisema Mallya.

Alizitaja nyaraka na vitu vingine wanavyotakiwa kuvipeleka Aprili 16 ni hati ya usajili wa kanisa, bodi ya udhamini wa kanisa na majina yao, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake, na muundo wa uongozi wa kanisa lake.

Vingine ni namba ya usajili wa kanisa, ritani za kanisa lake (mapato na matumizi ya fedha za kanisa lake), mtu anayechukua na kurekodi mkanda wa video kanisani kwake, pamoja na waraka wa Baraza la Maaskofu uliosomwa makanisani.

Hata hivyo mapema jana asubuhi wafuasi wake walifika kwa wingi kituoni hapo huku wengine wakiwa wamevalia sare za Kikosi cha Polisi Jamii na wengine wakiwa wamevaa mavazi yanayovaliwa na viongozi wa dini yenye kola nyeupe kuonesha kuwa wao ni viongozi wa kanisa hilo.

Hali ya usalama ilikuwa imeimarishwa vya kutosha katika kituo hicho cha Polisi huku askari wa Kikosi cha Polisi Jamii kutoka katika kanisa la Gwajima wakiwa wamejipanga kuanzia lango la kuingilia kituoni hapo na kuachia hatua kadhaa mithili ya kumsubiri na kumpokea mfalme.

Hali hiyo iliwashangaza wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam waliokuwa wanapita karibu na eneo la kituo kikuu cha Polisi, na kusababisha hata wengine kuhatarisha usalama wao kutokana na hatari ya kugongwa na magari pamoja na vyombo vingine vya moto.

Mara baada ya kutoka kuhojiwa, wafuasi wake walishangilia na kurukaruka huku wakitanda barabara ya Stesheni na kusababisha adha ya usafiri kwani ilikuwa ni vigumu kwa magari kupita kutokana na purukushani na shangwe za wafuasi wa kiongozi huyo wa kiroho waliokuwa wametanda barabarani.

Hata hivyo, uwepo wa wafuasi hao ulikuwa ni kinyume cha sheria kwani tayari polisi walishapiga marufuku wafuasi hao kufika kituoni hapo wakati kiongozi wao akihojiwa.

Gwajima aliingia matatani mwishoni mwa mwezi uliopita na kujikuta akitakiwa kujisalimisha Polisi baada ya kutakiwa kufanya hivyo kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Katika siku ya kwanza aliyojisalimisha, Gwajima aliripotiwa kuzimia wakati akihojiwa na makachero wa Polisi kuhusiana na tuhuma dhidi ya Askofu Pengo, hali iliyosababisha akimbizwe hospitali ya TMJ, Mikocheni kwa matibabu alikokuwa kwa siku nne kabla ya kuachiwa kwa dhamana wakati akisubiri mahojiano zaidi.

Akiwa hospitalini hapo, wafuasi wake 15 wakiwemo wachungaji sita, mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), Dar es Salaam walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutaka kumtorosha askofu huyo kutoka hospitalini.

Ilielezwa kuwa, baada ya kuwapekua, watu hao walikutwa na begi lenye bastola aina ya BERRETA yenye namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za Short gun na vitabu viwili vya hundi.


Begi hilo liliripotiwa kuwa na hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Joseph Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundi cha Benki ya Equity, nyaraka mbalimbali za kampuni ya PUMA, chaja ya Simu na Tablets, suti mbili na nguo za ndani.
HABARI LEO

No comments:

Post a Comment