JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetoa
onyo kwa wafuasi wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambao
leo wamepanga kumsindikiza kiongozi wao kwenda katika mahojiano na jeshi hilo.
Hatua ya wafuasi hao kutaka kumsindikiza kiongozi huyo,
imekuja baaada ya kutangaziwa kujitokeza kwa wingi wakiwa katika kanisa hilo
lilipo Kawe, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi jana, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, alisema Askofu Gwajima
anaruhusiwa kwenda katika mahojiano na wanasheria pamoja na wasaidizi wake
wasiozidi watano tu.
“Ni bora wafuasi hao wakaendelea na shughuli zao za
kawaida zikiwamo za uzalishaji mali kuliko kurundikana katika geti la polisi
kwa sababu watakaofika kituoni hapa bila kuitwa watachukuliwa hatua za
kisheria,” alisema Kova.
Alisema kutokana na hali hiyo, hawategemei kuona
mrundikano katika maeneo hayo kwani kufanya hivyo ni kusababisha mkusanyiko
usiokuwa na kibali.
Kwa upande wake, mwanasheria wa Gwajima, John Mallya,
alisema mpango wa waumini wa kanisa hilo kumsindikiza kiongozi wao upo pale
pale.
“Waumini wataenda kama kawaida kumsindikiza kiongozi wao
kwa hiyo mpango huo utabaki pale pale kama walivyotangaziwa,” alisema Mallya.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Askofu Gwajima alifikishwa
kituoni hapo kwa tuhuma za kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Akiwa katika mahojiano, Askofu Gwajima alianguka na
kuzimia hali iliyosababisha kukimbizwa katika hospitali ya polisi iliyopo
Kurasini na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Baadaye alipelekwa na kulazwa katika Hospitali ya TMJ
jijini Dar es Salaam kabla ya kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo huku akiwa
anasukumwa katika kiti cha wagonjwa.
Mtanzania
No comments:
Post a Comment