Pages

Sunday, May 3, 2015

BOMU LIMEJERUHI WATU WATANO MOROGORO

Watu watano wamejeruhiwa katika tukio linalodaiwa kuwa la kigaidi baada ya kulipuliwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu. Tukio hilo inasemekana kutokea siku ya maadhimisho ya Mei mosi, katika kijiji cha Msolwa ujamaa, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Aidha, tukio hilo limetokea karibu na eneo ambalo siku chache zilizopita, jeshi la polisi lilikamata watu 10
wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi, majambia, risasi, bendera, vitabu na madaftari wakiwa ndani ya msikiti katika kijiji cha Kidatu wilayani hapa.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, saa 2.00 usiku juzi katika kijiji cha Sanje.

Alisema wananchi wa eneo hilo waliwaona vijana wawili wakipita katika eneo hilo na kuwatilia mashaka kutokana na muonekana wao.

Alisema mpaka sasa hajapata taarifa kamili za chanzo cha tukio, lakini alisema inawezekana ni muendelezo wa matukio ya kihalifu yaliyotokana na kukamatwa kwa watuhumiwa 12, waliokutwa na vitu mbalimbali ikiwamo milipuko hivi karibuni.

Alisema katika tukio hilo, watu watano wamejeruhiwa akiwamo dereva wa gari la halmashauri linalotumiwa na mwenyekiti wake, David Ligazio, ambalo limevunjwa kioo cha nyuma na mbele kikipasuliwa na mlipuko huo.

Alisema majeruhi wote akiwamo dereva wa gari hilo lenye namba za usajili SM 10632, Novatus Ngope (47), walikimbizwa katika kituo cha afya cha Nyandeo na baadaye kuhamishiwa  Hospitali ya Mtakatifu Kizito, wilayani Kilosa.

Katika tukio hilo, Ligazio akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya sikukuu hiyo kata ya Sanje, alikuja Mwenyekiti wa kitongoji hicho Joseph Mhenga akiwa na vijana wawili walioonekana si wenyeji wa eneo hilo.

Alisema mwenyekiti huyo alitaka ushauri  kuhusu vijana hao na ndipo alipoamuru wapelekwe katika kituo cha polisi.

Alisema kabla ya kupelekwa kituoni, vijana hao walipekuliwa na mmoja wa askari mgambo na kukutwa na bomu ambalo walilitoa na  kulirushia kwenye gari la mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero.

Alisema bomu hilo lililipuka na kumjeruhi dereva na watu wengine wanne akiwamo askari mgambo ambayo hali yake ni mbaya.

Aliwataja wengine kuwa ni Amos Msopole(29) na Azama Naniyunya (59), ambao wamelazwa  hospitali ya Mt. Kizito, Mikumi wilayani Kilosa.

Akizungumzia tukio hilo, Afisa Mtendaji wa kata ya Sanje, Hawa Ndachuwa, alisema siku ya tukio watu wawili walikodi pikipiki kutoka Kidatu na kuomba wapelekwe Mkula.

Hata hivyo, dereva wa bodaboda aliwatilia shaka na kujifanya anawaomba wamuongezee fedha za malipo kwani mapatano hayakulingana na umbali.

Alisema watu hao walikubali kumuongezea fedha na walimwomba kuwaonyesha sehemu ya kutolea fedha. Wakati wakihangaika kutoa fedha, mwendesha bodaboda huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji.

Alisema baada ya wananchi kuwaona watu hao, walipatwa na mshituko kutokana na mavazi yao na kuanza kuwapekua chini ya ulinzi wa askari mgambo wa kijiji.

Alisema mtuhumiwa mmoja alikutwa na viberiti vya gesi na mwingine alikuwa mgumu kutoa ushirikiano na wananchi walizidi kumtilia shaka baada ya kuona kuwa ana kitu alichokihifadhi katika kiuno.

Alisema wakati wanaendelea kuwapekua mtuhumiwa wa kwanza alifanikiwa kukimbia. Aidha, wakati wanajiandaa kumdhibiti wa pili alitoa kitu kinachofanana na bomu na kurusha lilipo hilo gari la mwenyekiti na kutoa mlipuko mkubwa na yeye kufanikiwa kukimbia.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul, alipotafutwa kwa njia ya simu, msaidizi wake alisema amekwenda eneo la tukio.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Maximilian Mwenda, alithibisha kupokea majeruhi wanne.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment