Pages

Sunday, May 3, 2015

Kutana na Evelyne Rugemalila, mbunifu anayetamba kuwang'arisha vibonge

Kwa wafuatiliaji wa masuala ya mitindo na wanamitindo wa ndani, Evelyn Rugemarila si jina geni masikioni mwao.    Kupitia lebo yake ya Eve Collections, Evelyn ameingia kwenye orodha ya wabunifu wa mavazi ya wanawake wanaofanya vizuri kwa sasa nchini Tanzania.

“Siku zote nimekuwa naamini
nachokifanya na kukubali kujifunza kutoka kwa watu wengine,” anasema Evelyn katika mahojiano na Johari.

“Kuna wakati unaweza kutamani kufanya kitu, lakini wewe mwenyewe ukajikatisha tamaa. Wengi wanakosea hapo hasa wanawake.

“Binafsi nilijiamini wakati naanza kazi hii ndiyo maana nimeweza kusimama mpaka leo na najivunia kuwa miongoni mwa wabunifu mahiri nchini Tanzania,” anasema mbunifu huyo.

Safari yake kuelekea kuwa mbunifu
“Nilimuelezea wazo langu mama yangu namshukuru Mungu alinielewa na kuniunga mkono kwa kunipatia fedha. Nikaagiza vifaa China na kuanza kufuata malighafi za vitambaa Nigeria.”

Mtazamo wake katika tasnia ya mitindo

Evelyn anaelezea kuwa kuna maendeleo makubwa katika tasnia hii ambayo kwa sasa inaonekana kuanza kuingia vichwani mwa Watanzania wengi.

Anaeleza kuwa kumekuwepo na ongezeko la wabunifu ambao wanajitahidi kutengeneza nguo mbalimbali na Watanzania kwa kiasi fulani wameanza kuonyesha muamko wa kupenda kazi za nyumbani.

Pamoja na mafanikio hayo, Evelyn anasema kuwa bado kuna watu wanaojiita wabunifu lakini  hakuna ubunifu wanaofanya na matokeo yake wanaiga mitindo ya wengine.

“Nasema hivyo kwa ushahidi. Kuna watu nawafahamu fika kuwa wanakubali kuchukua mitindo yangu kutoka kwa wateja na kuwashonea kwa gharama nafuu.

Kutokana na ukweli huo ni ngumu kwa tasnia yetu kukua na kuyafikia mataifa mengine kama wenzetu Nigeria. Kule kila mbunifu ana ladha yake na hakuna anayekubali kuiga kazi ya mwenzake,” anasisitiza.

Anafafanua kuwa kwa uzoefu wake wa kutembelea nchi mbalimbali amegundua kuwa watu wengi wanaojihusisha na ubunifu wamesomea na kuwekeza fedha za kutosha kwenye kazi zao.

“Mataifa mengine huwezi kuwa mbunifu bila kuwa na elimu au kuwekeza fedha za kutosha kutafuta malighafi nzuri na sio kubabaisha kama ambavyo wengi wanafanya hapa nchini,” anafafanua.

Mwanamama huyo anasema mpaka sasa  ameshashiriki maonyesho mawili ya mitindo nje ya nchi na kufanikiwa kuzitangaza nguo zake ambazo kwa kiasi kikubwa hutawaliwa na nakshi za Kiafrika.

Historia kwa ufupi

Evelyn alizaliwa Desemba 1971, mjini Muleba akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu ya mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemarila.


Evelyn anasema alijikuta katika tasnia hiyo baada ya kushindwa kupata nguo zinazoendana na mwili wake.

Evelyn anaeleza kuwa unene wa mwili wake ulimuweka katika wakati mgumu kupata nguo zinazomtosha na kumkaa vizuri mwilini.

“Napenda kuvaa vizuri lakini nilikuwa sipati nguo zinazonikaa kwa jinsi ninavyopenda mpaka nilivyokwenda kumtembelea ndugu yangu nchini Nigeria,” anasema.

Anasema akiwa Nigeria alivutiwa na namna wabunifu wa nchi hiyo walivyokuwa wakitengeneza nguo zao kwa kutumia vitambaa vyenye nakshi za kuvutia.

“Binafsi nilipenda jinsi walivyonishonea nguo ambazo zilinikaa vizuri kwenye mwili ambao mpaka wakati huo ilikuwa ngumu kupata vazi linalonipendeza kutokana na unene”.

Aliporejea nyumbani watu wengi walionyesha kuzipenda nguo hizo na kumshawishi kubuni mavazi kwa kutumia malighafi za vitambaa kutoka Nigeria.

Kwa kuwa alikuwa na mapenzi na ushonaji, akaona ni vyema akaifanya kazi hiyo kwa kiwango cha ubora zaidi kwa kuwalenga watu wenye maumbile makubwa.
Elimu ya msingi aliipata Shule ya Msingi ya Mlimani jijini Dar es Salaam na kisha kuhamia Arusha alikomalizia darasa la saba.

Baada ya kuhitimu elimu ya msingi alijiunga na masomo ya kidato cha kwanza nchini Kenya ambako alisoma mpaka kidato cha tano.

Alikwenda Uingereza katika Chuo cha Reden alikojiunga na kidato cha sita kisha kuunganisha elimu ya shahada ya sosholojia chuoni hapo.

Huo haukuwa mwisho wa safari ya elimu, kwani aliendelea na stashahada ya utawala katika Chuo Kikuu cha East London kisha kendelea na Shahada ya juu Chuo Kikuu cha West Minister.

Baada ya kumaliza masomo yake Evelyn  alirejea nyumbani na kujihusisha na biashara za familia yake ambayo kwa wakati huo walikuwa na  kampuni iliyokuwa ikijihusisha na  uingizaji na usambazaji wa bia ya Heineken nchini.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment