Pages

Sunday, May 3, 2015

MWANDOSYA: Mungu ameniponya niwatumikie Watanzania.........Amesema ni mwanasiasa pekee MWENYE BAHATI KUBWA ya kuzushiwa kifo mara tatu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) Profesa Mark Mwandosya, amesema kitendo cha kuzushiwa kufa mara tatu na kunusurika kufa akiwa anaumwa  kimeonesha jinsi Mungu anavyompenda na kuthamini kazi yake kwa Watanzania.

Akifafanua mambo mbalimbali aliyoulizwa kuhusiana na kuonekana akiwa mkimya, 
huku watu mbalimbali wakimtaja kuwa miongoni mwa wanaotajwa kuwania kuteuliwa  na CCM  kupokea kijiti cha urais kutoka mikononi mwa rais wa awamu ya nne, Dkt.Jakaya  Kikwete, alisema amekuwa akitumia muda mwingi kufanya  kazi za  Watanzania.

Alisema mara baada ya kupona na kuimarika akiwa amepewa wadhifa huo wa kumsaidia Rais katika ofisi yake amekuwa akitumia muda mwingi kufanya kazi  akimsaidia rais ili Watanzania wapate maisha bora ili kuifanya imani ya aliyemteua ipate haki yake.

"Unajua mimi niliteuliwa na Rais kwa imani kubwa nikiwa sijaimarika vema  baada ya kutoka kuugua na hivyo baada  ya kuimarika Mungu amenisaidia kwa hakika kazi yangu  kubwa  imekuwa ni kufanya kazi kusaidia Watanzania  kulingana  na  jinsi  nilivyopangiwa na  Rais," alisema Profesa Mwandosya.

Alisema kuwa ni kiongozi wa Serikali na mwanasiasa pekee mwenye bahati kubwa  ya kuzushiwa kifo mara tatu huku taarifa zikiwa  zimesambaa  bila  kujua  nani alikuwa anafanya kazi hiyo. Hata hivyo alisema amekuwa na afya  njema   hadi  sasa akiwa anaendelea  kufanya kazi za wananchi.

"Mimi naamini kuwa pamoja na kuzushiwa kifo mara tatu Mungu aliniponya kwa  upendo wake na kwa kutambua utumishi wangu kwa Watanzania  niliouonesha tangu  nianze uwaziri katika wizara ya Uchukuzi,Mazingira, Maji na sasa  katika  ofisi  ya  Rais,naamini Mungu amethamini kazi yangu," alisema.

Prof. Mwandosya ambaye ni mbunge  wa Jimbo la Rungwe Mashariki,ambaye  ametangaza kutowania tena  nafasi hiyo  baada  ya kuchaguliwa kwa nyakati zote bila ya kupingwa huku mwaka 2005 akifanikiwa kuingia katika mchakato wa kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM," alisema imani yake  ni kuwa Watanzania watapata kiongozi makini.

Alisema amekuwa akiulizwa mara kwa mara kuhusu ukimya wake wa kutotaka kuzungumzia masuala ya kutangaza rasmi kuwania  urais ambapo amekuwa akijibu wazi kuwa Watanzania wasubiri wakati filimbi ipigwe na chama na ndipo  atakapoweza kutoa msimamo wake kwa kufuata taratibu za  chama  zilizowekwa.

Alisema kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni kwa Wtanzania kulinda   amani na utulivu wakati huu wa kuelekea kupata  Katiba Mpya na kupata viongozi  wapya watakaoweza kuongoza katika kipindi cha awamu ya tano tangu Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania   ianze.

MAJIRA

No comments:

Post a Comment