Pages

Friday, May 8, 2015

Mafuriko Dar, nyumba zajaa maji wananchi wahaha..

Wananchi wakivushana eneo la jangwani
HALI tete imelikumba jiji la Dar es Salaam kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha tokea jana kiasi cha kusababisha mafuriko hasa katika maeneo ya mabonde huku familia nyingi zikikosa makazi baada ya nyumba wanazoishi kujaa maji.

Kufuatia hali hii Serikali imetangaza kuifunga kwa muda barabara ya
Jangwani baada ya eneo hilo kujaa maji kiasi kwamba hakuna gari inayoweza kuingia wala kutoka.

Eneo la jangwani na Posta yametajwa kuwa Miongoni mwa maeneo ambayo yameathirika zaidi na mvua hii, na maeneo mengine ni Bonde la Mpunga Msasani, Mwananyamala, na Masaki.

Inadaiwa kuwa nyumba nyingi zimejaa maji kiasi cha kuwafanya watu kuhama makazi yao huku wakipoteza thamani zao zilizokuwa ndani ya nyumba zao.

Maeneo mengine ni yale ambayo mto Msimbazi umepita, ambapo wakazi wengi wanaokaa kandokando ya mto huo wameathiriwa vibaya na mvua baada ya mto huo kujaa na kuanza kuingia kwenye makazi ya watu.

Pamoja na kunyesha kwa mvua hiyo, hadi majira haya hakuna taarifa za kifo zilizotolewa, aidha vyombo vya usalama vimeendelea kutoa msaada kwa waathiriaka mbalimbali wa mafuriko hayo.

wakazi wa eneo la Sinza hasa katika eneo la Bamaga, wamesikitishwa na kitendo cha watu kuziba mitaro kwa kutupa takataka ovyo, wakieleza kuwa hicho ndiyo chanzo cha kufurika kwa maji katika mitaa yao jambo ambalo limesababisha adha kubwa.

Eneo lingine ambalo limeathirika ni Kinondoni ambapo wananchi wa maeneo ya mabonde wanalalamika kuchelewa kutoa vitu vyao ndani, kwani asilimia kubwa ya wakazi hao mali zao zimezama ndani ya vyumba vyao.

Maeneo mengine ambayo wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanaendelea kuhaha ni pamoja na eneo la  Mabibo, Tandale, Tabata, Mwananyamala Kisiwani, kwa Kopa, Tabata Kinyerezi, na eneo la posta ambapo ofisi nyingi zimeonekana kuzingirwa na maji huku hali ya sintofahamu ikitawa.

Pamoja na kuendelea kunyesha kwa mvua hiyo vijana wa kazi wamekuwa wakijipatia ridhiki kwa kuwavusha watu maeneo mbalimbali kwa gharama ya kati ya Sh500 hadi 1000, tuvuti hii ilipozungumza nao walijieleza kuwa wapo tayari kuwasaidia watu, kuwavusha maeneo mbalimbali na pindi wanapofanya hivyo hupewa fedha za shukrani.

“Hatuwezi kuomba mvua iendelee kunyesha, kwani inaleta usumbufu mkubwa wa watu, pia mali nyingi kupotea, hii ni kazi ya Mungu, na sisi tunapata riziki humuhumu, tunasaidia kuwavusha watu, pia kusukuma magari yanapokwama, tunapofanya hivi tunapewa pesa kidogo kati ya Sh 500 hadi 1000”,  amesema kijana mmoja katika eneo la Jangwani.

Aidha wataalamu wa hali ya hewa wanaeleza wazi kuwa kama mvua ikiendelea kunyesha kwa muda wa siku tatu ama nne mfululizo madhara amakubwa yanaweza kujitokeza katika jiji la Dar es Salaam kufuatia kuziba kwa miundombinu ya kupitisha maji.
Aidha sababu nyingine iliyotajwa ni wananchi kuvamia na kujenga kandokando ya mito na mabwawa ambayo awali yalikuwa yanasaidia kuhifadhi maji ili yasiwadhuru wananchi..

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment