Pages

Saturday, May 2, 2015

Wateja wa Luku wazidi kutaabika......Tanesco imesema kuwa huduma zinaendelea kupatikana vituo mbalimbali vya MAXCOM, ATM za CRDB na NMB

Wakati wateja wa umeme wamendelea kutaabika, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limetoa malekezo zaidi ya namna ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi.

Taarifa ya Tanesco imekuja baada ya tatizo lililojitokeza kwa baadhi ya mawakala wa Luku kushindwa
kutoa huduma ya kuuza umeme na kusema litamalizika karibuni.

Hali hiyo imetokana na Kampuni ya Selcom ambaye ni wakala wa kuuza na kuziunganisha baadhi ya kampuni za simu kwa Tanesco kusitishiwa huduma kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu yake ikiwamo kughushi nyaraka na kukiuka taratibu za kulipa kodi.

Taarifa iliyotolewa jana na shirika hilo, na kusainiwa na Ofisa Habari wake, Adrian Severin ilisema kuwa huduma zinaendelea kupatikana kupitia Kampuni ya MAXCOM katika Vituo mbalimbali, ATM za CRDB na NMB, NMB Mobile pamoja na ofisi zote za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nchi nzima hadi siku ya Jumamosi na Jumapili na siku za Sikukukuu kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku.

“Shirika linaomba radhi kwa usumbufu wowote unaojitokeza, wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa”alisema Sevelin.

Wakazi wa Dar waonja joto ya jiwe

Gazeti hili lilizunguka katika vituo mbalimbali vya kutoa huduma hiyo na kukuta misululu ya wananchi wakisubiri huduma hiyo huku kukiwa na tatizo la mtandao.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti katika vituo mbalimbali kikiwamo cha Kisutu, Kinondoni Mkwajuni, Buguruni Sheli, Gongo la Mboto, Faya, Mwananyamala , Mwenge Mpakani, Kigogo, Tandale, Mbagala Zakhem, walisema kuwa wamesimama katika foleni hizo kusubiri huduma hiyo tangu saa 12 asubuhi.

Imelda Wahuzi aliyekutwa katika kituo cha Buguruni alisema kuwa ameanza kupata adha hiyo tangu jana mchana , ambapo aliahirisha kununua akiadhimia kudamka asubuhi ya leo, lakini anashangaa amefika kituoni hapo saa 12asubuhi na hadi saa nne asubuhi hajapata umeme.

Muuza umeme katika kituo hicho ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kuwa pamoja na watu kuja kwa wingi kupata huduma hiyo katika kituo hicho bado kuna tatizo la mtandao kusumbua ndiyo maana foleni inakuwa kubwa.

Alisema kama siyo mtandao kusingekuwa na foleni, huku akikiri kuwa hajawahi kuwa na watu wengi kama siku hizi mbili, yaani juzi na jana.

Ibrahimu Hassan aliyekutwa katika foleni Kisutu alisema kuwa amelazimika kusitisha shughuli zake baada ya siku iliyopita kupata hasara kwa sababu hakufanya kazi katika kiwanda chake cha kuchomelea mageti kutokana na kukosa umeme.

Alisema hajawahi kununua umeme katika foleni kiasi hicho kwani hununua kwa njia ya simu, baada ya kupata ujumbe mfupi kutoka kwenye mtandao wa simu kuwa hawezi kununua umeme kutokana na tatizo la kiufundi ndiyo amefika katika kituo hicho.

Wakizungumza kwa jazba na mwandishi wa gazeti hili, wateja waliokutwa katika kituo cha mafuta mpakani, walisema kuwa ni kero kwani hakuna mwenye uhakika wa kupata umeme kwani kila saa mtandao unagoma.

“Hii nchi bwana kama imeuzwa, kila kitu shida, ukienda benki foleni, hospitali, kwenye maji basi hata umeme, tumechoka jamani, ”alisema kijana wa makamo aliyejitambulisha kwa jina moja la Henry.

Kwa upande wa muuza umeme katika kituo cha Mbagala Rangi Tatu, Hidaya Ussi alisema kuwa kila unapofika mwisho wa mwezi kunakuwa na adha kama hiyo ya wateja kuwa wengi. “Hali hii ni kawaida kila mwezi huwa tunakutana nayo, wateja wanakuwa wengi, lakini jana (juzi) na leo (jana) wamezidi kwa sababu baadhi ya vituo vidogo vidogo vimefungwa hivyo wote wanakuja huku, mtandao nao unachangia huduma kuwa ya taratibu, ”alisema Ussi.

Selcom waiangukia Wizara

Mkurugenzi Mtendaji wa Selcom, Sameer Hirji, amemuomba Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene aingilie kati mgogoro wao na Tanesco ili waendelee kutoa huduma, huku akifafanua tuhuma zilizotolewa dhidi yao juu ya kukiuka kulipa kodi. Selcom ilisitishiwa kutoa huduma kwa kile kilichoelezwa kukwepa kodi.

Taarifa ya mkurugenzi huyo kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa lengo lao siyo kuharibu huduma bali kuziboresha hivyo Waziri kwa kutumia mamlaka yake anaweza kuumaliza mgogoro huo.

“Kwa kuzingatia makubaliano yetu na Tanesco juu ya uuzaji wa Luku tumekuwa wahanga wa mara kwa mara kwa jambo hili kwa kuliweka wazi hili Selcom haiwajibiki kwa TRA. Utaratibu wa mauzo ya Luku kama ulivyoanishwa chini ya sheria ya mwaka 2011 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) Tanesco ndiye mmiliki halali husika wa bidhaa na siyo msambazaji wa huduma,, ” ilisema taarifa hiyo.

Hata hivyo, jana mchana Selcom iliwatumia ujumbe mfupi mawakala wao kuwaomba radhi kutokana na usumbufu uliojitokeza

“Tuomba radhi kwa usumbufu mnaopata kutokana na tatizo la Luku, juhudi zinafanyika kuhakikisha huduma hii inaanza kufanya kazi haraka iwezekanavyo asante,” ulisomeka ujumbe huo.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment