Pages

Wednesday, December 2, 2015

HUENDA UNA MASWALI MENGI KABLA HUJAFIKIA UAMUZI WA KUNUNUA KITANDA CHA CHUMA. HIZI NI FAIDA NA CHANGAMOTO ZAKE


Moja kati ya manunuzi muhimu zaidi ambayo utafanya ukiwa mahali unapoishi ni kitanda. Kitanda chako ndio mahali unapopata usingizi unaouhitaji sana ili mwili wako uweze kuchaji kwa ajili ya pilika za siku inayofuata. Kuhakikisha kuwa unapata faida zote za usingizi unatakiwa kuwa na kitanda sahihi ambacho kitapumzisha mwili wako vizuri.
Na hii ndio sababu unatakiwa kuwa na godoro la uhakika pamoja na fremu ya kitanda imara kukidhi matakwa ya mwili wako. Mbali na usingizi mnono unaopata kutokana na kitanda sahii, vilevile kitanda hicho kinaleta mvuto kwenye chumba cha kulala.

Kwa maana hiyo fremu ya kitanda ni jambo muhimu la kuchunguza kabla ya kufanya uamuzi wa kununua. Kazi kubwa ya fremu hii ni kubeba godoro na kufanya kitanda kiwe tayari kwa kutumika. Fremu ya kitanda inaweza kutengenezwa kwa malighafi zozote lakini malighafi mbili kubwa ni mbao na chuma. Wakati wa kuchagua fremu hii ya kitanda vigezo vikubwa huwa ni ladha binafsi ya mnunuzi, bajeti na uimara unaohitaji.

Katika kuandaa makala hii nimefanya mahojiano na Bi Janet Moshi ambaye ni mjasiriamali anayetengeneza fenicha za chuma na ameeleza kwa kina faida na changamoto za kitanda cha chuma.

Anaeleza dondoo zifuatazo kuhusiana na faida  za kitanda cha chuma. Dondoo hizi zitakusaidia wakati wa kufanya uamuzi wa manunuzi ya fremu ya kitanda.

Uimara- Kama unataka kununua kitanda ambacho kitadumu muda mrefu na kinahimili uchakavu basi nunua cha chuma. Kitanda cha chuma hakiharibiki kirahisi na hata pale vinapokuwa ni viwili pamoja vya kubebana juu na chini hukuti vikilegea na kuchezacheza. Utunzaji unaotakiwa sanasana ni mmoja tu nao ni kupaka rangi baada ya kipindi. Kutokana na uimara wake, bila shaka hutakaa ujutie kuwekeza kwenye kitanda cha chuma.

Wepesi- Kitanda cha chumba ni chepesi ukilinganisha na kitanda cha mbao ngumu kwa maana ya mkongo na mninga. Hii inarahisisha usogezaji wa pasipo kufungua sukuruu pale unapotaka kukihamisha toka eneo moja la chumba kwenda lingine ndani ya chumba hicho chicho.

Gharama- Faida kuu muhimu ya kitanda cha chuma ni kuwa bei yake iko chini, kwa mfano wakati kitanda cha chuma cha futi sita kwa sita ki nauzwa shilingi laki sita, kile cha ukubwa huohuo cha mninga au mkongo kinauzwa shilingi milioni 2. Baadhi ya watu wanadhania vitanda vya chuma ni ghali kutokana na urembo wake, lakini kumbe sio. Fremu ya kitanda inapokuwa ya gharama nafuu inakuwezesha kuwekeza hela zaidi kwa ajili ya kununua gogodo imara zaidi.

Matumizi- Uraisi wa kukibomoa pale ambapo unakihamisha toka eneo moja hadi lingine. Kitanda cha chuma kimeunganishwa kwa sukuruu na nati na ndio maana ni rahisi kukifungua na kukibeba vipandevipande.

Upatikanaji- Unaweza kupata kitanda cha chuma cha ukubwa wowote na chenye vizuizi vya kuzuia godoro lisikimbie angalau kila mahali penye mafundi vyuma. Na hata kama unatafuta cha mtoto unapata na kwa rangi unayohitaji.

Muonekano- Kitanda cha chuma kina muonekano rahisi kabisa hadi ule ambao una mapambo mengi mno. Vitanda vya chuma vinaambatana na mionekano mingi maridadi na ya kipekee. Na kwa maana hiyo chumba kizima cha kulala kinaonekana kuwa na mvuto kutokana na urembo wa kitanda. Pia ni rahisi kubadili mapambo ya kitanda cha chuma pale unatakapohitaji kufanya hivyo.

Eneo- Kitanda cha chuma kinawezesha matumizi madogo ya eneo. Kwa maana ya kwamba miguu yake sio mipana kama ya kitanda cha mbao. Kwa hivyo unakuta eneo ambalo kitanda cha chuma kinatosha, eneo hilohilo kitanda cha mbao cha ukubwa huohuo kisingetosha. Hii ni faida kwa yule mwenye chumba kidogo cha kulala.

Mvungu- Kwa kawaida kitanda cha chuma kimeenda juu kuliko cha boksi cha mbao. Na hii inawezesha urahisi wa kufanya usafi eneo la chini ya kitanda. Zaidi ya hilo, eneo chini ya kitanda cha chuma linaweza kutumika kuhifadhi baadhi ya vitu na hivyo kukuongezea mahali pa kuhifadhia hapo chumbani.

Changamoto za kitanda cha chuma ni hizi zifuatazo:

Endapo ile mipira kwenye miguu ya kitanda cha chuma itasagika na kutokurudishiwa mipya basi kuna uwezekano wa miguu ya kitanda kuharibu sakafu pale kinaposogezwa kwa kuburuzwa.

Chuma kina kawaida ya kubadilika kuendana na hali ya joto au baridi. Endapo chumbani kuna baridi basi tegemea chuma za kitanda nazo kuwa na baridi. Vilevile kwa upande wa joto.

Kitanda cha chuma kinaweza kisiwafae watu wa mabondeni ambao nyumba zao zinasimamisha maji sakafuni. Endapo nyakati za mvua sakafu ya chumba chenye kitanda cha chuma inasimamisha maji kwa siku mbili au tatu na kuendelea basi kuna uwezekano mkubwa wa miguu ya kitanda cha chumba kuharibiwa na kutu.

Msomaji wangu hizo ni faida na changamoto za kitanda cha chuma. Nina uhakika kuwa utafanya uamuzi sahihi pale utakapoamua kufanya manunuzi. Tukutane makala ijayo!

Je, unauza bidhaa au huduma inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue? Nijulishe simu/whatsapp 0755200023 







No comments:

Post a Comment