Thursday, December 4, 2014

my article for newspaper: ubora wa tile za bafuni

Umuhimu wa kujali ubora wakati wa kununua marumaru za bafuni


Bila shaka kila mmoja anataka apate bidhaa au huduma kwa thamani ya hela aliyotoa wakati wa ujenzi wa nyumba yake, lakini chaguo la marumaru za bafuni inahitaji kuwa makini zaidi ya hilo. Katika makala hii nitakuwa na Mhandisi David ambaye atatujuza umuhimu wa kuzingatia ubora zaidi ya gharama wakati wa kununua marumaru za bafuni.

Unaweza kuwa umepata marumaru za bei nafuu, lakini zisizokuwa na kiwango. Marumaru za aina hii zitakugharimu kwa kiasi kikubwa muda wote utakaokuwa unaishi kwenye nyumba yako hiyo.
Linapokuja swala la marumaru za bafuni, malighafi, rangi, uimara, mtelezo, na usimikaji ni mambo muhimu zaidi ya kuzingatia, anasema David. Hakikisha kuwa unapata ushauri kwa fundi mwenye uwezo kabla ya kufikia kufanya uamuzi.

Marumaru za bafuni zipo za kuanzia maumbo madogo zenye nyongeza ya border za aina na michoro mbalimbali. Wajenzi wanatafuta marumaru za maumbo tofauti tofauti  kutoka umbo la pembe nne lililozoeleka hadi malighafi nyingine kama mawe ya asili na vioo. Wanapenda pia mabafu yao yawe na muonekano wa  kazi za sanaa zaidi, anasema David. Ila marumaru za bafuni zinafanya kazi kubwa, zinatakiwa kufanya mvuke usisambae vyumba vingine na kulinda kuta zisiharibiwe na ukungu na hali ya umajimaji. Zinatakiwa zizibwe vyema na grout maeneo ya miungio na ziwe na usalama kutembea juu yake zinapowkuwa zimeloa, anasema mhandishi.

Pamoja na mawe ya asili, marumaru bado zitabaki kuwa chaguo maarufu zaidi kwa ajili ya kuta na sakafu za bafuni. Marumaru ngumu zina rangi sawa kwenye unene wake wote, ingawa zina gharama zaidi, na hapa ndipo mnunuzi anapopaswa kuwa makini. Ujue kutofautisha kama unanunua marumaru zilizopakwa rangi kwa juu tu, na hizi ni zile nyepesi na bei yake iko chini. Aina hii ni kuwa baada ya muda si mrefu rangi inatoka kutokana na kukanyagwa mara kwa mara, kwa kuwa rangi imepakwa kwenye eneo la juu la marumaru kwa unene kiasi tu na sio unene wote. Hizi zilizopakwa rangi inakuwa eneo la juu tu mfano barafu kwenye mlima au kwenye keki! Hizi za aina hii zinafaa zaidi kwa mapambo pengine kutengenezea ua la ukutani lakini sio kwa kuhimili shurba za sakafu ya bafuni. Marumaru  ambazo zina rangi hiyo hiyo hadi ndani kwenye kiini na unene wote wa marumaru ni imara zaidi kwa matumizi ya sakafu ya bafuni.

Kwa hivyo muhimu zaidi ni kutumia marumaru hizi ngumu zenye rangi sawa kila mahali kwa ajili ya sakafu na kuchagua za bei rahisi zinazoendana na zile ngumu kwa ajili ya ukuta, anasema David. Usimikaji wa marumaru ni kazi ya sanaa kwahivyo inahitaji fundi mwenye uwezo nayo.

Zaidi ya kuweka marumaru bafuni unaweza kuweka pia jiwe la asili kama vile marble lakini iliyo ngumu. Ubora wa jiwe na usimikaji wake ni muhimu sana. Uwekaji wa jiwe la asili ni wa kitaalam. Kunaweza kuwa na shida ya kufitisha slabu kubwa ya jiwe hilo kwenye maeneo ya kutolea maji machafu na kuingiza maji safi,  na muhimu zaidi ya yote sio kila jiwe la asili linafaa kwenye mazingira ya mvuke na majimaji ya bafuni, anasema mhandisi. Mawe mengine ya asili yananyonya maji na mwishowe kuwa na mipasuko.

Marumaru zitaongeza thamaini ya nyumba yako, kwahivyo kuwa tayari kutumia muda na pesa. Kwa bafu la kisasa na muonekno wa kifahari chagua marumaru zenye rangi za mwanga kama vile nyeupe ukutani huku ukiweka miisho na mpangilio fulani  wenye mvuto kwa baadhi ya maeneo ya ukuta.
Haijalishi ni mtindo gani wa marumaru utakaochagua kwa ajili ya bafu lako, zingatia ubora na usimikaji wa kitaalam kabla ya kufanya maamuzi yoyote. Dondoo muhimu kuliko zote, kabla hujaanza kutengeneza bafu lako angalia thamani ya nyumba yako. Ubora wa bafu uendane na thamani ya nyumba. Kwa kuzingatia hilo utafanya uamuzi sahihi kwa kushirikisha wataalam watakaokufanya usijutie maamuzi yako hapo baadaye.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment