Thursday, November 20, 2014

my article for newspaper: jinsi ya kupamba bedroom

Jinsi ya kupamba chumba cha kulala

Kwa nyumba nyingi chumba cha kulala ni chumba binafsi zaidi. Ni chumba pia ambacho kina vitu vingi zaidi binafsi. Kinaweza kuwa kama kiota cha mahaba au mahali patakatifu pa kulala na kupumzika. Pia kinaweza kuwa chumba cha kuchangamka na kutuliza kwa watoto, kwa jinsi wanavyokuwa wakigundua kuwa wanamiliki chumba chao wenyewe.
Kupenda kufurahisha marafiki, majirani na wageni; wenye nyumba wengi wanamalizia nguvu zao kupamba vile vyumba vya kuonekana na hadhara ndani ya nyumba. Umefika wakati wa kuwa mchoyo na kuelekeza nguvu zako kwenye chumba cha kulala. Juu ya yote ni kuwa kabla ya kuoga kujiaandaa kutoka ni lazima kwanza utokee kitandani.
Kwanza kabisa anza na kitanda kwa ajii kitovu cha chumba chochote cha kulala ni kitanda. Ni wazi kuwa kitu cha kwanza cha kuzingatia kwenye kitanda itakuwa ni godoro, lakini usisahau ubao wa kichwani. Ni ngumu kudharau umuhimu wa sababu za kisaikolojia katika kupata usingizi mwororo. Hisia na hata muonekano wa kitanda chako wakati unapoingia humo inaweza kuelezea ni namna gani unavyojisikia wakati unapotoka humo.
Kwa upande wa sakafu chaguo zuri zaidi kwa ajili ya chumba cha kulala ni zulia na mara zote imekuwa hivyo. Hamna kitu kizuri kama kuamka na kuweka miguu yako kwenye sakafu ambayo inaelekea kuwa na hisia kama za kitandani kwa kupata joto lile lile mithili ya la kitandani. Wengine hupenda kuweka sakafu za marumaru na mbao lakini eneo la pembeni mwa kitanda wengi wanapenda kuweka zulia.
Wazo la mwanga katika chumba cha kulala kwa baadhi linadharauliwa. Taa zisizokuwa na maridadi na balbu za juu ya kichwa tu zimeanza kupoteza mvuto kwenye chumba cha kulala cha kisasa. Taa za vivuli za kuweka juu ya vimeza vya kando mwa kitanda na za ukutani za maridadi ndio zinaendana na wakati kwa chumba cha kulala, kwa ajili ya mwanga wa chumba hiki kwa matumizi ya wakati wowote iwe ni mchana, jioni au usiku. Taa ndogo zinaweza kuwekwa kwa ajili ya kutumia muda maalum ambapo hutaki kuwasha taa zote kwa mfano wakati wa kusoma au kushikisha kifungo.

Kwa vyumba vidogo vya kulala mara nyingi vinafaidika na uwepo na makabati ya nguo, madroo na shelfu kwa kusaidia kuhifadhi na kuweka mpangilio. Baadhi ya vitu vidogo dogo na nguo vinapoukuwa vimewekwa kwenye sehemu hizi za kuhifadhia, chumba kinaonekana nadhifu.

Mara nyingi rangi za mwanga  zinashauriwa zaidi kwenye chumba cha kulala kwa ajili zinaleta hisia ya mapumziko. Rangi za vitambaa vya malazi viendane na rangi nyingine hapo chumbani na hata zile za samani. Shuka za rangi na maua ya kuvutia zinunuliwe ili kuongeza uzuri wa chumba.
Komfota lenye rangi nzito litaendana na samani au ubao wa kichwani wa mbao. Hii pia ni kweli kwa mapazia.

Wakati huo huo kumbuka kuweka samani zenye ukubwa na wingi wa kuendana na ukubwa wa chumba. Kabla hujanunua samani hizo ni vyema kwanza kufahamu mpangilio wa sakafu na ukubwa uliopo.

Kutengeneza bajeti ni muhimu kwa mradi wowote wa maboresho ya nyumbani. Kujipa wastani wa gharama inayohitajika itakusaidia kuamua ni nini kinachoweza kufanyika na kipi si kipaumbele. Baadhi ya shughuli kwenye mradi huu unaweza kufanya mwenyewe, kwa baadhi itakubidi utafute mtaalam. Kama kipaumbele chako ni ukuta kwa mfano, basi unaweza kutafuta mtalam wa rangi akapaka, ilihali ukitandika zulia mwenyewe. Vyovyote utakavyoamua, ni wakati wa kufanya chumba chako kuwa chako tena.

Kupamba chumba cha kulala ni shughuli mojawapo ya maboresho ya nyumbani ambayo inaweza kuhuisha tena afya yako na mahali unapoishi.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

...picha hizi za mapambo haya yamenitumbuiza...

Hii picha nimefurahishwa zaidi na jinsi ya kupamba kwa mto ya soseji. Angalia hilo sofa kati kaweka soseji na iliyokuwa sandwiched na square, so nice...


Hii fremu unaweza iweka jikoni hasa kama mlango wako wa jikoni ni wa kuingilia toka nje pia. Ni pambo na ukaribisho vilevile


 haya tena ni ubunifu tu

lovely

Kama unakaa nyumba ya ghorofa ona hapa chini ya ngazi unavyoweza kufanya mambo.

Monday, November 17, 2014

designs simple za majiko kwa wanaoanza familia

Kuna aina nyingi za majiko ambazo wewe mdada unayeanza familia unaweza kuchagua kulifanya jiko lako kuwa na mashiko na kufanya kazi iliyokusudiwa kwenye nyumba. Siku hizi imekuwa rahisi kupata mawazo kwa kuchungulia dondoo mbalimbali kwenye majarida, kudesa la jirani au rafiki, kuangalia video na mitandao mbalimbali kwa mfano unavyosoma hapa sasa.
Muonekano wa jiko kwa asilimia kubwa unachukuliwa na tile na makabati. Tile za floor na ukuta wa jiko, zipo za kumwaga, ni wewe tu kuamua rangi na muundo upi unataka na kwa finishing ipi. 
Kitu kingine  unatakiwa kuzingatia kwenye design ya jiko ni makabati. Hard wood eg mkongo, mninga ndio mambo yote na ni muhimu sana, usidanganyike kwa urembo wa soft wood kwani si lolote si chochote kwa jikoni. Jiko litolee gharama lidumu.
 hili kwa nyumba yako ya room 3 safi sana
 rangi za makabati nazo ni decoration
 tile za floo nimezipenda, na kuwa na kisehemu cha kulia kama nafasi inaruhusu si mbaya
 rangi zimenibamba ila tile za floor big nooo

Thursday, November 13, 2014

my article for newspaper: vioo vya mapambo

Boresha muonekano wa ndani ya nyumba kwa kuweka vioo vya mapambo.

Vioo vina kitu kwakweli ambacho ni maalum ndani yake. Vinakusaidia kukujulisha unaonekanaje na pia kukuwezesha kujiweka jinsi ambayo unataka uonekane. Zaidi ya haya maandalizi binafsi na kujiridhisha na muonekano wako kabla hujatoka, vioo vinasaidia pia kwenye kupamba ndani na hivyo kufanya muonekano wa nyumba kuwa maridadi na nadhifu zaidi kwa kila mgeni anayekutembelea.

Kama kuna pambo la ndani ambalo wenye nyumba hatakiwi kulikosa, basi ni kioo. Havitumiki tu kujiangalia unapoingia, bali vina mahadhi yake kwenye kuongeza staili ya chumba au muonekano wa kupagawisha kwa kumfanya mgeni kuduwaa. Sababu nyingine kuu hapa ni kuwa vioo vinaweza kuwa  na bajeti rafiki. Ni kweli kuwa kuna vioo ambavyo ni lazima viwepo nyumbani kwa matumizi kuwa watu wanahitaji ili kuhakikisha kuwa wanaonekana jinsi wanavyotaka kuonekana, lakini leo kwenye makala hii tunaongelea vioo kama mapambo ambavyo unaweka kwenye ukuta wa nyumba yako ili kuongeza staili na ukubwa.

Utagundua kuwa leo, sokoni kuna aina nyingi na tofauti za miundo na aina za vioo. Watengenezeaji wa vioo vya mapambo wanakuja juu kwa kuongeza ubunifu hasa wa fremu wanazofungia vioo hivi. Unaweza kuvipata vioo hivi vikiwa kwenye fremu ya kila malighafi unayohitaji kwa mandhari unaotaka kutengeneza.
Fremu nayo ni kigezo muhimu cha kioo kuwa kifaa cha mapambo. Unaweza kuagiza kioo kwa umbo unalotaka kwa mfano unaweza kuwa na kioo kwenye ukuta wa sebule ambacho kinatoa sura kwenye taswira nne kwa jinsi ambayo ukijitazama unaona uso nne zinazofanana.. Haijalishi staili unayotaka au bajeti uliyonayo, kuna uhakika wa kupata kioo ambacho ni sahihi kwa mradi wako.

Sababu ya kuweka vioo hivi ndani ya nyumba ni ukweli rahisi kuwa unataka kutumia ile hali ya kujiona ndani ya kioo kwa faida ya kimapambo. Baadhi wananunua vioo na kuvitundika kama sanaa nyingine za ukutani, kwa maana ya kuwa wanakitundika katikati ya picha na fremu nyingine, au wanakiweka kwenye ukuta ambao hauna kitu kingine ambacho kingefaa hapo. Hata hivyo unaweza kutumia vioo vya mapambo kuakisi mwanga na vifaa. Kwa mfano unaweza kuwa na ujia (corridor) ambao una mlango upande mmoja lakini mwingine hauna. Pambo lako hapo linaweza kuwa mmea wa kijani (uwe hai au mfu) pale kwenye ukuta usiokuwa na mlango pamoja na kioo. Kioo kitauakisi ujia kwa kuukuza uonekane mpana na mrefu. Kupamba kwa vioo kunafanya eneo dogo lionekane kubwa na mbinu hii inatumika na wataalam wengi wa ubunifu wa ndani nyumba.

Kupamba kwa vioo kunaongeza mwanga wa chumba. Chumba kilichopakwa rangi ya giza kinaweza kuonekana kidogo, kuongeza vioo kwenye kuta zake kutaboresha mwanga. Njia sahihi zaidi ya kuongeza mwanga wa jua bila kuongeza taa ni kufunga vioo vitazamane na madirisha. Vioo vinadaka mwanga wa jua toka dirishani na kuusambaza chumba kizima. Hii inaweza kuwa njia mojawapo pia ya kubana matumizi badala ya kuwasha taa mchana.

Kupamba kwa vioo vya mapambo hakuhitaji mtaalam. Mtu akiwa na vifaa vya toolbox anaweza kufunga vioo ukutani  na kutengeneza chumba chenye muonekano mzuri kwa gharama nafuu.
Chagua vioo vyenye maumbo ya kuvutia, pembe nne ni nzuri ila vioo vyenye maumbo yasiyozoeleka vinafanya umaridadi zaidi. Tafiti aina na maumbo mbalimbali ya vioo kabla hujamua ni vipi unataka.

Ili kukifanya chumba kisicho na uwiano kionekane kuwa nao, funga vioo vya mapambo ukutani. Vioo hivi viwekwe kuakisi vitu fulani kwenye chumba ili kufanya ionekane kama vitu hivi viko katika kila upande wa chumba, kwahivyo pale unapoingia uone kama chumba kina uwiano na ni kikubwa.

Baadhi ya wenye nyumba wanatamani waboreshe muonekano wa ndani wa nyumba zao. Marekebisho yana gharama kubwa, hata hivyo wewe mwenye nyumba usizime tamanio lako. Unaweza kunyanyua uso wa ndani ya nyumba yako kwa kutumia vioo vya mapambo badala ya marekebisho makubwa.. Mradi huu mdogo wa kunyanyua uso kwa kutumia vioo unaweza kukupa matokeo usiyotarajia. Kupamba kwa vioo ni moja kati ya njia nyepesi na rahisi za kuboresha muonekano wa ndani ya nyumba.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com



Saturday, November 8, 2014

tv cabinet ni moja kati ya post zangu iliyopendwa kuliko...

nakuongezea hapa dondoo chache za muhimu kabla hujanunua kabati la tv, twende kazi...
kabati hili ni moja kati ya fenicha ya msingi hapo sebuleni ambapo unakutana na marafiki zako, kula dinner na kuangalia tv. Wakati unapotaka kununua kabati la tv, ukubwa wa tv yako unahusu.
wakati wa kununua usifikirie tv tu. fikiria pia vitu vidogodogo ambavyo vinatakiwa kuwa hapo lakini vihifadhiwe, kwa mfano remote, kwahivyo nunua kabati lenye droo moja au mbili na hata likiwa pia na shelfu itakuwa poa zaidi.. kwahivyo kumbuka kuwa usifikirie tv tu.
la mwisho lakini si dogo unatakiwa uamue malighafi na rangi za kabati lako. kuna makabati mengi ambayo machoni yanavutia lakini kwa ubora si lolote si chochote. kwa swala la rangi hakikisha una research hadi uone kitu kinachokuvutia ndio ununue. Good luck!



super saturday na marafiki zangu wa ukweli...

hapa na pale leo na watu wangu wadogo...

 pozi la kibaunsa..sungusungu wangu
 pozi zikazidi hadi rafiki akalamba chini
akanyanyuka akijongea tartiiibu

Friday, November 7, 2014

njia rahisi kabisa ya kupamba sebule

kwa vile sebule ni sehemu muhimu ndani ya nyumba inahitaji kutupiwa jicho zaidi ya nyingine zote na ni lazima ipambwe kwa njia mbalimbali ili iwe na mvuto mbele ya kila mgeni anayekutembelea, na hii wala si ngumu.
kwanza kabisa weka fenicha zenye mvuto ambazo ni sofa, vimeza vya kando, kimeza cha kati, meza ya chakula na viti vyake.
weka taa maridadi na zenye mwanga wa kutosha kumulika sebule yote. weka taa za vivuli juu ya meza na sakafuni ili kuleta matokeo makubwa. kama wewe ni mshabiki wa wallpaper chagua ukuta wa tv ubandike, ning'iniza picha na fremu ukutani na hata vikapu vidogodogo vikiwa na maua ya kutengeneza.
weka vyungu vikubwa vya maua juu ya meza au sakafuni kwenye kona. weka kioo kikubwa katika ukuta wowote na upambe boda zake kwa fremu za kuvutia. unaweza pia kuweka sanamu kwenye kona na pembe za sebule yako.
mwisho kabisa usisahau kuweka pazia na fimbo za kuvutia.



Thursday, November 6, 2014

my article for newspaper: fenicha za kwenye bustani na varanda

Zingatia haya kabla ya kununua fenicha za nje ya nyumba


Fenicha za nje ya nyumba pia zinajulikana kama fenicha za kwenye bustani au varanda.  Aina hii ya fenicha huwa imetengenezwa kwa malighafi inayozuia maji kupenya, kwa kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya nje. Fenicha za  nje ya nyumba zimekuwa zikitumika toka enzi za himaya ya Roma.

Fenicha za nje ya nyumba  ni muhimu kwa mikutano wakati unapokuwa na kikundi cha watu kwa ajili ya siku maalum kama vile siku ya kuzaliwa na kadhalika. Hakuna kinachofurahisha zaidi kama kuwa na kiusingizi kwenye upepo mwanana wa kwenye varanda au bustani. Kuwa na chakula cha usiku na mwenzi wako wakati nyota ziking’aa angani inakuwa ni mahaba zaidi ya ndani ya nyumba.

Ila kuna jambo linalofanya aina hii ya fenicha kuwa tofauti na zile za ndani; malighafi ya fenicha za nje ya nyumba ni lazima iwe imara kwa sababu fenicha zitapambana na mvua kubwa, jua kali, upepo na baridi kali. Je hali ya hewa ya unapoishi ni joto na ukame, au unaishi karibia na pwani? Mvua ni za mara kwa mara? Haya yote ni maswali muhimu ya kupatikana majibu kabla ya kununua fenicha za nje ya nyumba. Hapa ni sababu, hali ya joto na ukame inafanya mbao kupasuka. Upepo mkali unaweza kufanya fenicha za aluminiam zipeperushwe.

Ndio maana ni muhimu sana kuhakikisha kuwa fenicha unazotumia kwenye mazingira ya nje ya nyumba ni sahihi kwa matumizi hayo.

Kwa malighafi, fenicha nyingi za kutumia nje ya nyumba zimetengenezwa kwa plastiki, mbao aluminiam na chuma cha pua. Amua ni malighafi ya aina gani unataka kwa ajili ya fenicha zako za nje. Vitu vitatu ambavyo vitakusaidia kuamua ni hali ya hewa, utunzaji na muonekano. Baadhi ya malighafi kama vile aluminiam hazihitaji utunzaji wa kina. Chuma cha pua kinaweza kudumu kwa muda mrefu sana na kinamudu joto na unyevu. Hapa ni muhimu kufahamu kuwa fenicha za nje za mbao sio imara kama nyingine, kwa hivyo inatakiwa kuziweka dawa mara kwa mara, anasema mseremala Rajab Hamis.Bottom of Form

Fenicha za nje ya nyumba zinakusaidia kuongeza ukubwa wa makazi yako, unapata eneo zaidi la kupumzika hasa wakati ule ambao jua sio kali sana au mvua sio nyingi. Kwa hivyo fenicha hizi zinakamilisha ahadi ya mapumziko, burudani na raha kwa ujumla. Uchaguzi wa fenicha za nje unazingatia hatua zilezile za kununua fenicha za ndani. Japo kunahitajika umakini wa ziada kwa ajili ya tofauti  kati ya fenicha hizi mbili.

Fikiria ni eneo kiasi gani ulilonalo na lina umbo la namna gani. Je ni varanda ndefu na nyembamba au ni fupi pana? Tumia eneo na umbo la varanda au bustani yako kufahamu ukubwa wa fenicha zako za nje. Hakikisha unaacha nafasi ya kutosha kati ya fenicha zako ili uweze kupishana kirahisi. Tumia utaratibu ule ule wa kupanga fenicha za ndani. Kwa eneo dogo meza za ukubwa wa kwenye mgahawa na stuli zitafaa zaidi kwani zitachukua nafasi ndogo.

Ni wapi utakapoweka fenicha zako za nje, je kwenye bustani yako kuna eneo la kukaa ambalo lina paa? Na pia je fenicha zako zitakaa juu ya sakafu laini ya udongo na majani au zitakaa juu ya sakafu ngumu? Hii itakusaidia kuchagua malighafi ambayo itaoana na mazingira yako.

Hakikisha kuwa ukikalia fenicha zako unapumzika vyema. Hata kama viti haviji na mito unaweza kutengenezesha mito yako mwenyewe na uwe unaihifadhi ndani majira ambayo hutumii fenicha za nje. Jaribu fenicha za nje kabla ya kununua na hata kuzilaza kwa jinsi ambayo ungetaka viwe kama vitanda vya mchana.

Yote hayo yakiwa yameshasemwa bajeti yako ndio itaamua ni nini unachoweza kununua. Siwezi nikasisitiza ni kwa namna gani ni muhimu kununua fenicha imara zaidi unazoweza kumudu. Kama uchumi unagomba, bado kuna namna unayoweza kupata fenicha za nje zilizo imara kwa hela uliyonayo. Unaweza kupata fenicha za nje nzuri na imara kwa bei nafuu kabisa kwa kununua zile zilizotumika. Fenicha zinazouzwa kwenye minada ya wafanyakazi wa kimataifa wanaomaliza muda wao na hivyo kurejea kwao, ukizifanyia maboresho kidogo na kuzisafisha zinaonekana kama mpya, na huwa hizi zinakuwa na ubora unaokubalika. Unaweza pia kufikiria kubadilisha mito na makusheni kwa ajili ya kuhuisha fenicha za nje za zamani.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com