Tuesday, September 20, 2016

Rangi hizi 8 za sofa hazitakuangusha

Sio siri kuwa kununua sofa ni hela nyingi. Kama utaweza kuchagua ya rangi sahihi ni kwamba hutajutia. Pamoja na changamoto unayoweza kukutana nayo wakati wa kuchagua rangi ushauri wangu ni kwamba chagua  ambayo haitakubana katika kupendezesha sebule yako.
Sofa ya kati ya rangi hizi zifuatazo itakupa wigo mpana wa kupendezesha ndani kwa
kukuwezesha kubadilisha yale mapamba madogomadogo kila unapohitaji kufanya hivyo.

Nyeupe
Sofa nyeupe haina kikomo cha muda. Pia unaweza kuongezea pambo la rangi yoyote unayotaka. Huu ni muonekano mmoja ambao kamwe hauchoshi. Sasa unaweza ukawa unajiuliza je utaiweza kuitunza kwa hiyo rangi yake? Malighafi ambazo sio moja kwa moja kitambaa ni rahisi kusafishika.

Nyeusi
Sofa nyeusi ni ongezeko muhimu kwenye sebule yoyote. Inafiti kwenye rangi na mitindo mbalimbali ya upambaji na inafanya iwe rahisi kuongeza mapambo sebuleni kwako kwasababu karibia kila kitu kinaendana na nyeusi.

Krimu
Krimu ni rangi nyingine pia inayokupa wigo mpana wa kupamba. Ni rangi ya kiwango inayooana na nyeusi, bluu, nyekundu au kijivu.

Biskuti
Ndio, ni rangi kama ya biskuti hizi hizi tunazokula ila sio zile nyeusi zenye chokoleti. Rangi ya biskuti iko kwenye kundi la rangi zisizoegemea kwenye upande wowote na inaoana vyema na bluu, nyeusi na nyekundu.

Udongo
Wengi wenu bila shaka mna sofa za rangi ya udongo kwasababu ndio imekuwa maarufu kwa miaka kadhaa ya nyuma. Changamoto ya rangi hii ni kuwa unaweza kujikuta kila kitu ni rangi ya udongo kuanzia kabati, meza na mapambo madogodogo kama vile mito, fremu za sanaa za picha pamoja na michoro ya ukutani. Rangi hii kwa sofa ni poa kama utaiepuka kwenye hivi vitu vingine. Pia kama una watoto ni rangi nzuri kwani inasaidia sana kuficha madoa.
Ila kwa siku za karibuni rangi ya udongo ni kama vile imewekwa kando baada ya kijivu kuonekana kuja kwa kasi na kuwa maarufu zaidi. Lakini bado sofa za rangi la udongo ni nzuri na mara zote zina muonekano wenye kiwango cha juu.

Kijivu
Sofa za kijivu zinaendana vyema na rangi asili ya mbao, pia nyeusi na nyeupe. Rangi ya kijivu kinashika kasi kubwa kwenye kupendezesha nyumba kwa sasa.

Rangi za asili
Rangi za asili kama vile kijani na bluu ya maji nazo zinatulia vizuri kwenye sofa. Kijani kinaendana vizuri na udongo, nyekundu, chungwa, zambarau na bluu. Sofa ya kijani haikubani kupamba na rangi nyingine.

Ngozi
Rangi ambazo pengine usingezipata kwenye malighafi nyingine za kutengenezezea sofa, unazipata kwenye ngozi.

Hakika rangi hizo hapo juu zinakuwezesha kupendezesha kwa urahisi pale unapotaka kubadilisha mapambo mengine madogomadogo. Kwenye fenicha kubwa kama sofa epuka rangi kali kama nyekundu na zambarau kwani zinaweza kukupa shida ya kuoanisha na mapambo mengine. Rangi kali za kuwaka zitumie kwenye vitupio kama mito, vitambaa, na sanaa za ukutani na za kwenye kabati la mapambo.

No comments:

Post a Comment