Friday, January 31, 2014

Friday, January 24, 2014

my article for newspaper: rangi za mazulia


Kupamba nyumba yako ni zaidi ya kuchagua rangi za kuta na aina ya fenicha — unatakiwa pia uchague rangi sahihi ya zulia.
Kuchagua rangi sahihi za mazulia kwa ajili ya nyumba yako sio uamuzi mdogo, mazulia ambayo utakaa nayo kwa miaka. Kwa ajili kuweka mazulia ni moja ya mapambo ya ndani yanayogharimu zaidi kimuda na kipesa. Kwa mfano si busara kutandika zulia la ukuta kwa ukuta ambalo unategemea kuondoa chini ya miaka mitatu. Kwanza si kazi ya kitoto kuanza kutoa vitu ndani kwa ajili ya kutanzika zulia la aina hii, na pili huwa zulia hili ni kubwa kwa hivyo pia ni gharama. Nimefanya mahojiana na Bi Aisha Idd ambaye anauza mazulia ya nyumbani kutaka kujua mambo ya kuzingatia kwa upande wa rangi wakati wa kununua mazulia ya nyumbani.
Bi Aisha anasema michoro na rangi za mazulia zinabadilika kila wakati kwa hivyo kwa ajili mazulia ni gharama, unatakiwa kuchagua yale ya rangi ambazo zitaoana na muonekano wa sasa ama mipango ya baadaye kama ipo juu ya nyumba yako. “Kwa kawaida rangi za mapambo ya sakafu huwa zinakuwa nyuma mwaka 1-2 kulinganisha na zile rangi za mitindo ya nguo, anasema Bi Aisha” Hii ina maana kwamba rangi maarufu zaidi kwenye maduka ya nguo za wanawake, zitaanza kuonekana kwenye sakafu za nyumba miaka kadhaa mbele. Upo hapo!
Kwa mazulia ya nyumbani ambazo zinaonekana zimepitwa na wakati kwa sasa ni rangi za dhahabu, kijani, silva, damu ya mzee na rangi ya udongo. Rangi zisizokolea au kwa maneno mengine rangi za mwanga kama vile bluu, khaki, kijivu na rangi ya maziwa zinaonekana kuwa maarufu zaidi kwa sasa. Hata hivyo hakuna rangi ambayo inashika kasi kwa sasa kama kijivu na khaki na wala haijalishi mabadiliko ya mara kwa mara ya rangi hizi. Aisha anasema labda ni kutokana na kuwa kuna jinsi nyingi ya kuoanisha rangi hizi mbili na vizulia vya kutupia.  
Sasa basi wakati wa kuchagua mazulia kwa ajili ya sakafu za nyumba yako zingatia mambo kadha wa kadha. Bahati nzuri ni kuwa vizulia vile vya kutupia baadhi ya maeneo vinakuja kwa bei, michoro na rangi lukuki ambapo ushindwe wewe tu. Kwa kweli sio ngumu kupata ukubwa na rangi unazotaka kwa uwezo ulio nao. Siku zote kumbuka kuwa uchaguzi wako wa mazulia ya nyubani kwa kila chumba ni msingi wa ladha yako.
Baadhi ya dondoo zifuatatzo zitakusaidia kuchagua rangi sahihi ya mazulia ya kwenye vyumba vya nyumba yako. Kwa kuwa zulia huwa ni la kudumu na kuweka la rangi fulani ni  uamuzi wa gharama kufanya, hapa ni dondoo chache za kukusaidia katika uamuzi huo mgumu.
Kwanza kabisa fahamu kuwa zulia ni moyo wa nyumba yako. Linatoa utambulisho wako hasa lile la sebuleni. Kwa vile mnachukua muda mwingi sebuleni kama familia, fikiria rangi ambayo inaenda kukubaliana na mfumo wa maisha yenu. Je sebule yako ni rasmi au ni ya kujimwaya mwaya?
Kuamua ni mazulia ya rangi ipi ununue, fahamu ni kwa kiasi gani yatakanyagwa. Zulia linavyozidi kukanyagwa ndivyo kuna uwezekano wa kuchafuka kwa maana ya kumwagikiwa vimiminika vilivyobebwa na wapitaji, madoa na majasho ya miguu. Mazulia ya rangi za mwanga kwa mfano khaki na kijivu huonyesha uchafu kirahisi lakini yanaweza kusafishika kwa dawa za kuondoa madoa kwenye mazulia ila kama mazulia yenyewe sio imara basi yataanza kuonyesha alama za uchakavu kwenye maeneo hayo ukiliinganisha na mazulia ya rangi za giza. Kama una wanyama wa ndani au sakafu ya nje ya nyumba isiyo ngumu ni rahisi mazulia yako kuchafuka kuliko yule anayeishi kwenye nyumba yenye mazingira ya nje yaliyowekwa sakafu ngumu. Familia nyingi haziweki zulia jikoni.
Fikiria matumizi ya eneo ambapo zulia litawekwa kabla ya kuamua rangi. Je unataka zulia lilete mwanga ama lipunguze mwanga chumba ambacho kina mwanga mkali zaidi? Nyekundu ni sahihi kwa vyumbani, sebuleni na kwenye ujia kwani haionyeshi madoa kwa hasira kama rangi za mwanga. Ila kwa vyumba ambavyo vina kiasi kikubwa cha mwanga wa jua fikiria juu ya zulia kuchuja, tatizo ambalo linaonyesha sana kwenye zulia za rangi za giza.
Kuchagua rangi kunahusika sana na vitu mbalimbali anbavyo vinahusika kwenye zulia hilo. Chagua rangi za giza kama kuna watoto wadogo ili kuficha yale madoa yasiyoepukika. Kama una wanyama wa ndani fikiria vitu kama tope wanaloweza kuingiza. Hata kama huhusiki na hivyo vyote basi fikiria hata sherehe na wale wageni ambao kwa vyovyote vile hawatainama kuvua viatu vyao!
Chagua rangi ya zulia itakayoendana na haiba na mazingira ya nyumbani kwako. Kwa mfano, kuna familia ambazo kuna sebule rasmi kwa ajili ya wageni tu na kuna nyingine ya  familia. Hii rasmi huenda kwa kawaida huwa na muonekano wa rangi za kifahari na rangi za mazulia yake huwa ni moja kwa mfano zulia la sakafu yote ya sebule rasmi yaweza kuwa ya rangi ya maziwa. Sasa kabla ya kuamua rangi ya zulia jiulize je unapenda kutembea kwenye chumba ambacho zulia lake lote ni la rangi moja tena ya mwanga?
Rangi za zulia utakazochagua zinahusiana vip na rangi za kuta na mapambo mengine hapo chumbani? Kila chumba kinahitaji sehemu moja ambayo ni kitovu. Zulia lako linaweza kuwa ndio kitovu, hautaki zulia lishindane na mapambo yako mengine kwa ajili chumba kinaweza kuonekana vurugu vurugu.
Shirikisha wanafamilia na chukua kura! Kwa ajili wote mnaenda kutumia mazulia haya, inaweza kuwa vyema kujua ni rangi zipi familia yako inaona zitafaa zaidi chumba fulani. Lete sampo nyumbani mshauriane pamoja. Huenda ukagundua rangi ambayo haukuwa umeiwaza mwanzo.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange.  Vivi ni mjasiriamali  upande wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Thursday, January 23, 2014

buriani Mhe. Bwa'mdogo; tuta miss biashara uliyokuwa unatupa

jana nilishtushwa kujua kuwa Marehemu Mheshimiwa Saidi Bwanamdogo kumbe ni aliyekuwa mteja wangu wa kufua nguo. toka nianze kufanya DC & Laundry sijawahi kupata biashara kubwa kwa wakati mmoja kama nilivyokuwa napata kwa Mheshimiwa Bwa'mdogo, kiasi kikubwa kabisa cha nguo alichowahi kuniletea ni kanzu 500. kwa mara ya kwanza alipokuja ofsini kwangu kama mteja nilimuuliza jina la kwenye risiti niandike nani? akaniambia Bwa'mdogo, nikadhania kama ananitania kwa ajili hata muonekano wake alioneekana mdogo mdogo nikadhani ndio maana kajiita hivyo; ila baada ya kifo chake jana nilipoona picha du! ndio nikajua kuwa lilikuwa jina lake rasmi. sikuwahi hata kufahamu kuwa alikuwa mbunge tena wa Chalinze. buriani Bwa'mdogo..you will be missed! 
Ian DC & Laundry

Monday, January 20, 2014

uzazi kweli kazi...

mwanakabumbu wangu akiandaliwa kwa ajili ya mechi ya alhamisi. kaniambia mechi yao inaitwa under 6 eti!

akiwa anajaribishwa gear kama zipo bomba
 yuko fit na ameahidi ushindi kwa timu yake
akionyesha atakavyolisakata kabumbu lenyewe

Saturday, January 18, 2014

Thursday, January 16, 2014

My article for newspaper: chumba cha kufulia


Eneo la kufulia liwe na muonekano na vifaa hivi.

Ni mara ngapi kwa juma ambazo unafua nguo? Familia ya watu wanne kwa mfano, inaweza kuwa inafua kati ya mara 3-4 kwa juma. Kwa maana hiyo ni vyema kuwa na chumba ama eneo maalum la kufulia nguo ambalo lina vitu muhimu vinavyotakikana kuwepo ili kufanikisha kwa haraka na kwa urahisi mchakato mzima wa kuondoa nguo kutoka kwenye uchafu hadi kuiweka katika hali ya kufaa kuvaliwa tena.

Asilimia kubwa ya kaya katika nchi zinazoendelea hakuna mahali au chumba maalum cha kufulia na badala yake hasa maeneo ya mijini mahali pa kufulia ni juu ya shimo la maji taka! Hii sio sawa kwa mfuaji kwani muda wote anaokuwa anafua pale anavuta hewa chafu inayotoka shimoni humo hivyo kuhatarisha afya. Kwa wenzetu walioendelea na baadhi ya familia katika nchi zinazoendelea, kwenye makazi yao wana chumba au eneo maalum la kufulia linalokidhi viwango vya vifaa na mahitaji. Si sawa kuwa na eneo tu la nje karibia na chanzo cha maji kwa ajili ya kufulia kwani kuna vitu muhimu ambavyo vinafanikisha zoezi la kufua na kwa kweli huwezi kuvihifadhi nje tu kwenye eneo hilo.

Eneo ama chumba cha kufulia kitafaa zaidi kikiwa kiko maeneo ya uani. Ili kuwa na eneo sahihi la kufulia ambalo utaokoa muda na nguvu zako na kukufanya uvutiwe na kazi hiyo fikiria shughuli zitakazofanyika hapo: kuchambua nguo, kufua, kukausha, kunyoosha, kutundika na kukunja. Weka mpangilio wa kuwezesha vifaa vyako viendane na mtiririko huo. Wala hutakiwi kuwa na eneo kuubwa kwa kazi hii, dogo liwavyo, eneo hili litawezesha nguo zitoke kwenye sinki iwapo unafua kwa mikono au kwenye mashine kwenda kukaushwa/kuanikwa, na kupelekwa meza ama kaunta ya kunyooshea na kukunjwa ama kutundikwa kuendana na hitaji la kila nguo.

Nchi yetu imejaaliwa kuwa kwenye ukanda wa jua la kutosha ambapo hatuna haja ya kuwa na mashine za kukaushia nguo. Rasilimali ya jua tuliyonayo inatutosha hatuhitaji kukausha kwa mashine za umeme. Kinachotakiwa tu ni kuwa na kamba za kukaushia karibia na mahali pako hapo pa kufulia.
Ni lazima kuwa na mahali pa kutundikia nguo zinazonyooshwa ambazo hazitakunjwa. Fimbo za kutundia mahali pa kufulia zinahusu. Fimbo hizi ziwe mbali kidogo na ukuta ili nguo zilizokwisha nyooshwa zisiuguse. Fimbo hizi ni za kutundika nguo kwa muda tu wakati wa kunyoosha kabla hasijasambazwa katika makabati ya nguo husika. Zile nguo zinazokunjwa baada ya kunyooshwa nazo zinahitajika mahali pa kuhifadhia kwa muda katika chumba cha kufulia kabla hazijasambazwa kwenye droo zinazohusika. Kwa maana hiyo pamoja na fimbo ya kutundikia, pia unahitaji kuwa na shelfu. Huu mpangilio ni kwa ajili ya kurahisisha mchakato wa kuondoa nguo kwenye kutoweza kuvalika kutokana na uchafu hadi kuiwezesha kuvalika tena; kwa hiyo ni kwa kaya yoyote na wala usidhanie ni maisha ya watu wa daraja fulani tu.
 Gawa sakafu ya eneo lako la kufulia katika maeneo mawili. Lile la maji maji kwa mfano kwenye sinki na lile kavu kwa mfano pale pa kunyooshea. Utajikuta hili eneo kavu halipati maji kabisa na waweza kupamba hata kwa kizulia. Kama una mashine ya kufulia weka upande sawa na wa sinki ili hata imuwie rahisi fundi bomba endapo kutakuwa na tatizo lolote kwani bomba zote zitakuwa eneo moja na kufanya zile shughuli za maji maji kuwa pamoja. Tenga la nguo chafu liwe jirani kwa ajili ya urahisi wa kubeba na kuweka kwenye mashine au kwenye sinki.
Eneo la kamba za kukaushia lisiwe mbali na panaponyooshewa ili iwe rahisi kuanua nguo na kupeleka moja kwa moja kwenye kaunta ya kunyooshea. Ili kutumia eneo dogo mara nyingi baadhi ya wenye nyumba wanapenda kujenga kaunta ya kunyooshea juu ya mashine ya kufulia. Inakuwa ni busara kutumia eneo hili la juu ya mashine badala ya kuliacha bure na badala yake kwenda kuweka kimeza cha kunyooshea kwingine. Na kwa bahati nzuri mashine za kufulia kwa ajili ya majumbani zina urefu chini kidogo ya meza ya kunyooshea kwa hivyo hakuna ubaya kujengea hii kaunta ya kunyooshea juu yake. Pia kaunta iliyojengwa kwa zege kwa ajili ya kunyooshea ni imara na inadumu maisha kulinganisha na meza.
Kuweka vifaa katika mpangilio kunarahisisha mambo. Kusanya sabuni na dawa zako zote za kufuli katika shelfu mojawapo ili kila kitu kiwe kwenye ncha ya vidole vyako pale unapokihitaji. Hakikisha baadhi ya madawa na blichi zinakuwa eneo la juu ambalo watoto wadogo hawawezi kufikia, kama vipi weka loki kabisa.  
Mahali pako pa kufulia pawe na mwanga wa kutosha. Mwanga mwingi wa asili ni mzuri zaidi hasa wakati wa kufua kwa mkono na kunyoosha. Mwanga pia unakuonyesha ndani ya mashine kukuridhisha kuwa hakuna nguo iliyosahaulika.
 Sakafu inayofaa bafuni na jikoni inafaa pia eneo la kufulia. Sakafu ya marumaru ni rahisi kusafisha, haipitishi maji na ikitokea kumwagika haiharibiwi na blichi.
Kufua haitakiwi kuwa kazi ya kuchukiza. Weka mpangilio huu mahali pako pa kufulia  na kamwe hutachukia mchakato mzima wa kufua na kunyoosha nguo.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

Tuesday, January 14, 2014

Venus ni mtu kama wewe


 wadau hii ni nyumba ya mwanatenis Venus Williams iliyoko sokoni huko Marekani. hapa nakuonyesha picha chache za vitu basic vinavyotakiwa walau viwe kwenye makazi ya binadamu. Of course V ni celebrity mkubwa ila na wewe unaweza kuwa na nyumba similar na hii ingawa ya kwako inaweza kuwa ndogo ya kawaida. kaza buti tutafika tu!
  eneo la mlango wa mbele. nimeyapenda mawe ya kukanyagia
 sebuleni hamna mbwembwe na ung'aro ung'aro wa kichina mwingi, sofa zake bomba, kimeza chake cha kahawa murua, TV yake ya ukutani superb na kizulia chenye mashiko
 eating area. umeona hiyo taa?
 jikoni kuna my favorite kizulia cha jikoni. eeh, unajua unasimama sana kuosha vyombo na shughuli nyingine za kwenye sinki kwa hivyo muhimu miguu kuburudika juu ya zulia.
 bedroom na ki bedside carpet chake
 sink la bafuni na ki medicine cabinet chake
taulo zimehifadhiwa hygienically


Thursday, January 2, 2014

My article for newspaper: malengo ya mwaka mpya



Ni wakati mwingine tena wa mwaka ambao wengi wetu wanapenda kufanya mabadiliko kwenye maisha yao. Je umeshafikiria mabadiliko ya mwaka mpya kwa ajili ya kiota chako? Japo mabadiliko haya yanajulikana na wengi zaidi kama maazimio, kwa kutia msisitizo zaidi makala hii itayaita malengo. Malengo yanatamkwa kwa kusisitiza wakati uliopo ni nini tamanio lako (kwa mfano kuamua kubadili mpangilio wa fenicha za sebuleni kwako ili kuwezesha kunogesha zaidi mazungumzo) wakati maazimio yanatamka ni nini ungependa huko mbeleni ya kuwa unaenda kufanya nini wakati ujao.
Mara nyingi malengo (au maazimio) ya mwaka mpya yanatupiliwa mbali hata kama nguvu za kutosha ziliwekwa ili kuhakikisha yanafanikiwa. Moja ya sababu za malengo kutofanikiwa ni mazingira ya nyumbani kwako kutosaidia kuwezesha mafanikio ya malengo hayo. Kama unataka kufanya mabadiliko ndani ya maisha yako bila kuhusisha mazingira yako kufanikiwa ni mbinde. Kwa maana ya kwamba kama unaweka malengo yako ya mwaka 2014 kwa ajili ya makazi yako na ukayaacha mazingira yalivyo, ni ngumu sana kubadili chochote. Hata matangazo kwa mfano ya kujikinga na maambukizi ya VVU yanaonyesha uhusiano kati ya maambukizi na mazingira fulani ambayo yanachochea maambukizi hayo.
Kanuni ya malengo kuwa na uhusiano na mazingira inahusika karibia katika kila kitu. Kama unataka mwaka huu uwe tofauti basi unatakiwa kuweka mazingira ya kuwezesha malengo yako.
Je mazingira yako yanakusaidia kupata kile unachokihitaji? Kwenye mazingira ya nyumbani kwako vitu ambavyo havijakaa mahali pake au vimekaa mahali ambapo havifanyi kazi yake au havitumiki tena vinakukwamisha kutimiza malengo yako hapo nyumbani. Tembelea kwenye makabati ya nguo na vyombo angalia kwa umakini kuona ni vitu gani vya kuhifadhi, vya kugawa ama vya kutupa. Fanya hivyo kwa nia ya kupata nafasi ya kile tu kitakachosaidia kufanikisha malengo yako.
Pengine lengo lako la mwaka mpya ni kutokula hovyo kwa nia ya kupungua uzito. Je mara zote unaingia nyumbani kwa kupitia mlango wa nyuma ambapo unaingilia moja kwa moja jikoni? Kumbuka kanuni kuwa unachokiona mwanzo kinagusa zaidi akili yako, kwa hiyo kama mara ungiapo ndani unakutana na jokufu, chakula na kadhalika utapata hamu ya kula hapo hapo. Tumia mlango wa mbele ambapo utaona kitu tofauti mara uingiapo ndani - kitu ambacho hakitakufikirisha kula.
Mahusiano mengi yanaweza kuboreshwa kwa mapambo ya nyumbani hasa katika swala la kuwasiliana. Je chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni mahali patakatifu kwa wawili? Hakikisha vitu kama taa, vimeza, na viti kwenye chumba hicho viko viwili viwili.
Au lengo lako mwaka huu ni kuwa na wageni wengi zaidi nyumbani? Hakikisha basi mlango wa mbele unaonekana na kuna njia ya wazi ya kuingilia. Taa zinazomulika njia ya kuelekea mlango huo ziwe zinafanya kazi. Pitia mlango wa mbele kama mgeni mtarajiwa uone kama kila kitu kiko sawa. Je njia hiyo inakaribisha? Na sebule yako je nayo inavutia kwa ajili ya wageni wako wengi ambao unapenda kuwaalika nyumbani mwaka huu?
Kwa wale ambao azimio lao kuu la mwaka 2014 ni kupamba nyumba zao hakikisha unachagua rangi kwa umakini, fikiria mpangilio wa fenicha je zinawatendea haki watumiaji wa chumba husika. Angalia vitu ambavyo inabidi uvifanyie kazi ili kuboresha muonekano wa makazi yako. Kama kwa mfano sakafu ya sebule yako ni ya marumaru na unachoka kusugua na kusafisha kila siku na unakiri kuwa ni ngumu kuifanya iwe safi; basi weka zulia kubwa ambapo utasafisha kwa mashine ya upepo mara mbili au tatu kwa wiki.
Ikiwa unaazimia kutojaza vyombo vichafu kwenye karo basi mwaka ujao lenga kuosha chombo mara baada ya kukitumia. Na hata hakikisha wanafamilia wengine pia wanafanya hivyo.
Huenda kijani kinakubariki lakini huna eneo kubwa ya kuweza kuwa na bustani za ardhini. Otesha basi bustani za kwenye vyungu walau ukifungua pazia la chumba cha kulala kunapopambazuka ukutane na kijani. Azimia kupamba ndani mwako kwa maua freshi japo mara moja kwa mwezi.
Kweli, baadhi ya mabadiliko ya nyumbani kwako unaweza kuhitaji kutafuta msaada, lakini kuna mabadiliko mengi sana ambayo hayahitaji gharama lakini yanahitaji muda na nguvu ( na pengine kautaalamu)  kwahiyo kwa 2014 kwa nini usiazimie kupamba mwenyewe? Unaonaje? Ni azimio moja zuri kwa ajili ya makazi yako ambalo unaweza kutekeleza. Fanya usafi mkubwa ndani ya nyumba yako mara moja kwa mwezi ( weka tarehe kwenye kalenda yako na isismamie). Mwanamke unatakiwa upende usafi na usiwe mvivu. Shirikisha na wanafamilia wengine pia.
Hii inaweza isikubalike kwa baadhi ya watu ila ni mawazo binafsi kuwa azimia kila anayeingia ndani avue viatu mlangoni. Viatu vya wanawake vilivyo na visigino vya ncha kali mara nyingine vinakwaruza sakafu za marumaru na mbao na kuacha alama na vile vya wanaume baadhi vina soli zinazoacha rangi sakafuni na hivyo kufanya sakafu ionekane zee kuliko kawaida.
Mwaka huu lenga kuweka nyumba yako nadhifu kila mara kama vile unategemea mgeni wa heshima!
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk