Thursday, July 31, 2014

my article for newspaper: kusafisha bafuni


Hakuna anayetaka kusafisha bafuni, lakini ukisafisha kila unapotumia, kazi inakuwa na maumivu kidogo kuliko kuacha hadi wakati wa usafi mkubwa. Makala hii itakujuza ni jinsi ya kuweka kuta, bafu, sinki, bomba, eneo la kuogea na bakuli la choo nadhifu kila wakati.
Unapoanza kusafisha bafuni, kwanza ondoa vitu vyote vya kuhamishika kama vile vizulia, tenga la nguo chafu, kimeza au kikabati na kindoo cha taka.
Hakikisha kuwa dirisha liko wazi ili hewa ipite kuondoa hewa nzito.

Baada ya hapo ondoa buibui kwenye kona za dari ikifuatiwa na kufuta vumbi mlango kwa nje na ndani. Kwa ujumla wakati wa kusafisha chumba anzia juu kushuka chini. Ruhusu taka za vumbi na buibui zimwagike sakafuni kwa ajili utasafisha mwishoni. Kitambaa cha kufutia kinafaa sana kwa kazi hii japo pia waweza kutumia fagio.

Mimina blichi ama sabuni za kusafishia kwenye bakuli la choo na iache iondoe uchafu taratibu.

Weka dawa ya unga wa kusafishia zile sehemu ambazo zina uchafu. Kama kuna uchafu umejijenga kwenye lile eneo la kuogea, sinki ama pembeni na bomba weka unga wa kusafishia halafu sugua taratibu kwa brashi. Ukiacha unga huu ukae kati ya dakika 10 hadi 15 wakati ukifanya jambo jingine itaruhusu kulainisha uchafu. Hakikisha unasoma maelezo ya dawa ya kusafishia ili kuwa na uhakika unatumia kiasi sahihi ambacho hakitaharibu maeneo yako. Pia ni vyema kujaribu dawa eneo dogo kabla ya kusafishia eneo kubwa.

Paka sabuni au dawa nyingine za kusafishia kwenye kuta za bafu kama ni za marumaru. Kwa kutumia sponji ama brashi sugua sehemu uliyoweka sabuni. Isuuze vizuri kuondoa michirizi yoyote michafu na kama ukuta ni wa karibia na sinki ama bakuli la choo ukaushe kwa taulo. Ukuta wa sehemu ya kuogea unaweza kuuacha bila kuukausha. Ni vyema kuvaa glovu wakati wa kusugua kwani baadhi ya madawa na sabuni zinaweza kuchubua ngozi.

Safisha bomba la kuogea ambalo sio siri kuwa wasafishajiwengi huwa hawakumbuki kusafisha. Bomba inatumika tu kusafishia kwingine ila yenyewe inasahaulika kusafishwa. Ni kama msemo wa mshumaa kujiunguza kumulikia wengine! Kwa sababu hiyo utakuta kwenye bomba na vichwa vyake kunakuwa na uchafu wa sabuni zilizogandian. Hali huu huweza ikasababisha makazi ya vijidudu.

Pazia la bafuni huwa linaandamwa na ukungu eneo linalogusana na sakafu. Ni vizuri zaidi ukalifungua na kulifua kwenye maji ya moto kwa kiasi kidogo cha sabuni na blichi. Kumbuka adui nambari moja wa ukungu ni blichi. Kiasi kidogo kitaondoa uchafu bila hata kusugua.

Angalia eneo la sinki na sugua mabaki ya sabuni na dawa za mswaki kwa sabuni kidogo pamoja na sponji au brashi. Mswaki wa zamani unaweza kutumika kuondoa uchafu kutoka eneo la kati  ya bomba na mishikio yake. Kuwa makini kuwa brashi la kusugulia bakuli la choo lisitumike kusugulia  sinki. Hii inaweza kusambaza maradhi kwa kuruhusu vijidudu vya kwenye choo kuingia kwenye sinki la mswaki. Kuzuia hali hii isitokee, brashi la bakuli la choo liwe la peke yake. Ni muhimu kutumia blichi kusafishia bafuni ili kusaidia kuua vijidudu.

Safisha kioo kwa kutumia ama maji na taulo au dawa ya kusafishia vioo na taulo.

Safisha nje ya choo ukianza na ile sehemu ya juu ya kuvuta maji, taratibu endelea kusafisha eneo lote la nje ya choo ambalo ni pamoja na mfuniko na eneo la chini ya pale pa kukalia na futa kwa taulo. Kumbuka kitaulo hiki kimetengwa kwa kusafishia choo pekee.
Sugua ndani ya bakuli la choo kwa brashi yake halafu vuta maji. Huna haja ya kusugua kwa nguvu nyingi. Acha sabuni na dawa ya kusafishia ikufanyia kazi hiyo.

Sasa ni wakati wa kusafisha sakafu ukinanzia na zile sehemu zilizojifisha hadi zile za wazi. Safisha mavumbi yote na uchafu wote ulio chini na pale eneo la choo lilipounganika na sakafu. Eneo hili kwa kawaida huwa ni chafu sana na lile bomba la nyuma linajaa mavumbi. Malizia kwa kusuuza kwa maji masafi kuondoa sabuni itakayoweza kubaki na kusababisha utelezi.

Subiri kidogo sakafu ikauke ndipo urudishe vile vitu ulivyoondoa awali.
Ili kuweka bafu lako katika hali ya usafi na kupunguza kutumia nguvu kubwa ya kusafisha unatakiwa uwe unasafisha maeneo mbalimbali ya bafu mara baada ya kuyatumia. Kwa mfano safisha bakuli la choo kila baada ya kulitumia, vile vile eneo la kuogea pamoja na sinki. Hata kama sehemu hizi hazionekani kuchafuka safisha tu kwani madini yaliyoko kwenye maji nayo yaweza kufanya alama. Kama utafanya hivi, usafi mkubwa utakuwa na maumivu kidogo kwani uchafu hautakuwa umejijenga.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Thursday, July 24, 2014

my article for newspaper: mpangilio wa chumba cha kulala

Chumba chako cha kulala ni sehemu ambayo unalala, kwahivyo ni muhimu pawe katika mazingira ya kupumzikia. Wakati huohuo unataka pawe eneo la kufanyia shughuli mbalimbali zinazotakikana kufanyikia hapo kwa mfano kujiandaa kwa ajili ya kutoka asubuhi. Jinsi ambavyo fenicha zimepangwa italeta matokeo chanya au hasi kwa mazingira ya chumba chako cha kulala. Kitanda ni fenicha nambari moja kwa chumba chochote cha kulala na kwa asili ndio kitovu cha jicho linakotazama.

Vyumba vya kulala vinavyotumika na watu wa kundi fulani vina mahitaji ya kipekee kwa kundi hilo. Iwe unapanga chumba cha kulala cha wakuu wa familia, cha mgeni au cha watoto makala hii itakupa dondoo za jinsi unavyoweza kupangilia.

Iwapo unapanga chumba cha kulala cha wakuu wa familia (kumbuka kuwa chumba hiki sio lazima kiwe ni kikubwa zaidi kama wengi wanavyodhani) kinachotakiwa tu ni kuwa na vifaa muhimu vinavyohitajika mule. Na kama chumba chako ni kidogo zaidi ya ambavyo ungependa, fikiria mbinu za kukifanya kiwe kikubwa kama vile kuondoa mrundikano na kuweka fenicha, pazia na malazi yenye rangi za mwanga kwani zinafanya chumba kionekane kikubwa.

Tukiachana na ukubwa wa chumba cha kulala cha wakuu wa familia, dondoo hizi zitakusaidia kukifanya kiwe sehemu bora zaidi ya mapumziko. Weka vimeza vya pembeni mwa kitanda vyenye ukubwa wa kuendana na eneo lako. Kama unatazama luninga ukiwa kitandani utagundua kuwa vimeza hivi vitakusaidia. Tafuta eneo japo kwa kiti kimoja au viwili vya kukalia. Viti vinasaidia sana siku ya ugonjwa, kupumzika mchana au wakati wa kusoma. Fikiria kuweka zulia sakafu yote ya chumba hiki ili kuondoa kelele za fenicha na nyayo kwenye chumba. Kama una nafasi si mbaya kuweka deski kwa ajili ya kukaa na kuandika chochote.

Kwa upande wa watoto wanaoingia kwenye rika la ujana huwa wanajua ni nini wanachotaka kwenye chumba chao cha kulala, na hawachelewi kukuambia wewe mzazi au mlezi wanahitaji sehemu ya kuhifadhia vitabu na muziki ama eneo lao lingine la kuhifadhia vitu vyao vingine vyovyote unavyoweza kudhani.Wana mawazo yao kuhusu mpangilio na rangi, kwa hiyo waulize!

Pilika nyingi zaidi ya kuperuzi mitandao na burudani zinafanyika kwenye chumba cha kulala cha watoto wa rika hili la kuingia kwenye ujana. Viti vya ziada na vimeza vitawezesha eneo la wageni wao. Weka fenicha zitakazotumika na rahisi kutunza.

Vyumba vya kulala vya watoto wadogo viwekwe fenicha kwa kufikiria miaka yao ijayo. Ila mwanzoni, hakikisha unaweka eneo la kuwabadilishia karibia na kitanda. Kwenye chumba hiki hakikisha usalama unapewa kipaumbele. Usiweke kitanda karibia na dirisha kama dirisha hilo linafunguliwa mara kwa mara. Mara nyingi kuweka kitanda katikati kama chumba kina nafasi kubwa huwa ndio mpangilio mzuri zaidi.  Ila kama nyumba yako ina viyoyozi na madirisha hayahitajiki kufunguliwa basi unaweza kuweka kitanda chini ya dirisha.

Hakikisha mtoto hawezi kuanguka toka kitandani. Hakikisha droo za chumba hiki ni laini kufunga, kwa mfano endapo mtoto atakuwa amefungua kwa bahati mbaya basi reli zitateleza zenyewe na droo kufunga. Zikiwa ni droo ngumu kufunga mtoto anaweza akanyanuka droo ikiwa wazi na kona yake ikamtoboa kichwani. Vitasa vya milango na mikono ya makabati visiwe na ncha kali kwenye chumba hiki. Ikiwezekana funika swichi za umeme na nyaya zisisambae sakafuni.

Kuwa na chumba cha mgeni kunamfanya mgeni wako kuwa huru zaidi ugenini na hata wewe mwenyeji wake. Unaweza kupanga chumba cha kulala cha mgeni kwa kitanda sahihi na vifaa vinavyohitajika na kukisahau. Hakikisha kuwa mgeni wako ana sehemu ya kutosha ya kuhifadhia, seti mbili za shuka, mito na komfota au kava la duveti.

Kwa kufanya haya utakuwa umeweka mpangilio wa kufaa kwa kila chumba cha kulala kwa watu wa kada mbalimbali walioko ndani ya familia yako.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

--vitu vizuri-- urembo wa Tanga stone kwenye nguzo

Tanga stone kwa vile yanatokea Tanga...yanaweza kukatwa ukubwa unaolingana ama unaweza kuyatumia bila kuyakata. Pia unaweza kuyaongezea urembo kwa kuya polish. Jiwe hili la asili limewashika sana WaTZ  na wasio na kuwa maarufu sana kwenye majengo mengi nchini.


Friday, July 18, 2014

Thursday, July 17, 2014

my article for newspaper: kung'arisha nguo nyeupe

Jinsi ya kung’arisha nguo nyeupe

Sababu kadhaa zinaweza kufanya nguo nyeupe zipoteze weupe wake. Huenda utafuata kanuni za utunzaji wa nguo nyeupe, lakini bado zinaweza kubadilika na kuwa na rangi ya njano baada ya muda. Unjano mara nyingi unatokea kwenye nguo ambazo hazijahifadhiwa vizuri kwa kugusana na mbao au bodi za kabati.

Haiepukiki kuwa baada ya muda nguo hupata udongo na kuanza kuonyesha uchakavu. Nguo nyeupe ni chambo cha madoa, na madoa hayo huonekana zaidi ya nguo yenyewe. Habari njema ni kuwa nguo nyeupe hata iwe imendamwa na madoa kwa kiasi gani, bado inaweza kuokolewa.

Soma makala ifuatayo ambapo Aisha Idd ambaye ni mtaalam wa kufua anatujuza namna tunavyoweza kurudisha tena uhai wa nguo nyeupe. Anasema kuna njia kadhaa za kuweza kuzing’arisha tena. Baadhi ya njia zinaweza kuharibu vitambaa laini kwa hivyo kuwa makini.

Unatakiwa kufua nguo nyeupe mara kwa mara. Madoa yanavyokaa kipindi kifupi, ndivyo ilivyo rahisi kuyaondoa. Hii hasa inahusu kwa njano ya kikwapa itokanayo na kutokwa jasho na deodoranti. Weka dawa ya kuondoa madoa kwenye maeneo haya na mengine yenye madoa kabla ya kufua nguo nzima.

Njia ya kwanza na iliyozoeleka na wengi ya kung’arisha nguo nyeupe ni kuweka blichi wakati wa kufua. Blichi ya klorini inashauriwa kutumika zaidi kwa kipimo kilichoelekezwa kwenye chupa na kwenye nguo za pamba. Itumie tu kwa nguo nyeupe na ambazo zinaruhusu blichi. “Hakikisha unasoma lebo ya nguo kabla ya kuamua kutumia njia fulani ya kuing’arisha,” anasema Aisha. Kuna nguo hata kama ni nyeupe ila lebo yake inasema usitumie blichi.
Pia blichi ikizidi inaweza kuharibu nguo na wakati mwingine kuleta mistari ya njano kwenye nguo nyeupe kwa hiyo kuwa makini na kiasi cha blichi kinachotakiwa kuchanganywa na maji. Wakati mwingine yapasa kuloweka nguo zako kwenye maji yenye blichi kwa usiku mzima.

Unaweza kuweka rangi ya bluu kwenye maji ya kusuuzia ili kufanya nguo zako nyeupe zing’ae.  Unachotakiwa ni kufuata maelekezo kwenye chupa ya bluu. Bluu inaongeza ubluu kwenye nguo ambao unaifanya ionekane nyeupe zaidi na ing’ae. Bluu inatakiwa kuwekwa na maji ya baridi.

Kuanika nguo nyeupe zikauke juani ni njia mojawapo pia ya kuzingarisha. Kwenye jua kuna mionzi ya UV ambayo inafanya nguo nyeupe izidi kuwa nyeupe, anasema Bi Aisha. Bila shaka! Mwanga wa jua ni zana mojawapo kuu ya asili tuliyonayo ya kufanya nguo nyeupe zizidi kuwa nyeupe bila kutumia kemikali.

Vinega; ndio vinega hii hii unayoifahamu pamoja na sabuni yako ya kufulia vitang’arisha nguo zako nyeupe. Vinega ni kilainishi na marashi ya nguo, hii inawekwa kwenye maji wakati wa kusuuza. Usijali harufu kwani nguo zako hazitanukia kama vinegar bali harufu itapotea juani wakati wa kukaushwa.Vinega hii nyeupe pia inasaidia kuondoa mabaki ya sabuni kwenye nguo. Onyo: Kamwe usichanganye vinega na blichi kwani inafanya kemikali hatari kwa nguo zako, anasema Aisha.

Juisi ya ndimu ni njia nyingine ya asili ya kung’arisha nguo nyeupe. Weka nusu kikombe cha chai na sabuni kwenye maji ya kufulia (hata kama unafua kwa mashine) na endelea kufua nguo nyeupe kama kawaida. Itumie tu kwenye nguo nyeupe kwani inaweza kuharibu nguo za rangi.

Magadi soda (Baking Soda) nayo inaleta matokeo ya ajabu kwenye kung’arisha nguo nyeupe bila kutumia blichi. Hii pia weka nusu kikombe cha chai pamoja na sabuni yako ya kufulia. Nguo zitatoka nyeupe na zitang’aa kuliko.  Usishange hii ni moja ya viambato kwenye dawa za meno, ni kwa ajili ya kuongeza weupe.

Hizo hapo juu ni njia mbalimbali za kufanya nguo nyeupe ziwe nyeupe zaidi. Zingatia kuchagua sabuni za kufulia ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya kung’arisha na zitumie mara kwa mara kwa matokeo mazuri. Fua nguo nyeupe kwa maji ya baridi ili kufanya madoa na unjano usizame na kung’angania zaidi kwenye nyuzi za nguo. Usichanganye njia moja na nyingine pamoja kwani unaweza kutengeneza kemikali itakayoharibu nguo zako.

Kwa hivyo kwa matokeo mazuri, fua nguo zako nyeupe kwa sabuni za kawaida za kufulia ukiongeza moja ya njia za kung’arisha hapo juu tulizojuzwa na Bi Aisha. Halafu tundika nguo zikauke juani. Utashangazwa ni kwa namna gani zimeng’aa. Bottom of Form


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Tuesday, July 15, 2014

housekeeping: jinsi ya chap chap ya kusafisha pavers

Vitofali vya paving zaidi ya kuongeza mvuto kwenye landscape ya makazi yako, pia vinaleta muonekano wa uimara na usafi wa eneo iwe ni drive way, au njia ya miguu au uani. Vyovyote vile unavyotumia vitofali hivi kuendana na mahali ulipoviweka huwa vinachafuka na kuonekana kuchakaa hasa pale gari zinapoingia na tairi zenye tope na pia mimea ya mosi inayoota maeneo ya kati ya kitofali kimoja na chenzake pale masika inapofuliliza. Sasa basi njia za chap chap za kurudisha mvuto ni kuvisafisha ama kwa mashine ya presha au kama hauna mashine hiyo waweza kukwangua kule katikati ya kitofali kimoja na kingine (kwenye vifereji) ili kuondoa ukungu (mosi) wanaokuwa wameota na baada ya hapo ukafagia kwa mfagio mgumu na mpira wa maji. 

Kufanya hivi hasa baada ya masika kunafanya vitofali vyako ving'a e tena na kuingia kwenye kiangazi free of makoko. Endapo hutafanya hivyo (kusafisha kuondoa hayo makoko), kiangazi kinapotinga baada ya masika jua linayakausha na kutoka yenyewe na ndipo huleta sura mbovu kwenye vitofali. Kwa hivyo vifaa utakavyohitaji endapo huna pressure washer ni mpira wa bustani, kisu cha kukwangulia, na mfagio mgumu. Dondoo hii ni ya kusafsha chap chap bila gharama kubwa ili kurudisha landscape yako kwenye mvuto wa awali.

Friday, July 11, 2014

housekeeping: kisulisuli kimepamba moto

kwakweli upepo wa kipupwe hiki umetisha. Kwa wanaoacha milango wazi, kwa kipindi hiki ni bora tuu kuifunga kwani mavumbi yanajaa ndani na kwa wenye miti inayododosha ukifagia ama kuokota baada ya nusu saa ni vululuvlulu kila mahali.
 mti huu inaitwa Dodoma tree, huwa ni kijani kipindi chote cha mwaka. inadondosha majani machache mno hata pamoja na kisulisuli hiki.
Dodoma tree inafaa sana kuoteshwa eneo unalotaka lifunge na unaweza kuielekeza utakavyo. Kwa mfano unaweza kuikatia urefu fulani ili isiende juu zaidi au kuicha ikawa mikubwa kabisa, yote hayo ni wewe tu na jinsi roho yako ilivyopenda. Kama uko karibia na barabara vumbi, dodoma tree inasaidia kudaka vumbi lote na pia mizizi yake huwa ni midogo sana kiasi kwamba haipasui kuta nyufa. Ukiiotesha hutajuta, inapatikana kila mahali kwenye bustani za maua ila kuwa makini usibambikiwe. Ukishafanya hivyo urudi kunishukuru kwa desa!

rafiki yangu wa ukweli apanda udzungwa

ha ha haaa...mambo ya schoo trip haya. Mwalimu wake ananiambia kajitahidi kupanda mlima kilomita 3 hadi Udzungwa falls! Akirudi kitambi chote kitakuwa kimeyeyuka nadhani...



Monday, July 7, 2014

vitu vizuri: vizulia vya katani

bibi Pili ni mtaalam wa kutengeneza vizulia vizuri mno vya katani. leo nimemtembelea nijionee namna vitu hivi vizuri vinavyotengenezwa na matumizi yake ndani ya nyumba. karibu msomaji ujionee...
nikiianza safari

kizulia cha katani hicho bi Pili amekanyagia akitupa desa

vizulia vya rangi mbalimbali kwa ladha ya mteja

doormat ya mkonge hiyo...mwisho wa matumizi yake ni mwisho wa ubunifu wako


hii unaweza kuitumia kama bedside..ni mchanganyiko wa nyuzi za katani na za pamba

mwanzoni chote kinakuwa cheupe kwa ajili ndio rangi halisi ya katani. rangi watia baadaye ukipenda

hapa kizulia cha katani kimetumika kutengenezea mgongo wa kiti cha uvivu

kwenye karakana


nikajipatia kimoja nikakitupia jikoni kama hivi. nikiwa napika taratiibu miguu inatekenywa

Thursday, July 3, 2014

my article for newspaper: kutandika kitanda

Jinsi ya kutandika kitanda ili kionekane nadhifu na maridadi

Linaweza kuonekana ni jambo rahisi ila kufahamu mbinu za kutandika kitanda kionekane nadhifu na maridadi ni faida ya kila mmoja iwe ni mtu wa umri mdogo au wa makamo na awe ni mwanaume au mwanamke. Kuwa na kitanda kilichotandikwa vyema sio tu kinaonekana nadhifu, bali pia unajisikia vizuri wakati ukifunua shuka kwa ajili ya kulala usiku. Kitanda nadhifu kinaleta burudiko la moyo vilevile, kwa ajili kinaleta hisia ya utulivu na muonekano wa kuwa na mapangilio chumbani. Kitanda kilichotandikwa nadhifu pia, ni nadra kuanza kuhangaika kupanga shuka wakati wa kulala na hii inamaanisha amani zaidi na muda mchache wa kupambana na shuka na blanketi.

Awali ya yote ondoa malazi yote ( shuka na blanketi au komfota) pamoja na mito kitandani. Chukua shuka safi ambazo zinafiti ukubwa wa kitanda chako. Kama shuka zako ni zile za seti ya shuka moja ya kufitisha (hii ni ile yenye mipira kwenye kona zake) na ya pili ni flati (haina mipira), basi chukua hii ya mipira na ifitishe kwenye kona nne za godoro. Shuka hizi za kufitisha zinarahisisha sana utandikaji wa kitanda hasa kama saizi ya shuka na godoro ni sawasawa. Huna haja ya kunyoosha kusawazisha mikunjo kwani huwa inajisawazisha yenyewe ukishavalisha kwenye kona za godoro. Kama ni saizi sawa na godoro itafiti vizuri kabisa.

Baada ya hapo juu ya shuka ya kwanza tandaza ya pili ambayo ni ile flati kwa jinsi ambayo upande wenye pindo kubwa unakuwa kichwani na ule wa pindo dogo unakua miguuni. Hakikisha shuka hii inaning’inia ukubwa sawa kwenye pande zote za kitanda ikifuatiwa na kuichomekea kwenye godoro sehemu za miguuni wakati maeneo la kichawani na pembeni yakiachwa bila kuchomekewa.

Tandaza blanketi juu ya shuka ya flati ukilinyoosha vizuri kwa kadri unavyosogea. Ruhusu urefu kiasi wa blanketi kwa ajili ya kuchomekea miguuni. Kunja blanketi eneo la kichwani ukiwa umelishikisha pamoja na lile shuka la flati urefu wa saizi ya upana wa mto mkubwa wa kitandani. Baada ya kukunja chomekea kwa pamoja blanketi na shuka kwenye pande mbili ndefu za kitanda.Kama kitanda kinatumika kila siku utandikaji huu ni njia rahisi kwa mlalaji kufunua upande anaopandia kitandani, shuka ya juu iliyokunjiwa na blanketi na kuingia kitandani kulala. Ila kama kitanda husika hakitumiki mara kwa mara, kwa mfano kama ni kitanda cha chumba cha mgeni unaweza kufunika  kwa kuchomekea kote kote na juu yake kuweka kava la kuzuia vumbi hadi mgeni atakapotembelea.

Sasa basi endapo kitanda tunachotandika ni kwa ajili ya matumizi ya kila siku njia ya kukunja shuka na blanketi ni utandikaji utakaofaa zaidi. Eneo la kichwani mahali ambapo pamekunjiwa blanketi, lile shuka la kufitisha litakuwa linaonekana kwa hivyo chukua mito na weka juu yake.  Huenda unahitaji mito miwili tu kwa ajili ya kulalia, ila unaweza kuongeza mito kadhaa midogo midogo kama mapambo kukipa kitanda mvuto.Unaweza kuweka mito mitano hadi sita kuendana na ukubwa wa kitanda chako. Kanuni ya kuweka mito kitandani ni kuwa lile eneo la kichwani lisibaki na uwazi wa ukubwa wa mto. Kwa maana ya kwamba kama kuna uwazi wa kutosha mto uliobakia basi ongeza mto. Kwa mmoja namna hii ya utandikaji inaweza kuwa mwisho na akajiridhisha kitanda kimekamilika na kina mvuto, ila kwa mwingine anaweza kupenda kuongezea komfota.

Kwa hivyo kama wewe ni mmoja wa wanaopenda kutandika komfota kitandani basi litandaze juu ya blanketi huku ukilinyoosha vizuri kuondoa mikunjo yote inayoweza kutokeza. Huna haja ya kuchomekea komfota na huwa lenyewe ni njia mojawapo ya kupamba kitanda – liache tu likining’inia urefu unaolingana kwenye pande zote za kitanda na hapo kitanda kinakuwa kimemalizika kutandikwa.

Kuna baadhi yetu ambao hatuoni umuhimu wa shuka ya pili. Uzoefu wa kutumia shuka moja (ikiwa ni ile ya kufitisha ni bora zaidi) na komfota pekee inafanya utandikaji wa kila siku wa kitanda uwe rahisi, ila kiukweli ni kuwa hii shuka ya pili inaulinda mwili wa mlalaji usikwaruzwe na ugumu wa blanketi au komfota na pia husaidia kuweka blanketi au komfota safi na bila kusahau kuongezea mwili joto. Ni rahisi zaidi kufua shuka mara kwa mara kuliko blanketi au komfota, na pia makava haya ya kitanda yanadumu zaidi yakifuliwa mara chache.

Kutumia shuka ya flati ambayo ina ukubwa wa kutosha inafanya kitanda kiwe rahisi kulalia na kutandika tena asubuhi ya pili. Tumia shuka na blanketi zenye ukubwa wa kutosha kiasi kwamba havitachomoka chomoka ukiwa umelala. Kama una blanketi dogo ni bora kulikunja na kuliweka chini ya mito na ukawa unalikunjua na kujifunika wakati wa kulala tu kwa maana ya kwamba wakati wa kutandika unalikunja kwani ukiamua kuchomekea blanketi dogo litakusumbua kwa kuchomoka kila mara.

Zaidi ya kutandika safisha chumba chako cha kulala ili kuonyesha zile juhudi zako za kutandika. Kitanda pekee kikiwa maridadi ilhali sehemu ya chumba iliyobaki ni mrundikano unadhifu hauwezi kuonekana. Kutandika kitanda kunakuwezesha kuanza siku yako vizuri na kunakufanya ujiikie kuwa na mpandilio zaidi mapema mwa siku yako.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Tuesday, July 1, 2014

usiruhusu magugu kushamiri yaharibu bustani yako...

ukiona kote kijani kwa undani magugu yamejificha

muhimu kuyang'olea kwani yakishamiri yataharibu bustani

unaona kama hiyo ndago hapo kati ilivyotulia

magugu yote kwenye ndoo kwa ajili ya kutupiliwa mbali

gugu majani yake ni mapana zaidi

majani bila gugu