Friday, June 27, 2014

fabulous friday

ha ha haaa...tunamalizia mchakamchaka wa mitihani...



Thursday, June 19, 2014

my article for newspaper: Jinsi ya uchaguzi , uhifadhi na utunzaji wa visu vya jikoni

Jinsi ya kuchagua, kuhifadhi na kutunza visu vyako vya jikoni

Visu ni vifaa muhimu zaidi jikoni. Kwanza tuangalie muonekano wa jumla wa kisu kinachofaa jikoni ambacho tunaweza kukiita ni kisu cha mpishi. Kisu hiki ni kile ambacho walau unakitumia kwa kila shughuli unayofanya hapo jikoni. Ni muhimu sana kufahamu urefu na upana endapo utakuwa unataka kununa kisu hiki. Kisu cha mpishi kina urefu wa kati ya inchi 8 hadi 12 na upana wa kati ya inchi 1 ½ hadi 2.

Kisu cha mpishi kikiwa na urefu huu wa inchi 8 ni mwake kwa matumizi mengi tofauti tofauti kwani kikiwa kirefu sana huenda usiweze kutumia ncha yake vizuri. Mkono wa kisu cha mpishi unaweza kuwa umetengenezwa kwa vifaa na miundo mbalimbali. Vifaa na miundo ya aina fulani ni rahisi kushikika mkononi kuliko aina nyingine. Mikono mingine ya visu hivi inaweza kuwa inateleza wakati wa kukata chakula na hivyo kuleta usumbufu kwako. Sasa haya yote yakiwa yameshasemwa, basi ni juu yako kuchagua kisu cha mpishi ambacho utajisikia huru, burudani na rahisi kwako wewe mpishi kukitumia. Unajua jinsi panavyokuwa na visu kadhaa jikoni lakini unakuwa na kimoja ambacho unakipenda zaidi kwa maana ya kwamba unaona kinakufaa zaidi kwa matumizi.

Unapaswa kuwa na kati ya visu 3-5 jikoni kwako. Aina hizi tofauti tofauti zinapatikana kwenye seti ya visu. Hakikisha unachunguza kwa makini aina ya visu iliyopo kwenye seti endapo utakuwa unanunua kwa seti. Mara nyingi utakuta kule kwenye seti kuna aina ya kisu ambacho utakitumia mara chache sana ua hata labda hutakitumia kabisa. Kama ni hivyo basi ni bora kunua kimoja kimoja badala ya seti. Hata hivyo, faida mojawapo ya kununua visu kwa seti ni kuwa unapata na kihifadhio chake ambacho unaweza kutunzia visu vyako.

Kama unafanya kazi nyingi na nyama yenye mifupa au samaki wazima wazima basi fikiria kuwa na kisu kile ambacho sehemu ya kukatia ni kama msumeno kwa ajili ya kupenya kwenye mifupa na kingine kilicho laini kwa ajili ya kukatia minofu iliyotenganishwa toka kwenye mifupa.
Usalama na usahihi wa kuhifadhi visu vyako ni jambo la muhimu mno unalopaswa kuzingatia. Visu vikali kamwe visihifadhiwe vimesambaa  kwenye droo la kabati la jikoni vikiwa vinagongana na vyombo vingine kwa sababu kuu mbili:

Kwanza ni hatari kuingiza mkono wako kwenye droo kuchukua kisu kwani kinaweza kukukata, na pili msuguano wa visu na vyombo vingine kwenye droo vinaweza kusababisha visu kuwa butu.
Kitufe cha kuhifadhia visu au kipande cha sumaku kilichowekwa ukutani ni njia sahihi zaidi za kuhifadhi visu vyako vya jikoni. Kama hauna eneo la kaunta kwa ajili ya kuwekea kitufe cha visu au labda hauna ukuta kwa ajili ya kuwekea hiki kipande cha sumaku basi kwenye droo pekee ndio mahali unapoweza kuhifadhi visu vyako. Yaani droo liwe ni chaguo la mwisho baada ya kitufe na sumaku kushindikana. Kwa hali hii inabidi uwe na zuio la visu ukiwa umevalisha kwenye kila kisu au droo la mbao liliogawanywa visehemu vidogo dogo  ndani kwa ajili ya kila kisu kuhifadhiwa kwenye kisehemu chake.

Kwa hivyo tumeona kwamba utunzaji wa visu unaenda sambamba na uhifadhi sahihi. Visu vinatakiwa kusafishwa kwa mikono na kufutwa kabla ya kuhifadhiwa. Kwa vyovyote vile kisu chochote kitahitajika kunolewa baada ya kipindi fulani. Unaweza kufanya shughuli hii kwa kumshirikisha mtaalam. Baadhi ya wataalam huwa wanapita mitaani na baiskeli wakiwa wamebeba mashine zao za kunolea huku wakitangaza wananoa visu.Vinginevyo unaweza kuamua kufanya kazi ya kunoa visu vyako mwenyewe nyumbani. Kama utaamua kufanya mwenyewe basi kifaa kingine cha kufikiria ni hicho cha kunoa visu vyako. Wengine huwa hata na jiwe la kunokea visu ambalo linatumia ama mafuta au maji kama kilainishi wakati wa kunoa. Lakini aina nyingine za vinoleo vinavyouzwa madukani havihitaji vilainishi na vinoleo hivi ni rahisi zaidi kutumia kuliko jiwe.

Natumai umejifunza jambo kuhusu ununuzi, matumizi na uhifadhi wa visu vyako vya jikoni. Tukutane tena wiki ijayo.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Thursday, June 12, 2014

my article for newspaper: jinsi ya kutunza na kusafisha godoro

Kila mmoja anapenda usingizi wake, na tunategemea godoro kutupatia mahali safi na nyororo pa kulala. Ni nini kinafanyika pale godoro lako linapokuwa chafu? Ni kwa namna gani unazuia mavumbi na wadudu kuweka makao kwenye godoro lako na kukubughudhi na usingizi wako? Ni ratiba gani ya matunzo na usafi godoro inahitaji?

Kama inavyofahamika kwamba binadamu anatumia theluthi moja ya maisha yake akiwa amelaza mwili mlalo na tena wengi wetu juu ya godoro, basi ungetegemea kwamba kusafisha godoro ingekuwa ni orodha namba moja kati ya vitu vinavyopewa kipaumbele kwenye orodha ya kusafisha, lakini utashangaa wala siyo. Ni mara chache tunafikiria juu ya kusafisha godoro.

Tatizo ni kuwa, unaondoa shuka zote, unabakiwa na godoro ambalo limeshionewa foronya ambayo huwezi kuivua sio – kama vile kuna zipu unayoweza tu ukafungua kirahisi ukavua foronya na kwenda kuifua – hapana, ukweli wa masikitiko ni kuwa – wakati tunatoa shuka zote, tunakuwa kama tumeziba macho kwa uchafu mwingine wowote uliopo juu ya godoro lenyewe.

Godoro linaweza kuhifadhi uchafu wa vimiminika, madoa, vumbi na mbaya zaidi hata wadudu kama chawa na kunguni  – kwahivyo kuwa na godoro safi ni muhimu kwa sababu kadhaa zaidi ya kufahamu kuwa mwili ambao umevalishwa nusu unalilalia kukiwa na shuka pekee iliyotenganisha mwili huo na godoro.

Kusafisha godoro kwa mashine ya kunyonya vumbi ni muhimu kwa ajili ya kuondoa vumbi, seli za ngozi zilizokufa na uchafu mwingine unaotua kwenye godoro lako na ambao unajilimbikiza kadri muda unavyokwenda. Fikiria kusafisha godoro kwa namna hii kwa walau mara mbili kwa mwaka. Sasa kumbuka kuwa kwa vile mashine hii ya kusafishia kwa upepo ina vichwa kadhaa, utapaswa kutumia kile kichwa cha kusafishia viti na sio kile cha kawaida cha kusafishia zulia kwa huwa kinazoa kila aina ya uchafu kwa hivyo usingependa kukipitisha hicho kwenye godoro lako. Wakati wa kusafisha godoro ni vyema kusafisha pia mvunguni.

Vile vile kila baada ya miezi sita iwe ni wakati wa kugeuza godoro lako juu kwenda chini na miguuni kwenda kichwani. Fikiria kwa mfano mwenzi wako na wewe mna zaidi ya kilo mia, kwa hivyo kwa kugeuza na kuzungusha godoro inamaanisha kuwa mnaongeza uhai wake na kuleta uwiano wa uchakavu . Kulingana na ukubwa wa godoro, hii kwa kirahisi kabisa inaweza kuwa kazi ya watu wawili.

Madoa kama ya mapatapishi, jasho, damu, mkojo na vimiminika vingine toka mwilini huwa kuna wakati vinatua kwenye godoro. Kama ilivyo ada kwa doa lolote, ni vyema kulichangamkia liondoke mapema kabla halijakomaa zaidi. Madoa ya vimiminika yanatakiwa kwanza yafutwe kwa maji baridi, na kitambaa chenye unyevu. Na baadaye unyevu wa ziada unakaushwa na kitambaa kikavu. Kumbuka kufuta kwa kukandamiza badala ya kuzungusha mduara ili kuondoa uwezekano wa kuchana kitambaa cha godoro. Madoa haya ya viminika toka mwilini asili yake ni protini kwa hivyo tumia maji ya baridi pekee wakati wa kuondoa madoa haya.

Funika godoro lako kwa foronya ya kuvulika ili kulinda maeneo ya godoro. Chagua foronya ambayo inaosheka kirahisi ambayo ni rahisi kuvalisha na kuvua kwenye godoro lako. Foronya nyingine zimebuniwa maalum kwa kazi ya kuzuia kushika vumbi kwa hivyo kukupunguzia kazi ya kunyonya godoro vumbi mara kwa mara.

Kama maeneo ya godoro yamepatwa na tope au udongo ondoa kwa shampoo ya kusafishia sofa na mazulia. Safisha tu lile eneo lililochafuka kwa kutumia sponji. Suuza eneo hilo kwa sponji jingine la maji ya moto na kandamiza eneo hilo kwa kitambaa kikavu ili kunyonya unyevu. Unaweza kuruhusu eneo hilo kukauka kwa kuwasha feni au hata kutoa godoro nje kwenye jua kali. Usiruhusu maji kuzama sana ndani kwenye kiini cha godoro kwani maji na godoro sio marafiki.

Endapo godoro litakuwa makazi ya wadudu kama chawa na kunguni jambo hili si dogo eti wadudu hawa waondolewe tu na watu hapo nyumbani ambao sio wataalam wa kazi hii. Changamka mapema na mwite mtaalam. Watakusafishia na kupuliza dawa godoro lako chumba, na hata maeneo mengine ya makazi yako ambayo yatakuwa yamedhurika na wadudu hawa. Kama umefikiwa na wadudu hawa unataka waondoke na wataalam wanajua jinsi ya kufanya kazi yao.

Hongera kwa kuwa na dogoro safi ambalo litadumu muda mrefu!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Thursday, June 5, 2014

my article for newspaper: bustani za kwenye vyungu

Mwongozo wa bustani za maua za kwenye vyungu
Hata kama una eneo dogo kiasi gani lakini unapenda bustani za maua, unaweza ukatimiza tamanio lako hilo kwa kutengeneza bustani za maua za kwenye vyungu.
Au pengine labda una eneo la kutosha kuwa na bustani ya ardhini lakini bado kuna yale maeneo kama ukutani, ndani ya nyumba au kwenye varanda ambapo ungependa kuwa na maua, basi suluhisho ni bustani za kwenye vyungu.

Bustani hizi zinakuwezesha kutengeneza bustani maalum kwa ajili ya eneo lolote. Unaweza kuotesha humo maua yako ya upendeleo ambayo usingependa kuotesha kwenye eneo kubwa la bustani ya ardhini kwani labda yatamezwa na mimea mingine iliyopo kwenye bustani husika. Mtunza bustani wa bustani za kwenye vyungu kikomo chake ni ubunifu wake pekee, anasema landscaper Aisha Idd.

Kwenye makala hii bi Aisha atatufunza jinsi ya kuchagua vyombo vya kuoteshea, uwekaji wa mbolea, udongo na umwagiliaji wa bustani zako bila kusahau maua yanayofaa kuotesha kwenye vyungu na mengine mengi!
Baadhi ya vyombo vinavyoweza kutumika kwenye bustani za kwenye vyungu ni vyungu vidogo vya kuning’iniza na vile vikubwa vya kuweka chini pamoja na maboksi ya mbao.                                                                                                                                       

Aisha anatupa mwongozo wa namna ya kuchagua vyungu kwa ajili ya bustani yako hiyo. Anasema epuka vyungu vyenye midomo myembamba. Pia vyungu vya plastiki nyembamba sana vinaweza kuharibiwa na jua na vitafanya ua lililoko ndani kukaukiwa na maji mara kwa mara. Kama utachagua vyungu vya udongo fahamu kuwa udongo unapitisha maji hivyo kiasi cha mji kitakuwa kinapotea kupitia kuta za chungu. Vyungu vya seramiki na saruji ndio vizuri zaidi kwenye kuhifadhi maji ila vinatakiwa kuwa na matundu kadhaa.                                                                                                                                    

Maboksi ya mbao huenda yakaoza, mbao nyekundu na za aina ya cedar huwa haziozi na zinaweza kutumika bila tatizo. Maboksi ya mbao zilizowekwa dawa ya kuzuia kuoza au kuliwa na wadudu si mazuri kwani kemikali zlizopo kwenye dawa hizo huwa zinaweza kuunguza maua. Uzuri wa mabokisi ya mbao ya kuoteshea maua ni kuwa yanaweza kutengenezwa kwa umbo na ukubwa utakaofiti eneo linalohitajika kuwekwa.

Vyungu viwe na ukubwa wa wastani kwani vikiwa vidogo sana vitazuia mizizi ya mmea kutambaa vizuri na pia huwa vinakauka maji mapema sana. Ukubwa na idadi ya mimea inayooteshwa itatokana na ukubwa wa chungu kitakachotumika. Maua yenye mizizi inayoenda chini inahitaji vyungu virefu. Hakikisha kuwa vyungu vyako vinapitisha maji vizuri na tandika magazeti chini ili kuzuia udongo usiwe unakimbia chungu wakati wa kukimwagilia. Sasa utajiuliza hayo magazeti si yataloa? Ni kweli ila hata kama yakiloa yatatengeneza kizuizi chini kwani hama tujuavyo ni kuwa karatasi haiozi. Kwa upande wa vyungu vidogo vya kuning’iniza hakikisha ya kuwa hutundiki kwenye ukuta wenye jua la moja kwa moja kwani vitakuwa vinakaukiwa maji mara kwa mara.

Hakikisha kuwa chombo chako cha kuoteshea bustani za kwenye vyungu kinapitisha maji mapema lakini kinahifadhi unyevu wa kutosha kuweka mizizi katika hali ya maji. Mboji inafanya udongo mzuri sana wa kwenye vyungu. Ila ni muhimu kujua hitaji la mmea kwani usijezidisha udongo wenye mbolea kali, na pia mbolea nyingine kama ya kuku ina tindikali sana kwahivyo inahitaji maji kwa wingi pindi unapoiweka. Kadri utakavyokuwa unamwagilia mmea wako ndivyo utkavyokuwa unaweka mbolea kwani huwa maji yanaondoa baadhi ya vimeng’enyo. Pia kuna mbolea za dukani za maji maji ambazo waweza tumia kwa kupata maelezo ya kitaalam toka kwa wauzaji.

Umwagiliaji wa bustani yako ya kwenye vyungu ufanyike pale mmea unapohitaji maji kwa maana ya ikiwa dalili za hali ya kunyong’onyea zitaanza kujitokeza. Baadhi ya mimea inaweza kuvumilia na inahitaji ukame kiasi kwamba ukiimwagilia mara kwa mara unaisababishia kuwa na unyevu wakati wote kwa maana hiyo itakufa. Ielewe mimea uliyo nayo, anasema Aisha. Kuna mimea mingine ya kwenye vyungu kwa mfano, kama iko ndani ya nyumba inaweza kumwagiliwa vikombe viwili tu kwa juma zima. Kumwagilia kuwe ni hitaji na sio jambo la kila wakati na kanuni kuu ya kujua kuwa mmea unahitaji maji ni kujaribu udongo wake. Kama inchi moja au zaidi ya udongo ni mkavu basi mwagilia.

Kwenye mazingira ya uwazi, mimea ya kwenye vyungu inapoteza maji mapema. Wakati wa kiangazi bustani zilizowekwa kwenye mazingira haya huenda zikahitaji kumwagiliwa kila siku.   Sasa basi, ni muhimu kufahamu kuwa sio kila maua au mmea unafaa kuoteshwa kwenye vyungu. Mimea inayokubalika zaidi kwa bustani hizi ni ile yenye mizizi michache na mifupi. Pindi uendapo kwenye bustani za wauza maua zilizojaa maeneo mengi kando kando ya barabara kuu watakufahamisha.                             

Umaarufu wa bustani za kwenye vyungu umetisha.

Mimea kwenye vyungu inaonekana kila mahali, kutoka kwenye makazi ya watu hadi maofisini, mahotelini, kwenye ma mall na hata barabarani. Udongo mbaya au hakuna eneo la kuweka bustani sio kisingizio tena cha kutokuweza kufurahia kijiraha cha kuwa na bustani!

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk