Tuesday, May 24, 2016

Mambo matano ya kuzingatia ili friji lako lifanye kazi vizuri na kwa miaka mingi

Bila shaka unaponunua jokofu, unategemea lifanye kazi vizuri kwa miaka mingi ijayo. Hata hivyo ili jokofu lako liweze kutimiza matarajio hayo, hupaswi kuliacha tu bila utunzaji.  Njia sahii za utunzaji zitasaidia kifaa hiki kufanya kazi bila matatizo na kwa muda mrefu. Tupate ujuzi ufuatao
toka kwa mtalam wa majokofu bwana Hafiz Ali kama ifuatavyo:

Lipe nafasi za kupumua
Jokufu lako linahitaji nafasi za kutolea hewa ili liweze kufanya kazi vizuri. Kama umeweka jokofu likakabana moja kwa moja na ukuta lazima lifanye kazi ya ziada kuweka vyakula vyako baridi, ambapo halikutengenezwa kufanya kazi hiyo ya nyongeza. Wakati unapochagua mahali pa kuweka jokofu hakikisha angalau kuna nafasi wazi ya inchi mbili kila upande. Hii kwa upande wa nje na ni la kuzingatia sana hasa yale majiko ambayo yameshajengewa tayari eneo la kuwekea jokofu. Kwa upande wa ndani hakikisha kuwa hauhifadhi humo vyakula kwa mtindo wa vitu vikubwa na vilivyoshikana bila kuachiana nafasi.

Safisha koili za nje
Ni bahati mbaya kuwa pamoja na walio wengi kusafisha majokofu yao vizuri sana kwa ndani na milango kwa nje, wengi wetu tunasahau nyuma ya jokofu. Ambapo ndio kuna zile koili zinazosaidia kufanya chakula kibaki na ubaridi kwa sababu koili hizi zinaondoa joto toka ndani ya jokofu na friza. Kutegemea na muundo wa jokofu zipo koili zilizo nyuma au chini na ni rahisi kwa vumbi na chembechembe za  uchafu kujishika humo baada ya muda. Uchafu huu unasababisha jokofu kuongeza msukomo wa kazi yake ambapo inapelekea kulichosha na kusababisha matengenezo ya gharama.

Uzuri ni kwamba kusafisha koili  za nje ya jokofu ni hatua rahisi ya utunzaji wake ambayo unaweza tu kuifanya wewe mwenyewe. Zima jokofu, livute mbali na ukuta na tumia ufagilio wenye brashi laini kusafisha. Mavumbi yote yatadondoka sakafuni ambapo utasafisha sakafu baadaye. Fanya hivi kila baada ya miezi 6 kusaidia jokofu lako kufanya kazi vizuri.

Mipira ya milangoni iwe inakaba
Ili jokofu liweze kufanya kazi vizuri na pia matumizi mazuri ya nishati, milango yake inatakiwa iwe inabana kabisa. Milangoni mwa jokofu kuna mpira ambayo huwa unakuwa dhaifu baada ya muda. Inapotokea hivyo hewa ya nje ambayo ina joto inapenya na kuingia ndani ya jokofu, na kulisababishia kufanya kazi ya nyongeza kuondoa hilo joto la ziada. Hii inamaanisha bili kubwa za umeme na pia jokofu kuchakaa mapema.

Kuisaidia mipira ya milangoni idumu, uwe unaisafisha baada ya kipindi kwa sabuni na maji. Kama unahisi imeanza kudhoofika fanya jaribio jepesi: Kungua mlango uufikishe nusu halafu uachie polepole ujifunge wenzewe. Kama haubani vizuri basi tayari mpira umeanza kuchoka. Habari njema ni kwamba mipira ya spea ipo na sio bei kubwa na vilevile kuibandika upya ni rahisi tu.

Liyeyushe kila baada ya kipindi
Kama jokofu lako ni moja ya matoleo mapya utakuwa una bahati kwamba halijengi barafu ndani (non frost) na huna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu dondoo hii ya utunzaji. Ila kama ni la zamani kidogo, bila shaka una hii kadhia ya barafu kujaa ndani.
Barafu zinazojitenga katika koili zilizo ndani ya jokofu zinalilazimisha kufanya kazi ya nyongeza ili kubaki katika ubaridi unaotakiwa.

Barafu inapojijenga hadi inchi moja na nusu ni wakati wa kuyeyusha jokofu. Zima umeme, ondoa vyakula vyote, acha milango wazi na acha kifaa kiyeyuke. Endapo hujalitoa nje ya nyumba, unaweza kubeba mabonge ya barafu kadiri yanavyojiachia na kuweka kwenye chombo ili kuepuka maji wengi kujaa ndani. Mara barafu yote inapoyeyka, mwaga na kausha mashelfu yaliyojikusanya maji, washa jokofu na rudishia vyakula vyako.


Nifuate instagram @ vivimachange

No comments:

Post a Comment